
Ma Mwandishi Wetu
Mtumishi wa Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Tito Magoti pamoja na mwenzake, Theodory Giyani, ambaye mtaalamu wa mifumo ya kompyuta wamehukumiwa kulipa faini ya Sh 17.3milioni baada ya kupatikana na hatia ya kuongoza genge la uhalifu
Hukumu hiyo imetolewa leo, Januari 5, 2021 na Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega, baada ya washtakiwa hao kukiri mashtaka yao kwa DPP.
Mbali na kulipa fidia, mahakama hiyo, imewahukumu adhabu ya kutokutenda kosa lolote la jinai kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia leo.
Hakimu Mtega alisema, mahakama hiyo imewatia hatiani washtakiwa hao kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.
"washtakiwa mmetiwa hatiani kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu wa kupangwa, hivyo mnatakiwa kulipa kiasi cha Sh 17, 354,535 kama fidia kwa Serikali " alisema Hakimu Mtega.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi akisaidiana na wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya uamuzi kutokana na washtakiwa kukiri mashtaka yao.
Wakili Kadushi amesema washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu, lakini baada ya kufanya majadiliano na DPP, wamefutiwa mawili na kubakisha shtaka moja ambalo ni kuongoza genge la uhalifu.
Kadushi baada ya kueleza hayo, wakili Simom aliwasomea mashtaka, ambapo kati ya Februari mosi na Desemba 17, 2019 jijini Dar es Salaam na katika maeneo mbalimbali ya ndani ya nchi Tanzania, mshtakiwa Tito Magoti, Theodory Giyani na wenzao ambao hawajafikishwa mahakamani, walishiriki makosa ya uhalifu wa kupanga kwa kumiliki programu za kompyuta iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya kufanya uhalifu na kupelekea kujipatia fedha kiasi cha Sh 17, 354,535.
Washtakiwa hao walikuwa wanatetewa na mawakili , Fulgence Massawe, Jebra Kambole na Pasiansi Mlowe, waliiomba mahakama hiyo kuwapunguzia adhabu kwa sababu ni vijana wadogo na wanategemewa na familia zao na walionyesha ushirikiano tangu siku ya kwanza walipofikishwa mahakamani hapo.
Itakumbukwa kuwa Tito Magoti na mwenzake Theodory Giyan, kabla ya kufikishwa mahakamani walishikiliwa kwa zaidi ya masaa 72 huku taarifa za kukamatwa kwao zikiwa hazijawekwa wazi na Jeshi la Polisi.
Mnamo Disemba 24, 2019 Tito Magoti na mwenzake walifikishwa mbele ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka matatu ambayo kwa mujibu wa sheria za Tanzania, hayana dhamana hatua iliyopelekea kusota rumande kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Leave a comment