
Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
imetangaza kuchukua usimamizi wa Benki ya Biashara ya China kuanzia leo Novemba
19, 2020.
Uamuzi huo umefikiwa baada
ya Benki Kuu kugundua kuwa benki hiyo ina upungufu mkubwa wa mtaji kinyume na
matakwa ya Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya 2006.
Akizungumza jijini Dodoma
leo, Gavana wa BoT, Prof. Frolens Luoga ameweka wazi kuwa BoT ina mamlaka ya
kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuifilisi Benki yoyote pindi inaposhindwa
kukidhi masharti ya kuwa na akiba ya kutosha kuweza kuendesha shughuli za
kibenki ili kulinda wateja wa benki hiyo pamoja na sekta ya fedha.
Uamuzi huo wa kuiweka Benki
ya CCB chini ya BoT umelenga kuhakikisha Benki hiyo inarudi katika uwezo wa
kuendesha shughuli za kibenki kwa kuzingatia kanuni na taratibu zinazohitajika.
Pamoja na hatua hiyo, BoT
imevunja Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CCB na mabadiliko yote yanakusudiwa
kuanza rasmi leo Novemba 19, 2020.
Aidha, CCB itasitisha
shughuli zake kwa takribani siku 90 mpaka pale Benki Kuu ya Tanzania itakapotoa
maelekezo zaidi juu ya utaratibu unaohitajika.
Benki ya Biashara ya China
ilianza shughuli zake rasmi mnamo Novemba 2018 ikiwa na lengo la kusaidia
makampuni ya China yanayoendeshwa nchini Tanzania, pia kuwawezesha Watanzania
wanaofanya biashara nchini China.
Leave a comment