Habari

Serikali Yasema Kutoa Takwimu ni Kuwatisha Wananchi

"Sio suala la kutaka kila siku Waziri wa Afya aelezale kwenye TV waliofariki, wagonjwa, waliozikwa ni ujinga mtupu, unatishia taifa na kufanya lisitulie” - Dkt. Mollel.

Serikali imesema kuwa haitatoa takwimu za maambukizi ya virusi vya corona kwani kufanya hivyo ni kuongeza hofu kwa wananchi hali itakayopunguza kinga za miili yao na kupelekea kuongezeka kwa maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa huo 

Akizungumza na waandishi wa habari Naibu waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa matumizi ya data za magonjwa yote ni kwa ajili ya kuchakata na kisha kuja na mbinu za kisayansi kukabiliana na magonjwa hayo lakini sio swala la kutaka kila wiki Waziri wa Afya aelezale waliofariki na wagonjwa, kwani kufanya hivyo ni kuwatisha wananchi. 

“Wanasema Tanzania haitoi data, matumizi ya data za magonjwa yote, ni kwa ajili ya kuchakata na kisha kuja na mbinu za kisayansi kukabiliana na magonjwa hayo lakini sio swala la kutaka kila siku Waziri wa Afya aelezale kwenye TV waliofariki, wagonjwa, waliozikwa ni ujinga mtupu, unatishia taifa na kufanya lisitulie,” amesema Dk. Mollel.

Katika hatua nyingine Dkt Mollel amewataka Watanzania kuondoa hofu dhidi ya Virusi vya corona kwani hata nchi zilizochukua hatua kubwa za kupambana na virusi hivyo ndizo zimeonekana kuwa na idadi kubwa ya maambukizi.

“Hivi ni nchi gani inaweza kuchukua hatua zaidi na bora za kujikinga zaidi ya Marekani, Uingereza, au nchi zilizoendelea. Leo tunavyozungumza hivi kati ya Marekani na sisi, ni wapi wameumia zaidi na ugonjwa wa COVID-1?” amehoji Dkt Mollel.  

Kauli hii imekuja wakati ambapo shirika la Afya Duniani (WHO) limekuwa likitoa wito kwa mamlaka nchini. kuanza kutoa takwimu za watu waliambukizwa ugonjwa wa COVID-19, kuhimiza matumizi ya njia za tahadhari zinazotolewa na shirika hilo pamoja na kujiandaa kupokea chanjo dhidi ya COVID 19.

Katika taarifa yake ya February 20 mwaka huu,  kuhusu mwenendo wa COVID-19 nchini Tanzania, shirika la Afya Duniani (WHO) lilielelezea wasi wasiwasi wake kuhusu idadi ya wasafiri wa Tanzania waliopatikana na kuwa na virusi vya corona  

Hata hivyo serikali imekuwa ikihimiza zaidi watu kuendelea kuchukua tahadhari zinazotolewa na wizara ya Afya nchini dhidi ya maambukizi ya Virusi vya corona ikiwa ni pamoja na kumuomba Mungu na kutumia tiba asili.