Habari

UGANDA: Maandamano ya Kupinga Bobi Wine Kukamatwa, 16 Wafariki, 60 Wajeruhiwa na 300 Wako Lupango

Bobi Wine bado yuko chini ya mikono ya Polisi tangu jana, Wagombea wengine wa Upinzani wasitisha kampeni zao kupinga Bobi Wine kushikiliwa

Watu 16 wamefariki mpaka sasa katika maandamano yanayoendelea nchini Uganda wakipinga kukamatwa kwa mgombea urais, Bobi Wine.

 

Polisi wamesema jumla ya watu 60 wamejeruhiwa na 300 wamekamatwa.

 

Bwana Bobi Wine bado yuko chini ya ulinzi wa Polisi tangu jana, alikamatwa akiwa katika Mji wa Mashariki unaoitwa Luuka akishtumiwa kusababisha mikusanyiko ya watu ikiwa ni uvunjaji wa miongozo ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona iliyowekwa na Tume ya Uchaguzi nchini humo.

 

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya Jeshi la Polisi nchini humo mnamo Jumatano, Inspekta Jenerali wa Polisi alizungumzia malengo ya nchi katika kuimarisha utekelezaji wa taratibu za kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona kipindi cha  kampeni.

 

"Licha ya onyo lililotolewa mara kwa mara kwa wagombea, mawakala wao na umma juu ya athari mbaya na hatari za kiafya za kufanya mikutano na maandamano, bado tumekua tukiendelea kushuhudia vitendo vya ukaidi na upuuzaji kabisa wa miongozo ya EC [Tume ya Uchaguzi]. Kwa hiyo, wale ambao watakaidi miongozo hii ya Tume ya Uchaguzi na mipango yao mibaya inayolenga kuvuruga mchakato wa uchaguzi hakika itakumbana na athari, "ilisema taarifa hiyo.

 

Hata hivyo taarifa hiyo haikuweka wazi kuwa watu hao wamefariki vipi ingawa video na picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilikuwa zinaonesha watu wakiwa wamepigwa risasi na kulala chini huku wakiwa wametapakaa damu.

 

Wakati mamlaka imesema vizuizi ni muhimu kuzuia kuenea kwa virusi vya corona, wanachama wa upinzani wanadai kuwa suala hilo ni kisingizio cha kuzuia kampeni na kuwatisha wafuasi wa upinzani kabla ya uchaguzi ujao wa Januari.

 

Kufuatia habari za kukamatwa kwa Wine, waandamanaji waliingia kwenye barabara za Kampala, wakipambana na polisi na wanajeshi ambao walijibu kwa mabomu ya kutoa machozi.

Wakati huohuo,Wagombea urais kutoka vyama vya upinzani nchini Uganda wamesema kuwa wanasitisha kampeni zao hadi pale mgombea mwenzao Robert Kyagulanyi maarufu Kama Bobi Wine atakapoachiwa huru.

 

Wagombea hao wamesema ni vigumu kwao kuendelea na kampeni huku mgombea mwingine akiwa anaendelea kunyanyaswa na polisi kwa madai yasiyo na msingi.

 

Marekani imekemea ghasia zilizojitokeza katika mji mkuu wa Kampala na miji mingine nchini Uganda kufuatia kukamatwa kwa mgombea wa Urais Robert Kyagulanyi kupitia ujumbe uliosomeka "Pande zote zipinge vita na kuchukua hatua za kupunguza hofu iliyotanda nchini humo".

 

Bobi Wine alijiunga na siasa mnamo 2017 akiwa mgombea huru na amebaki kuwa mwiba kwa Rais Yoweri Museveni, akilaani sera zake na kuimba nyimbo zinazoipinga Serikali ya Museveni.


Bobi Wine sasa anapinga kitendo cha Museveni kushikilia madaraka kwa miongo mitatu. Hapo awali alikamatwa mapema Novemba baada ya kuidhinishwa na Tume ya Uchaguzi.