Habari

Umoja wa Mataifa Wasikitishwa na Ripoti za Ukatili wa Kingono Tigray

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa baadhi ya watu walilazimishwa kuwabaka wanafamilia wenzao, huku wanawake wakilazimishwa kufanya mapenzi na wanajeshi ili kupata mahitaji yao ya kila siku

Umoja wa Mataifa unasema umepokea ripoti za kusikitisha kuhusu ukatili wa kijinsia katika eneo lenye mgogoro la Tigray, ikiwamo ripoti zinazoonesha watu wanaolazimishwa kuwabaka wanafamilia wenzao.

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono katika maeneo yenye migogoro, Pramila Patten amesema kuna malalamiko mengi kutoka eneo la mapigano, hasa kutoka eneo la Mji Mkuu, Makele.

"Baadhi ya wanawake walilazimishwa kufanya mapenzi na wanajeshi ili kupata mahitaji ya kila siku," amesema Pramila, akizitaka pande zote zinazozozana kutofumbia macho uhalifu wa kingono.

Soma zaidi

- Wanajeshi 17 wa Ethiopia Wakamatwa kwa Tuhuma za Uhaini katika Mgogoro unaoendelea kwenye jimbo la Tigray

- Jeshi la Ethiopia Kuanza Operesheni ya Mwisho Kuchukua Mji Mkuu wa Jimbo la Tigray

Pramel ameongeza kuwa kumekuwa na ongezeko la mahitaji ya vidonge vya dharura vya kuzuia mimba na upimaji wa magonjwa ya zinaa, ikimaanisha kuwa kumekuwa na ukatili wa kingono katika eneo la mgogoro. Ameomba mashirika ya kutoa misaada kuongeza misaada ya kiutu kwa wahanga wa mapigano wanaoendelea kuwasili katika kambi za wakimbizi.

Zaidi ya Waethiopia 59,000 wamekimbilia nchini Sudan, huku Waeritrea 5,000 wakiathiriwa na mapigano hayo, wakilazimika kukaa katika makambi yenye hali mbaya ya kibinadamu, bila chakula wala maji.

Mapema mwezi huu, Televisheni ya Taifa ilirusha video inayomuonesha mwanajeshi akielezea wasiwasi wake kuhusu kile kinachoendelea katika eneo la mapigano.

"Kwanini wanawake wanabakwa katika Mji wa Makele?" mwanajeshi huyo alisikika. "Isingekuwa inashangaza sana kama imetokea wakati wa mapigano, kwa sababu hali hiyo haiwezi kuzuilika na inaweza kutegemewa. Lakini wakati huu polisi wa taifa na polisi wa eneo hilo wakiwa wamerejea, hali hiyo bado inaendelea."

Mgogoro wa Tigray ulianza mapema mwezi Novemba mwaka jana baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia kutangaza kuwatuma wanajeshi wake kupambana na vikosi vya eneo hilo baada ya vikosi hivyo kuvamia kambi ya kijeshi. Abiy alitangaza ushindi baadaye mwezi huohuo, baada ya wanajeshi wake kufanikiwa kuutwaa mji wa Tigray. Ingawa viongozi wengi wa TPLF wamekimbia eneo hilo, wameapa kuendelea kupambana na vikosi vya Abiy.

Maelfu ya watu wamefariki katika mgogoro huo, kwa mujibu wa mashirika ya kibinadamu nchini humo, lakini si rahisi kuelewa hali ya mambo ilivyo kutokana na kuzuiwa kwa vyombo vya habari kuripoti kutoka eneo la mapigano huku taasisi za kutoa misaada pia zikizuiwa kufanya kazi.