Habari

Ukata wa Fedha wapelekea Gazeti la Mtanzania kusitisha Uzalishaji

Kampuni hiyo inamilikiwa na Mfanyabiashara Bilionea, Rostam Aziz, ambaye aliinunua mwaka 2006 ikiwa inaitwa Habari Corporation Limited na ilikuwa inamilikiwa na Wanahabari nguli akiwemo Jenerali Ulimwengu na Salvatory Rweyemamu

Kampuni ya New Habari Limited (2006) inayomiliki magazeti ya Mtanzania, Rai, Bingwa na Dimba yatangaza kusitisha uzalishaji wa Magazeti hayo kutokana na mwenendo mbaya wa biashara unaoikabili kampuni hiyo.

Akizungumza na wafanyakazi wa kampuni hiyo leo Ijumaa Desemba 3, 2020 jijini Dar es Salaam, Mhariri Mtendaji, Dennis Msacky amesema uzalishaji wa magazeti hayo utasitishwa kuanzia Jumatatu Desemba 7, 2020.

Kampuni hiyo inamilikiwa na Mfanyabiashara Bilionea, Rostam Aziz, ambaye aliinunua mwaka 2006 ikiwa inaitwa Habari Corporation Limited na ilikuwa inamilikiwa na Wanahabari nguli akiwemo Jenerali Ulimwengu na Salvatory Rweyemamu.

Hii ni mara ya pili kwa kampuni hiyo kutangaza kusitisha uzalishaji, ambapo Mei 15, 2019 ilitangaza kuwa kuanzia Mei 20  hadi Juni 20 ingesitisha uzalishaji wa gazeti la Mtanzania kutokana na mabadiliko makubwa ya muundo yaliyokuwa yakiendelea.

Taarifa hiyo iliyotolewa na uongozi wa kampuni hiyo ilisema uamuzi huo ulifikiwa baada ya kampuni kubadili muundo na uendeshaji na kwamba gazeti hilo lingepatikana katika mfumo wa kidijitali kwa kipindi chote hicho.

Taarifa hiyo ya 2019 ilisema hatua hiyo itaendana pia na kupunguza wafanyakazi.

“Kampuni inautangazia umma na wateja wake kuwa hivi sasa kampuni inabadili muundo wa uendeshaji na uzalishaji, pia kubadili mwelekeo kutoka ‘print’ kwenda “digital”, hatua hiyo itaendana pia na kupunguza wafanyakazi" ilisema taarifa hiyo.

Hatua hiyo ya kusitishwa kwa uzalishaji wa gazeti la Mwananchi (Mei 20, 2019), iliibua mjadala mtandaoni baadhi ya watu wakidai kuwa ni shinikizo kutoka Serikalini. 

Mfano Mwanasiasa mashuhuri na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter, "Leo nimekwenda ninaponunua magazeti kila nikiwa Dar es Salaam. Gazeti la Mtanzania sasa rasmi halipo baada ya shinikizo kubwa kutoka kwa watawala na mazingira magumu ya Biashara"

Barani Afrika na duniani kote, makampuni yanayojihusisha na uzalishaji wa magazeti ya habari yamekuwa yakikumbwa na changamoto ya namna ya kuhama kutoka kwenye mfumo uliozoeleka wa uchapishaji wa magazeti na kushindwa kukumbatia mfumo mpya wa kidijitali ambako ndiko wasomaji wengi walikohamia.

Makampuni mengi ya magazeti yameshindwa kutumia fursa za kuzalisha mapato kwa kutumia fursa za kidijitali na kupelekea kukabiliwa na ukata wa fedha na kusitisha uzalishaji.

Hata hivyo, sheria mbovu za uendeshwaji wa magazeti na vyombo vya habari, ambazo zimekuwa zikikandamiza uhuru wa vyombo vya habari kuripoti baadhi ya habari ambazo zina maslahi kwa umma lakini hazipendwi na watawala, zimepelekea vyombo vya habari kushindwa kuwa na habari ambazo zinavutia wasomaji hivyo kupelekea kushuka kwa mauzo ya magazeti.

Hatua ya leo Ijumaa Disemba 4 2020 ya Kampuni ya New Habari Limited kusitisha uchapishaji kuanzia Jumatatu wiki ijayo, imeibua tena mjadala mtandaoni ambapo watu kadhaa wametoa maoni yao wakionyesha kusikitishwa na hatua hiyo.

 Mfano mwandishi mwandamizi, Nevile Meena ameandika kupitia ukurasa wake wa Twitter, "Sad. Taarifa za Kampuni ya New Habari 2006 Ltd kusitisha utoaji wa magazeti yake ni habari mbaya kwa tasnia yetu. Waandishi wa Habari tutaendelea kuzagaa mitaani bila kazi".

Naye Wakili Fatma Karume ameandika, "Propaganda haiuzi Magazeti! Habari inauza Magazeti. Ukitaka kufanya propaganda lazima uwe na deep pockets kama Magazeti ya Serikali yanayoendeshwa kwa kodi za wananchi"

Mtanzania ni moja ya gazeti la kila siku ambalo kwa miaka mingi limekuwa na wasomaji lukuki. Hili litakuwa ni gazeti la pili kwa mwaka huu 2020 kuondoka sokoni. 

Mwezi Juni mwaka huu, Serikali iliifutia leseni gazeti la kila siku, Tanzania Daima kwa kile ilichosema ni  'kukithiri na kujirudia' kwa makosa yanayokiuka sheria za nchi na maadili ya uandishi wa habari.

"Kwa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 9(b) cha sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016, nimefuta leseni ya TanzaniaDaima ikiwa ni baada ya kulionya gazeti hilo kwa zaidi ya mara 10 huku gazeti lenyewe likilazimika kuomba radhi mara mbili kwa uvunjifu wa maadili ya kitaaluma na sheria za nchi, ikiwemo kuchapisha habari za uongo, uchochezi na uzandiki", ilieleza barua kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari.