
Raia wa Ethiopia Gebreegziabher Mebratu Melese ambaye ni Mkuu
wa Masuala ya Usalama wa Umoja wa Afrika (AU) amefutwa kazi na Mwenyekiti wa
Umoja huo, Moussa Faki Mahamat baada ya Serikali ya Ethiopia kumtuhumu kwa
kukosa uaminifu.
Hatua hii inakuja huku Taifa hilo likikabiliwa na mapigano
kati ya Majeshi ya Serikali na vikosi vya Jimbo la Tigray.
Bw. Moussa Faki alichukua hatua hiyo Novemba 11 baada ya
Wizara ya Ulinzi ya Ethiopia kuuandikia barua Umoja wa Afrika(au) ikimtuhumu
Bw. Malese kwa kukosa uaminifu.
Mashambulizi ya ndege za kivita na vikosi vya ardhini dhidi
ya vikosi vya Tigray yamepelekea vifo kwa mamia na kusababisha idadi kubwa ya
wakimbizi kukimbilia nchi jirani ya Sudan.
Mashambulizi hayo ya vikosi vya Serikali yalianza Novemba 4
pale Waziri Mkuu Abiy Ahmed alipotangaza vita na vikosi vya Jimbo hilo
akivituhumu kwa kushambulia kambi za jeshi na kudharau maagizo ya Serikali
yake.
Kwenye barua iliyotoka kwa Waziri wa Ulinzi wa Ethiopia
kwenda AU imemtuhumu Gebreegziabher ambaye ana cheo cha Meja Jenerali kuwa hana
nia thabiti na malengo ya Umoja wa Afrika wala Serikali ya Ethiopia.
Siku ya jana Alhamisi Serikali ya Ethiopia ilitoa taarifa
kuwa inawashikilia watu takribani 150 ambao ni wapiganaji wa vikosi vya jimbo
la Tigray ambao walikuwa kwenye jiji la Addis Ababa na miji mingine wakiwa
katika mipango ya kufanya mashambulizi ya kigaidi.
Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU) yapo jijini Addis Ababa
nchini Ethiopia. Takribani vikosi 4,400 vya Ethiopia vipo nchini Somalia
vikilinda Amani.
Leave a comment