Habari

Rais Magufuli: Walionizidi Umri wasahau Urais, Kabudi na Lukuvi Hatuwezi Kuwapitisha

Hata Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anaweza asimalize hii miaka mitano mingine

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli juzi Novemba 16 2020 amemuapisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, baada ya kuidhinishwa wiki iliyopita na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kupitia hafla fupi ya Uapisho iliyofanyikia katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, Mkuu huyo wa nchi amewaapisha pia Mawaziri wawili wa Wizara muhimu, ambao ni; Professa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pamoja na Dkt. Philip Mpango kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Aidha, hafla hiyo ya uapisho imehudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine mbalimbali wa Serikali.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, anakuwa ni Waziri Mkuu wa pili baada ya Fredrick Sumaye kuteuliwa katika nafasi hiyo kwa vipindi viwili mfululizo. Majaliwa anaingia katika awamu yake ya pili akisifika kwa utendaji mzuri kwenye kipindi kilichopita cha miaka mitano.

Akihutubia hadhira iliyohudhuria hafla hiyo ya uapisho, Waziri Mkuu Majaliwa amemshukuru Rais Magufuli kwa uteuzi na kuahidi utendaji mzuri katika awamu yake mpya.

Pia, Waziri Mkuu amegusia suala la Saruji kupanda bei, "Wako wenzetu wachache wameanza kujisahau na tumeona kumeibuka upandaji bei wa saruji kwa gharama kubwa sana ambazo hazikubaliki na hakuna sababu ya msingi. Serikali yetu imefanya mambo makubwa sana, hatutarajii saruji kuwa na bei hiyo ambayo tumeiona".

Kutokana na sintofahamu hiyo, Waziri Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa wote nchini kuwa mpaka itakapofika tarehe 20, Novemba kila mmoja awe amefika palipo na kiwanda cha saruji kujua kwanini bei ya bidhaa hiyo imepanda kwa ongezeko la zaidi ya shilingi 3,000 na kwingine 4,000.

Naye Rais Magufuli akiongea baada ya kuwaapisha viongozi hao, amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuendelea kubaki katika nafasi yake itategemea na utendaji wake, sio lazima amalize miaka mitano.

"Nilikuwa naangalia kwenye vyombo vya habari na wengine wakishangilia Mh. Kassim amepata miaka mingine mitano, kana kwamba nimewaambia atakaa miaka 5. Nataka niwaambie, kazi ya Uwaziri Mkuu haina “guarantee”, itategemea na performance yake, kwahiyo tumuombee" alidokeza Rais Magufuli.

Akaongeza kwa kutoa historia fupi ya waliowahi kuwa mawaziri wakuu na muda waliokaa madarakani, "Waziri Mkuu wa kwanza alikuwa Mwalimu Nyerere, akafuata Kawawa akatumikia miaka 5, Edward Sokoine akatumikia miaka 3, akaja tena Sokoine akatumikia mwaka 1, akaja Sinde Warioba miaka 5. Nawatajia hii miaka ili mjue kazi ya Uwaziri Mkuu isivyotulia".

Katika hotuba yake pia, Rais Magufuli amegusia suala la Urais ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2025 na kuwataka wale wenye umri zaidi ya miaka 60 wasahau nafasi hiyo kwani Kamati Kuu ya Chama haiwezi kumpitisha mtu mwenye umri unaozidi miaka 60.

Kwa msisitizo, alimtaja Waziri wa Ardhi aliyemaliza muda wake, William Lukuvi, ambaye alikuwa anasifika kwa utendaji mzuri katika Baraza la Mawaziri lililopita.

Rais Magufuli amesema, "Sina uhakika kama Lukuvi ataupata Urais, sasa ana miaka zaidi ya 60. Yaani kwenye Kamati Kuu tuchague Rais anayenizidi umri? Maneno mengine yanaumiza lakini nataka niwaeleze mjitayarishe kisaikolojia kusudi msije mkapoteza hela zenu".

Hali kadhalika, Rais Magufuli amewataka Wabunge wa CCM wanaotolea macho nafasi za Uwaziri kuacha kwani walichaguliwa na wananchi kwenda kuwawakilisha Bungeni na sio kuwa Mawaziri.

"Tulienda kuomba ubunge kwamba tutawatumikia wananchi wetu na tulikabidhiwa ilani ya kurasa 303, sasa haya mengine yanatoka wapi? Nafasi za Mawaziri na Manaibu Waziri haziwezi kufika 30, sasa katika watu 350, hata ungekuwa wewe unateua ungepata shida kubwa" amesema Rais Magufuli.

Baada ya kupewa nafasi ya kuhutubia, Waziri wa Masuala ya Kigeni, Profesa Kalamagamba Kabudi, ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Magufuli kwa kusema, "Mh. Rais, hii ni mara ya 4 unanipa mshituko nisioutarajia. Unanipa nafasi bila kutarajia na umeniacha na butwaa. Januari 16, 2017, saa 10:00 jioni nikiwa darasani nafundisha sheria, kupitia kwa Msemaji wa Ikulu, Gerson Msigwa uliniteua kuwa mbunge" alieleza Kabudi.

Waziri wa Fedha, Dkt. Philip Mpango amesema japokuwa nchi imeingia kwenye uchumi wa kati, bado maeneo mengi nchini kuna umaskini kwahiyo kazi iliyopo mbele ni kubwa zaidi na inahitajika kufanya kazi kwa bidii kuwatumikia wananchi.

Katika hatua nyingine, Mwanasiasa wa Upinzani na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, kupitia ukurasa wake wa Twitter amepinga zoezi la uapisho wa Mawaziri wapya akidai kuwa Mawaziri Kabudi na Mpango ni Mawaziri bandia kwani wameteuliwa kinyume na masharti ya Katiba Ibara ya 55(1), kwa sababu Rais ameteua Mawaziri bila kushauriana na Waziri Mkuu.

“Katiba yetu i wazi. Rais anateua Mawaziri baada ya kushauriana na Waziri Mkuu. Waziri Mkuu anakuwa na Mamlaka baada ya kula kiapo. Leo Waziri Mkuu na Mawaziri wanakula kiapo Pamoja? Rais asiye na uhalali anaendelea kuvunja Katiba yetu. Anajiona Katiba ni Yeye na Yeye ni Katiba” ameandika Zitto.

Kwa sasa, kinachosubiriwa kwa hamu ni Baraza la Mawaziri ambapo wafuatiliaji wa mambo ya siasa pamoja na wananchi kwa ujumla wanatamani kujua ni nani watakaoteuliwa katika nafasi hizo nyeti, licha ya Rais Magufuli kutanabaisha kuwa atachelewa kidogo kutangaza baraza hilo.