Habari

Twitter na Facebook zafunga Akaunti za Rais Trump

Uondoaji huo ni hatua kubwa zinazofanywa na kampuni hizo za mitandao ya kijamii tofauti na hali ilivyokuwa hapo awali ambapo walikuwa wanasita kuchunguza na kuchukua uamuzi juu ya machapisho ya viongozi wakubwa wa kisiasa kama Rais

Twitter na Facebook zimechukua hatua ya kufungia akaunti za Rais Trump baada ya kutuma ujumbe kwa wafuasi wake waliovamia bunge la Marekani

Twitter iliondoa jumbe tatu kutoka kwenye akaunti ya Rais Donald Trump siku ya Jumatano na kusimamisha akaunti yake kwa masaa 12 baada ya  Rais huyo kuendelea kushinikiza nadharia potofu kuhusu uchaguzi pindi umati ulipovamia bunge la Marekani.

Kampuni hiyo pia ilionya kuwa ukiukaji zaidi wa sheria zake "utasababisha kufutiliwa mbali" kwa akaunti ya Twitter ya Rais Trump.

Moja ya jumbe ni pamoja na video ya Trump akirudia madai yasiyo na msingi kwamba uchaguzi ulihujumiwa huku akiwahimiza wafuasi wake kutawanyika baada ya ghasia kuzuka ndani na nje ya jumba la Capitol Hill. Alisema kuwa sheria na utulivu zinahitajika akidai kwamba anawapenda wafuasi wake.

Facebook na YouTube pia ziliondoa kanda ya video kutoka kwenye akaunti ya Trump kwa sababu ilikiuka sera inayopingana na  kusambaza madai ya udanganyifu kuhusu uchaguzi uliopita. Facebook ilisema ilizuia akaunti ya Rais huyo kwa masaa 24 kwa madai ya kuwa alikuwa anachochea badala ya kupunguza ghasia zilizokuwa zikiendelea.

 Hapo awali Twitter haikuwa imeondoa akaunti ya kiongozi huyo badala yake iliondoa uwezo wake wa kujibiwa , kupendwa na kutolewa maoni ikiwa nma ujumbe uliosomeka  "Madai haya ya ulaghai wa uchaguzi si halali, na  chapisho hili haliwezi kujibiwa, kutolewa maoni, au kupendwa kwa sababu linahatarisha hali ya usalama."

Twitter ilisema kupitia moja ya akaunti za kampuni yake kwamba ikiwa Trump ataondoa machapisho yake, akaunti yake itafunguliwa.

Uondoaji huo ni hatua kubwa zinazofanywa na kampuni hizo za mitandao ya kijamii tofauti na hali ilivyokuwa hapo awali ambapo walikuwa wanasita kuchunguza na kuchukua uamuzi juu ya  machapisho ya viongozi wakubwa wa kisiasa kama Rais. Twitter na Facebook wameweka mfumo za kukagua ukweli  kwenye baadhi ya machapisho ya Trump kuchunguza walijumuisha habari ambazo zinakiuka sheria zao, na hapo awali Twitter ilishawahi kufungia kwa muda akaunti  binafsi na za kampeni za Rais Trump.

YouTube ilisema katika taarifa kwamba video hiyo ilikiuka "sera kuhusu maudhui ambayo yanadai udanganyifu  kuhusu uchaguzi uliopita.”

Facebook ilisema: "Maandamano ya vurugu huko Capitol leo ni aibu. Tunakataza uchochezi na wito wa vurugu kwenye jukwaa letu. Tunakagua na kuondoa maudhui yote yanayokiuka sheria hizi."

Makamu wa Rais wa Uadilifu Facebook, Guy Rosen  alichapisha ujumbe uliosomeka ”Hii ni hali ya dharura na tunachukua hatua zinazostahiki ikiwa ni pamoja na kuondoa video ya Rais Trump. Tumeiondoa kwa sababu tunaamini inachangia badala ya kupunguza hatari ya vurugu zinazoendelea ."