
Jeshi la Polisi Tanzania limetoa ripoti ya hali ya usalama nchini Tanzania kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2020. Katika ripoti hiyo iliyotolewa Disemba 21, 2020 Jeshi la Polisi limeainisha matukio mbalimbali ya kiusalama yaliyojiri kwa kipindi hicho na kufanya ulinganisho wa hali kwa mwaka 2019.
Akisoma ripoti hiyo kwa wanahabari, Kamishna wa
Operesheni na Mafunzo ya Jeshi la Polisi, CP Liberatus Sabas amesema, kwa
ujumla hali ya usalama nchini imeimarika ikilinganishwa na mwaka 2019. CP Sabas
amesema kuimarika kwa hali kumetokana na juhudi za Jeshi la Polisi kwa
kushirikiana na vyombo vingine vya usalama na wananchi ambao wamekuwa wakitoa
taarifa na kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo katika kupambana na uhalifu.
“Kutokana na ushirikiano mzuri baina ya Jeshi la Polisi
na vyombo vingine vya usalama pamoja na wananchi, Jeshi la Polisi limefanikiwa
kupunguza matukio makubwa ya kihalifu ambayo yalikuwa ni kero kubwa kwa
wananchi ikiwemo makosa ya unyang’anyi kwa kutumia silaha, makosa ya mauaji na
ajali za barabarani.” - amesema CP
Sabas.
Akizungumzia matukio ya mauaji, amesema ripoti ya Jeshi
la Polisi inaonesha kwamba kwa ujumla mauaji yamepungua lakini matukio mengi ya
mauaji yaliyoripotiwa yametokana na wivu wa mapenzi, imani za kishirikina na
matukio ya kujichukulia sheria mkononi. Kwa mujibu wa CP Sabas mauaji
yanayotokana na wivu wa mapenzi yameongoza mwaka 2020.
Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania inayoandaliwa na
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) inaonesha kwa kipindi cha mwaka
2019, kulikuwa na matukio 105 ya watu kujiua kwa kujinyonga, matukio 8 ya
kujiua kwa kunywa sumu na matukio 2 ya kujiua kwa kujipiga risasi. Kwa mujibu
wa ripoti hiyo sababu kubwa ya watu kujiua ni pamoja na wivu wa kimapenzi.
Ripoti ya LHRC inaonesha pia kwamba matukio mengi ya mauaji yanayotokana na
wivu wa mapenzi huwakumba wanawake kwani jumla ya matukio nane (8) kati ya
matukio 12 ya mauaji dhidi ya wanawake yalitokana na wivu wa mapenzi.
Tafiti mbalimbali za afya zinaonesha sababu kubwa ya
mauaji hasa kwa wivu wa mapenzi ni watu kushindwa kukabiliana na tatizo la afya
ya akili. Mara nyingi wapenzi wanapohisi au kuona hali isiyo ya kawaida kwenye
mahusiano yao hushindwa kutawala hisia zao na kujikuta wanafanya uhalifu wa
kudhuru na hata kuua kinyume cha sheria.
Jeshi la polisi limesisitiza kwamba njia ya kukabiliana
na aina hii ya mauaji yanayotokana na wivu wa kimapenzi ni kutoa elimu kwa
jamii hasa kwa kushirikisha wadau muhimu ikiwemo viongozi wa dini.
Leave a comment