Habari

Ufaransa Yaamuru Mfadhili wa Mauaji ya Kimbari Rwanda Kushitakiwa Tanzania

Mahakama ya rufaa nchini Ufaransa imekubali kumpeleka mshukiwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, Felicein Kabuga, kushtakiwa nchini Tanzania. Bwana Kabuga alikamatwa nyumbani kwake nje ya mji wa Paris baada ya miaka 26 akikimbia mkono wa dola.

Uhamisho huo unakuja baada ya rufaa dhidi ya uamuzi wa kuhamisha kesi yake katika mahakama maalumu ya Umoja wa Mataifa kutupiliwa mbali na mahakama ya rufaa ya Ufaransa. Uamuzi wa kuhamisha kesi hiyo ulioamriwa na Jaji Mkuu wa mahakama hiyo, William H. Sekule.

Vuta n'kuvute hiyo iliyojitokeza mwezi Juni kati ya mawakili, waendesha mashtaka na Mkuu wa Mahakama ya kimataifa kwa ajili ya Rwanda. Mawakili walihoji kuwa Kabuga asingepata haki katika mahakama hiyo ya kimataifa yenye makao yake Mjini The Hague na Arusha nchini Tanzania, na kudai kwamba hali ya Kabuga kiafya imezorota sana kuweza kumpeleka nchini Tanzania.

Siku chache baada ya dai hilo, waendesha mashtaka wa mahakama ya kitaifa kwa ajili ya Rwanda waliomba kesi dhidi ya Kabuga ifunguliwe mjini The Hague kwa Hoja inayodai kuwa Arusha Tanzania kuna tishio la virusi vya Corona, pendekezo lililotupiliwa mbali na Jaji Mkuu wa mahakama hiyo, Wiliam H. Sekule.

Kabuga alikamatwa mwezi Mei nyumbani kwake jijini Paris baada ya kutafutwa kwa miaka 25. Anakabiliwa na mashtaka ya makosa ya kuyafadhili makundi yenye silaha wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka wa 1994, ambayo yalisababisha vifo vya watu laki nane ikiwa ni pamoja na Watutsi na Wahutu wenye msimamo wastani.

Félicien Kabuga, anayetuhumiwa kuwa 'mfadhili mkuu' wa mipango ya kutekeleza mauaji ya kimbari, alikamatwa mnamo Mei 16 mwaka huu huko Asnières-Sur-Seine karibu na mji wa Paris, eneo ambalo alikuwa anaishi kwa kutumia majina bandia baada ya kuwa mafichoni kwa miaka 25. Marekani ilitoa dau la dola milioni 5 kwa atakayeweza kutoa taarifa kuhusu bwana Kabuga ili aweze kukamatwa.

Félicien Kabuga ni mfanyabiashara maarufu nchini Rwanda, ambaye alitajwa kuwa mtu tajiri zaidi nchini humo kabla ya kufanyika kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Alizaliwa katika eneo la kaskazini mwa Rwanda ambako alijilimbikizia mali kutokana na biashara ya majani ya chai miaka ya 1970 na kuwekeza katika biashara tofauti nchini humo, mataifa jirani na ng'ambo. Alikuwa mwandani wa karibu wa chama tawala cha MRND na baba mkwe wa Rais Juvénal Habyarimana.

Kabuga anayetuhumiwa kuwa mfadhili mkuu wa mipango ya kutekeleza mauaji ya kimbari, alikuwa mwenye hisa mkuu katika kituo cha radio ya kibinafsi, RTLM, ambacho kililaumiwa kwa kuwahamasisha watu wa jamii ya Kihutu kuwaua wenzao wa Watutsi.