Habari

RPC Songwe, Uchunguzi wa kifo cha “Gwanda” anayesemekana kufa mikononi mwa Polisi utakuwa Huru na wa Haki

Gwanda alikamatwa Disemba 3 2020 akitoka mnadani, Disemba 4 2020 ndugu zake walipigiwa simu na walipofika hospitali waliambiwa Gwanda alifikishwa hospitali na askari polisi akiwa ameshafariki

Na Antony Sollo Songwe

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Songwe George Kyando ameihakikishia familia ya Marehemu Gwanda Jitungulu (44) anayedaiwa kuuawa kutokana na kipigo cha Askari Polisi akiwa katika Kituo cha Polisi Mkwajuni Wilaya ya Songwe Mkoani humo kuwa jeshi la polisi litafanya uchunguzi wa kina na uchunguzi huo utakuwa huru na wa Haki.

Akizungumza na timu ya watu sita walioteuliwa na familia ya marehemu Gwanda Jitungulu kufuatilia hatima ya kuchunguzwa kwa tukio la mauji ya ndugu yao anayedaiwa kuuawa kutokana na kipigo cha askari polisi akiwa katika kituo cha polisi cha Mkwajuni kilichopo Wilaya ya Songwe Kamanda wa jeshi la polisi George Kyando alisema, jeshi la polisi mkoa wa Songwe limepokea maelekezo kutoka kwa Viongozi wa ngazi za juu na litafanya kazi hiyo ya kuchunguza wahusika wa mauaji ya ndugu yao na ikibainika kuwa wahusika ni askari lazima watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa Mahakamani kujibu tuhuma za mauaji zinazowakabili.

“Jeshi la Polisi limepokea maelekezo kutoka kwa Viongozi wa ngazi za juu na litafanya kazi hiyo ya kuchunguza wahusika wa mauaji ya ndugu yao na ikibainika kuwa ni askari lazima watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za mauaji zinazowakabili.” - alisema kamanda Kyando

Akizungumza na Serengeti Post Madosa Jitungulu ambaye ni mdogo wa marehemu Gwanda jitungulu Madosa Jitungulu alisema siku ya tukio Disemba 3 2020, wakitokea mnadani  huko Mtega akiwa na kaka yake viongozi wawili ambao ni Afisa Mtendaji wa Kata ya Udinde na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kininga walimkamata kaka yake na kumpeleka Ofisi ya Kata wakimtuhumu kwa kosa la wizi wa mifugo.

Hata hivyo baada ya kumfikisha katika ofisi ya kata  ya Udinde, viongozi hao baadaye walimkabidhi mtuhumiwa huyo kwa askari wa jeshi la polisi kituo cha Mkwajuni. Siku moja baadaye Disemba 4 2020, familia ilipata taarifa kuwa ndugu yao Gwanda Jitungulu alikuwa amepelekwa Hospitali ya Mwambani Mkwajuni akiwa katika hali mbaya ya kiafya (hajitambui).

 

“Disemba 4 2020, tulipata taarifa kuwa ndugu yetu Gwanda Jitungulu alikuwa amepelekwa Hospitali ya Mwambani Mkwajuni akiwa na hali mbaya (hajitambui)na baada ya kufuatilia tuliambiwa kuwa Gwanda alifikishwa Hospitalini hapo na Askari wa Jeshi la Polisi Kituo cha Polisi cha Mkwajuni akiwa tayari ameshafariki.” - alisema Madosa Jitungulu ambaye ni mdogo wake na marehemu.

 

Akiongea kwa masikitiko makubwa Madosa ameiambia Serengeti Post kuwa, baada ya kuthibitishiwa kuwa ndugu yao alikuwa ameshafariki familia ilianza kutafakari juu ya kilichopelekea kifo cha marehemu na baadaye walikwenda kuonana na watendaji wa jeshi la polisi Wilaya ya Songwe pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Songwe ambao walielekeza kuchukua mwili na kwenda kuzika kitendo ambacho wanafamilia hao hawakukubaliana nacho.

“Kutokana na hali hiyo tulifanya kikao cha familia na kujadili tukio la kifo cha ndugu yetu ambapo katika kikao hicho iliteuliwa timu ya watu sita (6) kwenda Dodoma kuonana na viongozi wa ngazi za juu ili kutafuta ufumbuzi wa jambo hili.” – alieleza Madosa. 

Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu Gwanda Jitungulu baada ya timu hiyo kusafiri hadi Mkoani Dodoma walifika kwa Waziri wa Mifugo Mashimba Ndaki na baada ya kuwasikiliza alimuagiza Katibu wake kuwaandikia barua ili kuonana na Waziri wa Mambo ya Ndani ili waweze kupata suluhu juu ya jambo hilo.

Baada ya maelekezo toka kwa Waziri wa Mifugo Mashimba Ndaki timu hiyo ilikwenda kuonana na Waziri wa Mambo ya Ndani ili kusikiliza malalamiko yao kwa lengo kulipatia ufumbuzi jambo hilo na hata hivyo walielekezwa kuonana na Mkurugenzi wa dawati la Malalamiko Wizara ya Mambo ya Ndani Kamishna Albert Nyamuhanga ambaye baada ya kuwasikiliza ndugu wa marehemu Gwanda Jitungulu aliagiza warudi Mkoani Songwe ili wakaonane na Uongozi wa Jeshi la Polisi ngazi ya Mkoa ili kulipatia ufumbuzi jambo hili.

Disemba 17 2020, wakiwa kwa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe wawakilishi wa familia walieleza kuwa familia ya Marehemu Gwanda Jitungulu inaomba kufanyika uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha kifo cha ndugu yao akiwa mikononi mwa jeshi la polisi kituo cha polisi Mkwajuni Wilaya ya Songwe na kusema kuwa wakati ndugu yao akikamatwa hakuwa na tatizo lolote la kiafya.

“Sisi kama familia tunaomba kufanyika uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha kifo cha ndugu yetu akiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi Kituo cha Polisi Mkwajuni Wilaya ya Songwe na ikumbukwe kwamba wakati ndugu yetu akikamatwa hakuwa na tatizo lolote la kiafya lakini pia tunaomba kurejeshewa fedha kiasi cha Tshs 2,750,000/= alizokamatwa nazo marehemu siku ya tarehe 03/12/2020 wakati akitoka kuuza ng’ombe wake watano katika mnada ulioko Mtega Songwe.” - alisema Madosa Jitungulu 

Akizungumza na Serengeti Post Msemaji wa familia ya Marehemu  Gwanda Jitungulu Jilya Jidaha Dalala alisema baada ya kufika na kuonana na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando aliwasikiliza kwa makini na kuwahakikishia wanafamilia hao kuwa jeshi la Polisi litafanyia kazi maelekezo ya ngazi za juu na litatoa ushirikiano katika suala zima la kuchunguza chanzo cha kifo cha marehemu Gwanda Jitungulu na wote waliohusika watakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya Sheria.

“Baada ya kufika katika Ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe George Kyando alitusikiliza kwa makini na kutuhakikishia (wanafamilia ya Gwanda) kuwa jeshi la Polisi litafanyia kazi maelekezo ya ngazi za juu na litatoa ushirikiano katika suala zima la kuchunguza chanzo cha kifo cha marehemu Gwanda Jitungulu na wote waliohusika watakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya Sheria jambo ambalo kwa pamoja tumekubaliana kwenda kusimamia zoezi la uchunguzi wa mara ya pili wa mwili wa marehemu na baada ya hapo tutakwenda kuuhifadhi katika nyumba ya milele.” - alisema Jilya Jidaha Dalala. 

Disemba 17 2020, Serengeti Post lilishuhudia Askari Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Songwe, SSP Johnny Maro akiwa na msaidizi wake wakienda Mkwajuni wakiongozana na timu ya wanandugu na kufanikisha zoezi la uchunguzi wa mara ya pili wa mwili wa marehemu Gwanda Jitungulu na baadaye Kamanda wa Jeshi la Polisi George Simba Kyando alitoa gari kwa ajili ya kupeleka mwili wa marehemu kwa mazishi kijijini kwao Udinde huku Mkuu wa Wilaya ya Songwe Samwel Opulukwa akitoa gari lililobeba ndugu wa marehemu wapatao ishirini na sita kuwarejesha kijijini na Disemba 18 2020 mwili wa marehemu ulizikwa majira ya saa saba mchana baada ya kukaa chumba cha kuhifadhia maiti kwa takribani siku kumi na moja.

Kwa upande wao wananchi wa kijiji cha Udinde wameishukuru Serikali kwa hatua zilizofikiwa na kuomba watu wote waliohusika katika zoezi la ukamataji wa mtuhumiwa waweze kuchukuliwa hatua ikiwemo kufikishwa Mahakamani ili Sheria ichukue mkondo wake.

“Tunaishukuru Serikali kwa hatua ilizochukua kuurejesha mwili wa ndugu yetu lakini tunaomba taarifa za uchunguzi na wahusika wote wahojiwe naikibainika kuwa wamehusika na kifo cha ndugu yetu sheria ichukue mkondo wake.” - alisema mmoja wa wanandugu ambaye alikataa kuandikwa jina lake gazetini.

Ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) inaonesha uwepo wa matukio ya mauaji yanayotoka na maafisa wa vyombo vya dola kutumia nguvu kupita kiasi. Ripoti ya shirika hilo la haki za binadamu ya mwaka 2019 ilirekodi matukio matatu (3) yaliyoripotiwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Geita na Pwani. 

Hata hivyo, jeshi la polisi linapaswa kuepuka utumiaji wa nguvu kupita kiasi pale wanapomkamata mtuhumiwa na kumweka chini ya ulinzi au mahabusu kama inavyoelekezwa na viwango mbalimbali vya kitaifa na kimataifa kuhusu ukamataji na uwekaji kizuizini wa watuhumiwa, ikiwemo Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi na Kanuni za Umoja wa Mataifa za Utendaji Kazi wa Maafisa wa Vyombo vya Dola.