Habari

Trump Akubali Kukabidhi Madaraka kwa Amani

“Lengo langu sasa ni kuhakikisha kuwa mchakato wa kukabidhi madaraka unafanyika kwa njia ya Amani; wakati huu tunahitaji maridhiano”

Rais Donald Trump ametuma ujumbe wake wa kwanza kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter tangu kufungiwa kwa akaunti yake kufuatia ghasia za Jumatano zilizoibuka ndani na nje ya jumba la Capito Hill.

Kufuatia kufungiwa kwa akaunti yake kwa muda wa masaa 12  baada ya kampuni hiyo kudai jumbe zake zinachochea ghasia, Rais Trump alichapisha ujumbe wa video akisema “Sasa bunge la Congress limeidhinisha matokeo na utawala mpya utaingia tarehe 20 Januari”.

Lengo langu sasa ni kuhakikisha kuwa mchakato wa kukabidhi madaraka unafanyika kwa njia ya amani.

Trump alishiriki ujumbe huo alioufanya dakika chache kabla ya hotuba ya makubaliano, akikiri kuwa serikali mpya itachukua madaraka tarehe januari 20. Trump alisema alikuwa akifuata "kila njia ya kisheria kupinga matokeo ya uchaguzi" kwa lengo moja tu la kuhakikisha uadilifu unatendeka katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Trump pia alilaani wafanya ghasia ambao walivamia bunge la Marekani siku ya jumatano wakati wabunge wakiwa kwenye mchakato wa kupiga kura ili kuidhinisha matokeo ya uchaguzi.

Ujumbe wa Trump ulikuja baada ya wabunge wengi kumlaumu kwa kuwaita wafuasi kupinga matokeo ya uchaguzi na "kuacha udanganyifu" licha ya ushahidi wake dhidi ya matokeo kufutiliwa mbali.

Siku ya Alhamisi, wabunge wengi, wafanyakazi wa zamani wa Trump na wateule walitaka Trump aondolewe ofisini kufuatia ghasia. Wabunge wa vyama vyote viwili pamoja na viongozi waandamizi katika utawala wa Rais huyo wameanza mazungumzo juu ya kumuondoa madarakani. Spika wa bunge Nancy Pelosi amesema ikiwa hataondolewa kwa njia hiyo bunge litajaribu kwa mara ya pili kumfungulia mashtaka ili kumuondoa madarakani. Spika Pelosi moja kwa moja amemlaumu rais Trump kwa kuchochea alichoita uasi wa kutumia nguvu dhidi ya Marekani.

Katika kadhia nyingine hapo awali, Spika Pelosi na kiongozi wa maseneta wa chama cha Democratic, Chuck Schumer walijaribu kuwasiliana kwa njia ya simu na Makamu wa Rais Mike Pence kumtaka achukue nafasi ya Rais Trump mara moja kwa mujibu wa kipengele cha 25 cha katiba ya Marekani kinachomruhusu makamu wa Rais kuchukua hatua hiyo, ikiwa Rais ameshindwa kuyatimiza majukumu yake. Taarifa zaidi zinasema sasa idadi ya wabunge inaongezeka ya wanaomtaka Rais Trump ajiuzulu na tayari wanatafakari mashtaka mapya juu ya kumng’atua.