Habari

Serikali Kutumia Ndege Kudhibiti Nzige

Hata hivyo mpaka sasa hakuna na madhara yoyote yaliyoripotiwa kusababishwa na nzige hao kwani eneo lililovamiwa kwa kiasi kikubwa ni pori lakini pia asilimia kubwa ya nzige hao bado ni wadogo

Serikali nchini Tanzania imetangaza kuanza kutumia ndege kunyunyizia dawa makundi ya nzige yaliyovamia wilaya ya Longido na Simanjiro wakitokea nchini Kenya.

Taarifa za kuingia kwa makundi hayo zilitolewa kwa mara ya kwanza siku ya Ijumaa na mkuu wa wilaya ya Longido, Frank Mwaibambe ambaye amesema ndege ya Shirika la Chakula Duniani FAO inayotokea Nairobi inatarajia kuanza kazi ya kunyunyuzia dawa leo.

 “Kuanzia kesho (22.02.2021) ndege maalum itaanza kazi kupulizia sumu kuua nzige waliovamia maeneo ya Longido na Simanjiro ili wasiendelee kusambaa na kusababisha maafa” alisema Waziri wa KIlimo, Prof. Mkenda

Waziri Mkenda amesema tayari wataalam wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu (TPRI) wapo wilayani Longido na Simanjiro wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wake Dkt. Efrem Njau kwa kazi ya kudhibiti wadudu hao waharibifu wa mazao ya kilimo.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kutookota wala kula nzige watakaokuwa wameuwawa na viuatilifu (sumu) kwenye maeneo yote ambapo ndege hiyo itapita kuua nzige kwani viuatilifu hivyo vinaweza kuwa na madhara kwa binadamu.

Pia, ameagiza wataalam wa kilimo na watendaji wa vijiji na kata kutoa taarifa kwa wananchi juu ya uwepo wa kazi ya kuua nzige hivyo wasiwe na hofu watakapoona ndege inaruka chini kwenye maeneo.

“Wananchi wakiona nzige wameanguka chini wamekufa wasiwachukue au kula kwa kuwa wengi watakuwa wamekufa kwa sumu” alisisitiza Prof. Mkenda

Waziri huyo wa kilimo amesisitiza kuwa serikali itahakikisha mazao ya wakulima na malisho ya mifugo hayaharibiwi na nzige ndio maana ametembelea eneo hilo la Longido ambapo amebainisha mafanikio ya kuwadhibiti tangu walipoingia nchini mwezi Januari mwaka huu kwenye baadhi ya maeneo.

Hata hivyo, mpaka sasa hakuna na madhara yoyote yaliyoripotiwa kusababishwa na nzige hao kwani eneo lililovamiwa kwa kiasi kikubwa ni pori lakini pia asilimia kubwa ya nzige hao bado ni wadogo.

Mwaka jana makundi makubwa ya nzige yalivamia maeneo kadhaa nchini Kenya na Ethiopia na kuibua hofu ya kutokea kwa baa la njaa kutokana uharibifu mkubwa walioufanya.