Habari

Yanga Yalalamikia Kuvurugwa kwa Mipango Yake ya Ubingwa

Kama kuna bingwa kaandaliwa basi apewe kombe tujue moja - Yanga

Kunyemelewa na watani zao wa Jadi Klabu ya simba katika msimamo wa ligi kuu soka Tanzania bara ndio mzimu unaoutesa Klabu ya Yanga kwa hivi sasa wakati ambapo baadhi ya mashabiki wameonekana kuutupia lawama uongozi wa klabu hiyo kwa kutochukua hatua za mapema kuzuia Janga hilo.

Matokeo ya sare katika mechi mbili mfululizo walizozipata Yanga katika michezo yao ya Ligi Kuu Bara yamewaibua viongozi wa timu hiyo ambao wamezitupia lawama mamlaka za soka nchini wakidai kuwa zinahusika moja kwa moja na upatikanaji wa matokeo hayo 

Akizungumzia shutma hizo katika mkutano na waandishi wa habari,  Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Fredrick Mwakalebela amesema, kwa sasa timu yao haitendewi haki na mamlaka zote zinazosimamia soka, kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Kamati ya Waamuzi pamoja na Kamati ya saa 72.

Mwakalebela amelalamikia matukio yaliyojitokeza katika mchezo wa Klabu hiyo dhidi ya Mbeya City na kudai kuwa walinyimwa penati mbili za wazi ambazo walistaili kuzipata na zingepelekea wao kushinda mchezo huo na sio kupata pointi moja.

Mwakalebela pia amelalamikia mchezo wa timu huyo dhidi ya  Kagera sugar akidai kuwa walinyimwa penati ambazo zingewafanya kupata pointi tatu badala ya kupata moja, huku akidai kuwa mamlaka husika  kuna timu inayoandaliwa kuwa bingwa.

"Kama kuna bingwa kaandaliwa basi apewe kombe tujue moja, tunatarajia kamati husika zitatoa maamuzi katika hizo mechi zetu mbili na hao waamuzi wachukuliwe hatua stahiki tusitolewe kwenye mstari wetu wa kutwaa ubingwa msimu huu," amesisitiza Mwakalebela.

Mwakalebela amesema, Yanga wametumia gharama kubwa kuiandaa timu hiyo hivyo namna matukio yanayotokea na kufumbiwa macho na vyombo husika yanawafanya kutafsiri vibaya juu yao.

Hatahivyo baadhi ya wafuatilizi wa masuala ya soka nchini wanasema kuwa ni haki ya msingi kwa vilabu kuhoji ubora wa uendeshwaji wa ligi kuu pale inapohitajika lakini lazima malalamiko hayo yawe na mantiki na uhalisia. Gharib Mzinga mchambuzi wa masuala ya soka nchini anasema kuwa mwamuzi kuchezesha chini ya kiwango ni suala ambalo hutokea katika mchezo na waamuzi huadhibiwa kupitia kamati husika ya waamuzi

Kimsingi suala la performance ya waamuzi kuwa ndogo ni suala la kitaifa hilo sote tunalifahamu, lakini isionekane tu ni upande mmoja wao ndio wanaonewa peke yao hapana" amesema Mzinga. 

Yanga ambao kwasasa ni vinara katika msimamo wa ligi kuu soka Tanzania Bara wanatàrajiwa kuingia Dimbani leo kuzisaka pointi tatu nyingine dhidi ya klabu ya Mtibwa sugar kutoka Mkoani Mororgoro.