Habari

Shirika la Umeme, Kenya Matatani Baada ya Twiga wawili `Kupigwa Shoti'

Huduma ya Wanyamapori Kenya (KWS) ilithibitisha kuwa Shirika la Umeme linatakiwa kubadilisha nguzo za umeme ndani ya eneo hilo ili kuzuia vifo vya twiga ambao urefu wao umezidi nguzo zilizopo kwa sasa

Taarifa kutoka kwa Huduma ya Wanyamapori Kenya (KWS) ilithibitisha kutokea kwa tukio hilo la twiga wawili 'kupigwa shoti' ambalo lilitokea katika Hifadhi ya Soysambu huko Nakuru mwishoni mwa wiki na kulitaka Shirika la Umeme  kubadilisha nguzo  ndani ya eneo hilo ili kuzuia vifo vya twiga ambao urefu wao umezidi nguzo zilizopo kwa sasa.

Baadhi ya Wakenya wametumia mtandao wa kijamii wa Twitter siku ya Jumapili kuelezea hasira zao baada ya picha za twiga hao waliopigwa shoti hadi kufa kusambaa.

Wengine walihoji ni kwanini Shirika la Umeme Kenya halijashughulikia suala la ufupi wa nguzo za nyaya licha ya malalamiko kadhaa kwa miaka miwili iliyopita wakati wengine walikosoa upuuzaji wa spishi za wanyama walio hatarini kama vile twiga wa Rothschild.

KWS imesema maafisa wa shirika la umeme la Kenya, wataweka vigingi vinginevya umeme.

"Ripoti ya awali inaashiria urefu wa vigingi vya umeme kupitia hifadhi ya Soysambuvi uko chini, kuliko urefu wa twiga," sehemu ya taarifa ilisema.

Mhifadhi wa Wanyama, Bi Kahumbu alisema vifo vya wanyama hao vingezuiliwa ikiwa ushauri wa wataalamu ungezingatiwa.

"Nyaya hizi za umeme zimekuwa zikiwaua twiga na wanyama wengine.Tathmini ya kuchunguza hatari kabla ya mradi kuidhinishwa inafanywa kiholela. Inasikitisha kwamba hadi hali kama hii itokee ndio hatua ichukuliwe!" aliandika kwenye Twitter yake.