Habari

Serikali ya Ethiopia Yafunga Akaunti za Benki Zinazohusishwa na Waasi wa TPLF

Makampuni Makubwa katika sekta za fedha, madini, nguo, ujenzi, biashara ya jumla, na usafirishaji yamehusishwa

Serikali ya Ethiopia Jumanne ilifunga akaunti za benki za biashara zinazohusishwa na viongozi wa Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF)

 

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Ethiopia alitoa taarifa siku ya Jumanne  na kuorodhesha mashirika 34 ya biashara ambayo akaunti zao za benki zimefungwa, akisema kuna ushahidi kwamba kampuni hizo zinahusika katika kufadhili waasi huko Tigray na kujaribu kuharibu hali ya amani katiba wa nchi hiyo.

 

Kampuni zilizopigwa marufuku zinahusika katika sekta za fedha, madini, nguo, ujenzi, biashara ya jumla, usafirishaji, utengenezaji na sekta zingine, na kwa muda mrefu wamesemekana kuwa na uhusiano wa karibu na TPLF.

 

Miongoni mwao ni Sur Construction, moja ya kampuni kubwa zaidi za ujenzi nchini, Guna Trading Enterprise, Almeda Textile Manufacturing, Kiwanda cha Saruji cha Mesebo, na Trans Ethiopia ambayo imekuwa ikihusika katika usafirishaji na biashara ya nje.

 

Vilevile, kampuni ya utengenezaji madawa, Addis Pharmaceutical, ya Madini, Izana Mining, Mesfin Industrial Engineering, Selam Public Transport Association, na Mega Printing Company, kampuni ya uchapishaji.

 

Kufungwa kwa akaunti za kampuni hiyo kumekuja wiki mbili baada ya serikali kuchukua hatua dhidi ya Vikosi Maalum vya Tigray vinavyoongozwa na TPLF.

 

Vikwazo vya kifedha vilikuja wakati Waziri Mkuu Abiy Ahmed alitangaza kumaliza msamaha wa siku tatu uliopewa viongozi wa TPLF kujisalimisha kwa mamlaka. Viongozi hao walikuwa wakitafutwa na polisi wa Ethiopia.

 

Katika ujumbe uliochapishwa kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, Abiy alisema baadhi ya Kikosi Maalum cha Tigray na wanamgambo wamejisalimisha kwa amani kujiokoa na kuokoa watu wao.

 

Ingawa hakuonyesha ni wangapi wamejisalimisha, alisema wale ambao hawatojisalimisha watakumbana na nguvu kamili ya sheria wakati serikali yake ikitekeleza "hatua za mwisho" za kuishughulikia TPLF.

 

Wakati huo huo, mataifa mbalimbali na Jumuiya ya Kimataifa imeendelea kupaza sauti kutaka kusitishwa kwa mgogoro huo unaotajwa kuweza kusababisha ukosefu wa amani katika ukanda wa pembe ya Afrika.