Habari

SUMA-JKT Wapewa Siku 60 Kukamilisha Ujenzi wa Tenki la Maji

Oktoba 2020, Wizara ya Maji ilitoa bilioni moja kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) kutatatua changamoto ya upatikanaji wa maji

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba ametoa siku 60 kwa SUMA-JKT ambao wamepewa kandarasi ya ujenzi wa tanki la maji la Buigiri, Chamwino jijini Dodoma. Kemikimba ametoa agizo hilo Januari 19, 2021 akiwa katika ziara ya kukagua ujenzi wa tenki hilo linalotarajiwa kuwa na ujazo wa lita milioni 2.5.

 

Akizungumza wakati wa ziara, Kemikimba ameagiza ujenzi kukamilika mapema katika kipindi cha miezi miwili huku akisema taratibu zote zilishakamilika na ujenzi ulipaswa kuanza Septemba 2020. 

“Tumekubaliana na mkandarasi kuwa ujenzi wa tenki ukamilike ndani ya miezi miwili kwa hiyo wana siku 60 kuhakikisha ujenzi umekamilika,” amesema Kemikimba.

 

Ujenzi wa tenki hilo la Buigiri utagharimu kiasi cha shilingi milioni 998 na tenki hilo linatarajiwa kuhudumia wakazi wa Chamwino na Hospitali ya Rufaa ya Uhuru jijini Dodoma. 

 

Sambamba na kutoa agizo hilo kwa mkandarasi, Kemikimba ameitaka ofisi ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kufanya ufuatilia wa ujenzi wa tenki hilo kila siku ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati. 

 

Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu, Kemikimba ametembelea eneo la Ihumwa ambapo visima vya maji vinachimbwa na kuwataka kitengo cha uchimbaji visima kilicho chini ya RUWASA kuongeza kasi ya uchimbaji kwa lengo la kuhakiksha upatikanaji wa maji ya kutosha jijini Dodoma. 

Akiwa eneo la Nzunguni, Kemikimba amekagua zoezi la ukarabati wa kisima linalosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Dodoma (DUWASA) na kupongeza juhudi za DUWASA kuhakikisha upatikanaji wa maji jijini Dodoma.

 

Oktoba 2020, Wizara ya Maji ilitoa kiasi cha shilingi bilioni moja kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) kwa lengo la kutatatua changamoto ya upatikanaji wa maji jijini humo inayochochewa na ongezeko la watu.