
Kamati ya Maadili ya Shirikisho
la Soka Duniani, FIFA, limemfungia kwa miaka mitano Rais wa Shirikisho la Soka
Barani Afrika CAF, Ahmad Ahmad baada ya kukutwa na hatia ya uvinjifu wa
maadili.
Rais huyo hatoruhusiwa
kujihusisha na shughuli zote zinazohusiana na soka aidha la Kitaifa au Kimataifa.
Raia huyo wa Madagascar ambaye aliingia madarakani mwaka 2017 pia ametakiwa
kulipa faini ya Dola za Marekani 22,000.
Kamati hiyo ya Maadili ya
Fifa imemkuta Bw. Ahmad na hatia matumizi mabaya ya ofisi, matumizi ya fedha na
kutoa zawadi na upendeleo kwa baadhi ya watu kwa nafasi yake kama Rais wa
CAF.
Hatua hii inakuja huku Bw.
Ahmad akiwa kwenye mchakato wa uchaguzi wa kugombea muhula mwingine ili
kuendelea kuliongoza shirikisho hilo. Nafasi yake kama Rais wa CAF inamfanya
anakuwa Makamu wa Rais wa FIFA.
Miaka minne ya utawala wa
Ahmad iligubikwa na tuhuma za ubadhirifu wa fedha kwenye makao makuu ya CAF
ambayo yapo jijini Cairo, Misri.
Juni 2019 Rais huyo
alishikiliwa kwa mahojiano huko Paris nchini Ufaransa kwa tuhuma zinazohusiana
na uongozi wake ndani ya CAF.
Ukaguzi wa fedha uliofanywa
na FIFA ulionyesha kuna upotevu wa fedha ambapo kiasi cha Dola za Marekani 100,000
zililipwa kwa watu 18 akiwemo Rais Ahmad kwa ajili ya kusafiri kwenda kwenye Hijja
nchini Saudi Arabia.
Uchaguzi
Mkuu wa CAF unatarajiwa kufanyika Machi, 2021 huko Rabat nchini Morocco. Ahmad
aliingia madarakani mwaka 2017 kwa kuungwa mkono na viongozi wa FIFA ili
kumuondoa madarakani Issa Hayatou aliyeongoza shirikisho hilo kwa miaka 29.
Leave a comment