
Washindi wa kwanza wa Tuzo za Kidigitali (Tanzania Digital Awards) mwaka 2020 wametangazwa rasmi baada ya watanzania kupiga kura. Jumla ya wawania tuzo 50 wameibuka washindi katika jumla ya vipengele 50 kutoka katika makundi tisa ikiwemo kundi la Serikali Mtandaoni, Maendeleo na Diplomasia Mtandaoni, Masoko Mtandao, Burudani Mtandaoni, Vyombo vya Habari Mtandaoni, Uvumbuzi wa Kidijitali, Mawasiliano ya Kidijitali, Uchechemuzi Mtandaoni na Tuzo ya Ujumla ya Chaguo la Watu.
Tuzo hizi ambazo zimeanzishwa na kampuni ya Serengeti Bytes zilizinduliwa nchini Tanzania mnamo Januari 16, 2020 kwa lengo la kutambua juhudi za watu binafsi, mashirika, kampuni na hata Serikali katika kutumia teknolojia ya kidigitali kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Baadhi ya walioshinda vipengele vingi ni pamoja na Diamond Platnumz ambaye ameshinda vipengele vitatu ikiwemo kipengele cha Tuzo ya Ujumla, Msanii bora wa mwaka na mraghibishi wa mwaka. Millard Ayo pia ametwaa tuzo tatu, tuzo ya kiongozi bora wa vyombo vya habari vya mtandaoni, TV bora ya Mtandaoni na Blog bora ya Mtandaoni.
Taasisi zilizonyakua tuzo nyingi ni pamoja na Ubongo Kids na Idara ya Uhamiaji –kila mmoja tuzo mbili. Ubongo Kids wametwaa tuzo tuzo ya ukurasa bora wa elimu mtandaoni na tuzo ya aplikesheni bora ya elimu mtandaoni. Idara ya Uhamiaji wametwaa tuzo ya uvumbuzi bora kupitia huduma yao ya kutoa hati ya kusafiria kielektroniki. Uhamiaji pia wameshinda tuzo ya taasisi bora ya Serikali mtandaoni.
Vodacom Tanzania imeibuka na tuzo mbili baada ya aplikesheni yake ya M-PESA kuzawadiwa kama Aplikesheni Bora ya Huduma za Kifedha. Tuzo nyingine iliyoenda kwa Vodacom ni tuzo ya Kampeni Bora ya Masoko Mtandaoni ambapo Vodacom wameshinda kupitia kampeni yake ya ‘Yajayo Yanafurahisha’.
Tuzo ya heshima imekwenda kwa Muhidin Issa Michuzi ambaye ametambuliwa kama kiongozi bora wa vyombo vya habari mtandaoni kwa kuanzisha na kuendeleza vyombo vya habari kwa njia ya mtandao nchini Tanzania.
Akizungumza baada kutangaza orodha ya washindi, Mkuu wa Programu, Utafiti na Uvumbuzi wa Serengeti Bytes, Ndugu Genos Martin amesema kwa kiasi kikubwa tuzo hizi ziliathiriwa na mlipuko wa Covid-19 uliojitokeza mara baada ya kuzinduliwa kwa tuzo hizo. Hata hivyo, Martin anakiri kwamba Covid-19 kwa kiasi fulani imesaidia kuweka msisitizo wa namna ambavyo teknolojia za kidijitali haziepukiki katika maisha ya sasa na hivyo kufanya tuzo za Tanzania Digital Awards kuwa na maana zaidi.
‘’Mara baada ya kutangaza tuzo hizi kwa mara ya kwanza mwezi Januari tulipata mwitikio mkubwa sana wa watu na makampuni na hata taasisi za serikali na wadau wengine kujitokeza kushiriki. Kuingia kwa mlipuko wa Covid-19 nchini kumeathiri kwa kiasi kikubwa maandalizi ya tuzo hizi. Hata hivyo, Corona haijaharibu pekee bali kwa upande mwingine imeonesha wadau na hata sisi waandaaji kwamba matumzizi ya teknolojia za kidigitali ndio mtindo mpya wa maisha hivyo tuzo hizi zimekuja wakati sahihi na kila mmoja anapaswa kuziunga mkono”. – amesema Martin.
Akizungumzia kuhusu washindi, Martin amesema washindi wote wa tuzo za Tanzania Digital Awards wamestahili kushinda hasa kwa kutazama mambo makubwa wanayoyafanya kupitia majukwaa ya kidigitali. Martin amefafanua kwamba mwakani tuzo hizo zitatanuliwa zaidi kuhakikisha watu wengi zaidi wanashiriki na kila sekta inaguswa kwa lengo la kuchochea ubunifu na uvumbuzi katika kukuza maendeleo ya teknolojia za digitali nchini Tanzania.
“Tunawapongeza washindi wote kwa kupigiwa kura nyingi katika vipangele walivyowania, washindi wote wamestahili ushindi kwa kutazama juhudi zao katika majukwaa ya kidigitali. Tunaamini ushindi wao utachochea ubunifu na uvumbuzi katika kutatua changamoto mbalimbali katika jamii na taifa kwa ujumla. Katika tuzo zijazo tutahakikisha wadau wengi zaidi wa teknolojia za kidigitali kutoka katika sekta zote wanapata taarifa na kushiriki kikamilifu”. Amesema Martin.
Tuzo za Tanzania Digital Awards zilizundiliwa rasmi Januari 16, 2020 kwa lengo la kuwatambua watu, taasisi na kampuni zinazotumia teknolojia za kidigitali kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Tanzania Digital Awards zinalenga kuchagiza Uwajibikaji, Ubunifu na Uvumbuzi kwenye majukwaa ya Dijitali. Zikiwa katika Makundi tisa na zaidi ya vipengele vidogo 50, tuzo hizi ni za kwanza na kubwa zaidi kutambua juhudi zinazofanyika ili kuleta mapinduzi ya kidijitali Tanzania na nje ya mipaka.
Katika msimu wa kwanza, yalifanyika mapendekezo ya wawania tuzo zaidi ya 54, 034 huku kura zaidi ya 100,000 zikipigwa katika vipengele 50.
Serengeti Post tumekuwekea hapa orodha kamili ya washindi wa Tanzania Digital Awards:
BURUDANI MTANDAONI
Mwanamichezo bora
- Mbwana Samatta
Mchekeshaji bora wa kike
- Mama Nairo
Mchekeshaji bora wa kiume
· Joti
Mwanamuziki bora wa kiume
- Diamond Platnumz
Mwanamuziki bora wa kike
· Nandy
Blogu bora ya burudani
- Bongo5
Mwanamitindo bora wa kiume
- Idris Sultan
Mwanamitindo bora wa kike
- Hamisa Mobetto
MAWASILIANO MTANDAONI
Mtengeneza grafiki bora
- Karim Salkim
Ukurasa bora wa elimu
- Ubongo Kids (YouTube)
Mpiga picha bora
- Albert Manifester
Muandaa maudhui bora
- Masoud Kipanya
Mraghibishi wa mwaka
- Diamond Platnumz
Hashtag ya mwaka
- #ChangeTanzania
UVUMBUZI MTANDAONI
Mvumbuzi bora kidijitali
- Jumanne Mtambalike
Uvumbuzi bora kidijitali
- Immigration Passport Application System
Aplikesheni bora ya huduma za kifedha
- M-Pesa
Aplikesheni bora ya huduma za elimu
- Ubongo Kids (Math Rats)
MASOKO MTANDAONI
Mradi bora wa Uwajibikaji Jamii
- Mfumo wa Kusajili Vizazi Kidigitali (Mobile Birth Registration - Tigo)
Mjasiriamali bora wa kike
- Zuwena Yusuf Mohammed (Shilole)
Mjasiriamali bora wa kiume
- Sheria Ngowi
Kampuni bora ya Huduma za Masoko Mtandao
- Smart Codes
Kiongozi bora wa kibiashara wa kike
- Fatema Dewji
Kiongozi bora wa kibiashara wa kiume
- Mohamed Dewji
Kampeni bora ya Masoko Mtandaoni
- Yajayo Yanafurahisha (Vodacom)
Huduma bora kwa wateja mtandaoni
- NMB Bank
VYOMBO VYA HABARI MTANDAONI
Mtangazaji bora wa kike
- Dinny Nasoro – Dizzim Online
Mtangazaji bora wa kiume
- Fredrick Bundala – Simulizi na Sauti
Redio bora ya Mtandaoni
- +255 Global Radio
Kiongozi bora wa Vyombo vya Habari Mtandaoni wa kike
- Maria Tsehai Sarungi
Kiongozi bora wa Vyombo vya Habari Mtandaoni wa kiume
· Millard Ayo
Chombo bora cha Habari Mtandaoni
- Mwananchi Communications
Blog bora
- Millard Ayo
TV bora ya Mtandaoni
- Ayo TV
SERIKALI MTANDAONI
Tasisi bora ya Serikali Mtandaoni
- Idara ya Uhamiaji
Chama bora cha siasa
- CHADEMA
Kampeni bora ya kisiasa
- #MatokeoChanya
Ukurasa bora wa Serikali
- Shirika la Reli Tanzania (TRC)
Mwanasiasa bora wa kike
- Halima Mdee
Mwanasiasa bora wa kiume
- Zitto Kabwe
UCHECHEMUZI MTANDAONI
- Anna Henga
Kiongozi bora wa asasi za kiraia wa kiume
- Aidan Aeyakuze
Kampeni bora ya uchechemuzi mtandaoni
- Nyumba ni Choo (Wizara Afya)
Asasi ya kiraia bora mtandaoni
- Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
DIPLOMASIA MTANDAONI
Kiongozi bora wa kidiplomasia wa kike
- Pamela O’Donnell (Balozi wa Canada)
Kiongozi bora wa kidiplomasia wa kiume
- Peter VAN ACKER (Balozi wa Ubelgiji)
Ukurasa bora wa Balozi zilizopo Tanzania
- Ubalozi wa Marekani
Taasisi bora ya kimataifa mtandaoni
- Benki ya Dunia Tanzania
CHAGUO LA WATU
- Diamond Platnumz
TUZO YA HESHIMA
· Muhidin Issa Michuzi – Muasisi wa vyombo vya habri mtandaoni (Michuzi Blog)
Kwa taarifa zaidi tembelea www.digitalawards.co.tz
Leave a comment