Afrika

Watanzania Wawili Wafanya Vizuri Tuzo Za Kimataifa za Kalahari

Watanzania wawili, Dotto Rangimoto na Mpolenkile Noel wamefanya vizuri katika Tuzo za Kimataifa za Kalahari Short Story Competition zinazotolewa na CENE Littéraire Association. Rangimoto ameshika nafasi ya pili, Mpolenkile ameshika nafasi ya tatu, huku nafasi ya kwanza ikienda kwa Mkenya Igunza Mwanatunzi.

 

Mwezi Mei CENE Littéraire Association walizindua Msimu wa Kwanza wa Mashindano ya Kimataifa ya Hadithi Fupi kwa waandishi ambao bado hawajapata kuchapa vitabu vya hadithi.  Mashindano hayo yalipokea washiriki kutoka katika lugha za Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa. Washindi wa lugha ya Kiswahili walitangazwa Desemba 7, 2020.

 

Majaji wa mashindano haya kwa upande wa lugha ya Kiswahili ni Dkt Neema George Mturo ambaye ni Mhadhiri mzoefu wa somo la Fasihi ya Kiswahili na Isimu kwa upande wa Semantiki na Pragmatiki ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira; Lello Mmassy ambaye ni mchumi mwenye Shahada katika Maendeleo ya Uchumi aliyohitimu kutoka Chuo Kikuu Cha Mwalimu Nyerere na pia Mshindi wa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika kupitia riwaya yake ya Mimi na Rais; jaji mwingine ni Elias Mutani ambaye ni mwandishi wa riwaya na vitabu vingine, mhariri, mfasiri na mchapishaji kutoka Bagamoyo.

 

Hadithi iliyompa tuzo Igunza Mwanatunzi inaitwa Donda la Ukabila. Wakati iliyompa ushindi wa pili Dotto Rangimoto inaitwa Mama Yuko Wapi na iliyompa ushindi wa tatu Mpolenkile inaitwa Maumivu Makali. Mshindi wa kwanza atapatiwa kiasi cha Euro 1,000, mshindi wa pili atapatiwa Euro 500 na yule wa tatu atapatiwa Euro 300.

 

Akizungumza na Serengeti Post, miongoni mwa Majaji wa Tuzo hizo ambaye pia ni Mwandishi, Bw. Lello Mmassy amesema kuwa mpango huo wa tuzo ni mzuri na utawasaidia waandishi wadogo kuchipukia, na kufahamika zaidi.

 

‘’Kama miongoni mwa Majaji katika Tuzo za Kimataifa za Kalahari Short Story Competition zinazotolewa na CENE Littéraire Association nimefurahi kuona mwamko wa watanzania kushiriki kwa kuwasilisha hadithi zao. Tuzo hizi ni ni muhimu kwani zitawasaidia waandishi wanaochipukia kupata hadhira pana zaidi kwa kazi zao’’, Lello amesema.

 

Itakumbukwa kuwa, tuzo hizi ni mara ya kwanza kujumuisha fasihi ya Kiswahili. Hata hivyo, waandaaji wamesema kuwa mwamko wa waandishi ulikuwa wa kuridhisha ikizingatiwa ilikuwa ni msimu wa kwanza. Tuzo hizo zilitangazwa Mwezi Mei na uwasilishaji ulihitimishwa mwezi Agosti 2020 huku washindi wakitangazwa mwezi Disemba mwaka huu.