Habari

TBC, CHADEMA Wamaliza Tofauti Zao

Ni baada ya CHADEMA kuwafukuza waandishi wa habari waliokuwa wakiripoti uzinduzi wa kampeni za Chama hicho, pande zote mbili zimekubaliana kurudisha uhusiano

Mgogoro kati ya Shirika la Utangazaji nchini Tanzania na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) umemalizika baada ya viongozi wakuu wa aasisi hizo kukutana na kujadili suala hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jukwaa la Wahariri nchini Tanzania kupitia kwa Katibu wa Jukwaa hilo Nivville Meena, imesema kuwa kikao hicho cha maridhiano kilichofanyika katika ofisi za makao makuu ya Tume ya Uchaguzi NEC, yaliyopo mkoani Dodoma  kilihusisha viongozi wa taasisi tatu ambao ni pamoja na Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Deodatus Balile, Mkurugenzi wa TBC Ayubu Ryoba, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe pamoja na Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Dkt Willson Mahella Charles.

Mkurugenzi wa shirika la Utangazaji TBC, Ayubu Ryoba amesema kuwa hatua iliyochukuliwa na CHADEMA ya kuwafukuza waandishi wa habari wa chombo hicho katika mkutano wa ufunguzi wa kampeni wa chama hicho uliofanyika katika uwanja wa Zakiem, Mbagala Jijini Dar es Salaam ililenga kubomoa kiwango cha TBC kuaminika kwa umma, na pia kukiri makosa yaliyofanywa na watangazaji wa kituo hicho wakati wakirusha matangazo hayo na kuahidi kuwa shirika halitarudia makossa yaliyojitokeza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe ameeleza kuwa uhusiano kati ya chama hicho na TBC umekuwa si mzuri kwa muda mrefu, na kwamba hata vyombo vingine vya habari vimekuwa vikikataa kurusha matangazo yao hata kama kimelipia kwa maelezo ya kuwa kimepewa maelekezo kutoka juu. Freeman Mbowe amevitaka vyombo vya habari kufaya kazi kwa weledi katika kipindi chote cha kampeni

Awali Mkurugenzi wa Tume ya uchaguzi wakati akifungua kikao hicho alieleza kuhusu umuhimu wa vyombo vya habari vya umma na wajibu wake katika kutoa fursa kwa vyama vyote vya siasa kwa mujibu wa sheria. Lakini pia mwenyekiti wa Baraza la Wahariri, Deodatus Balile, ameeleza umuhimu wa vyombo vya habari kushirikiana na vyma vya siasa pamoja na vyama vya siasa kushirikiana na vyombo vya habari hasa katika kipindi cha kampeni

Baada ya mjadala katika ya pande zote mbili Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania, TBC, Ayub Ryoba pamoja na Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe walikubaliana kumaliza tofauti zao na kurejesha ushirikiano ambapo Mbowe amesema kuwa atawatangazia wanachama wa CHADEMA kuwa wapo tayari kufanya kazi na TBC, na TBC wameiomba CHADEMA kuwapa ratiba yao ya kampeni ili waweze kuendelea kurusha matangazo yao.