Habari

Twitter Yaifunga Kabisa Akaunti ya Rais Trump

Twitter imetoa hiyo taarifa usiku wa kuamkia leo na kuongeza kuwa awali ilifunga akaunti ya Rais huyo kwa kuwa ilikuwa inaonekana kuchochea ghasia zaidi

Twitter imetangaza kufungia kabisa akaunti yake ya twitter @realDonaldTrump, na akaunti ya kampeni ya @TeamTrump kutokana hatari ya kuchochea vurugu zaidi kufuatia vurugu zilizojitokeza katika jumba la Capitol Hill.

Twitter imetoa hiyo taarifa usiku wa kuamkia leo na kuongeza kuwa awali ilifunga akaunti ya Rais huyo kwa kuwa ilikuwa inaonekana kuchochea ghasia zaidi.

"Baada ya kuchunguza kwa karibu jumbe zinazochapishwa kwenye akaunti ya @realDonaldTrump na muktadha unaozunguka jumbe hizo na namna zinavyotafsiriwa ndani na nje ya Twitter - tumesimamisha kabisa akaunti hiyo kwa sababu zinaonekana kuhamasisha vurugu zaidi,”. kampuni hiyo aliandika katika chapisho la blogi

"Katika vurugu za kutisha zilizojitokeza hivi karibuni, tuliweka wazi Jumatano kwamba ukiukaji zaidi wa taratibu za Twitter ungeweza kusababisha hatua hii," taarifa ilieleza.

Rais Trump alifungiwa akaunti yake ya Twitter kwa saa 12 Jumatano baada ya kutoa wito kwa wafuasi wake kuvamia bunge ambao aliwaita "wazalendo".

Mamia ya wafuasi wake walivamia bunge wakijaribu kuvuruga kikao cha kuidhinisha ushindi wa Bwana Biden kama Rais. Vurugu hizo zilisabaisha vifo vya raia wanne na afisa mmoja wa polisi.

Mtandao wa Twitter baadaye ukaonya kuwa unaweza kumpiga marufuku Bwana Trump kuutumia kabisa ikiwa atakiuka tena kanuni za jukwaa hilo la mawasiliano.

Baada ya akaunti yake ya Twitter kuwezeshwa tena, Bwana Trump alituma ujumbe kwenye mtandao wa Twitter Ijumaa kuwa kampuni hiyo ilikuwa na mwisho kuchochea.

Katika moja ya ujumbe wake aliandika: "Wamarekani 75,000,000 Wazalendo walionipigia kura, Marekani Kwanza na Fanya Marekani kuwa Bora Tena, watakuwa na sauti inayosikiza siku zijazo. Hawatakosewa heshima au kuchukuliwa kwa uonevu kwa namna yoyote ile !!!"

Mtandao wa Twitter umesema ujumbe huo "unatafsiriwa kama ishara zaidi ya kuwa Rais Trump hana mpango wa kuhakikisha kunafanyika 'mabadilishano ya mamlaka kwa njia ya amani'".

Hata baada ya kufungiwa akaunti binafsi Trump hakuishia hapo  alishiriki ujumbe kupitia akaunti rasmi ya Rais wa Marekani @POTUS akisema kuwa "ataangalia uwezekano wa kuwa na mtandao wao utakaowezesha mawasiliano siku za usoni" na kukosoa Twitter. ingawa Twitter waliuondoa muda mfupi baada ya kuwekwa.

TRUMP ANASEMA HATAHUDHURIA UZINDUZI WA BIDEN

Rais Trump amesema kuwa hatohudhuria sherehe za kuapishwa rais wa 46 wa Marekani, Joe Biden.

Mtandao wa Twitter umesema kuwa ujumbe huo "umechukuliwa na wafuasi wake kadhaa kama thibitisho la kwamba uchaguzi huo haukuwa halali".

Mtandao wa Twitter umesema ujumbe wote huo alioandika "unakiuka sera na kanuni katika uhamasishaji wa vurugu".

Hatua hii itakuwa mara ya pili kwa Rais aliyepo madarakani kutohudhuria, ya kwanza ikiwa 1869 ambapo Andrew Johnson alisusa baada ya kuondolewa madarakani na Bunge la nchi hiyo.

Kwa kawaida, Rais aliyepo madarakani hupanda gari moja na Rais anayeingia madarakani kuelekea eneo la uapisho, ikiwa ni ishara ya umoja na kukabidhiana madaraka kwa amani na utulivu.