Habari

Rais Samia Suluhu Hassan: Fungulieni Vyombo Vya Habari Vilivyofungiwa

Wananchi na wadau wamedai kuwa maagizo hayo yanaleta sura mpya ya uhuru wa vyombo vya habari ambao ulilalamikiwa kubanwa sana kipindi cha mtangulizi wake, Hayati John Pombe Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni pamoja na Wizara ya Teknolojia na Mawasiliano kuvifungulia na kuviondolea adhabu vyombo vyote vya Habari vilivyofungiwa kwa makosa mbali mbali.

 

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Aprili 6, 2021 Ikulu Dar es salaam baada ya kuwaapisha watendaji wa wizara ambao ni makatibu wakuu, manaibu makatibu wakuu pamoja na wakuu wa taasisi mbalimbali.

 

Rais Samia amesema “Wizara ya Habari nasikia kuna vyombo vya habari mmevifungia, vifungulieni lakini wafuate sheria na miongozo ya serikali, tusiwape mdomo wa kusema tunabinya vyombo vya Habari, tusifungie tu kibabe.”

 

Wananchi na wadau wamedai kuwa maagizo hayo yanaleta sura mpya ya uhuru wa vyombo vya habari ambao ulilalamikiwa kubanwa sana kipindi cha mtangulizi wake, Hayati John Pombe Magufuli.

 

Aidha, watumiaji wa mitandao ya jamii wamepongeza hatua hiyo huku wakitoa mapendekezo ya kurekebishwa kwa sheria zinazokandamiza vyombo vya Habari.