Habari

Rais Magufuli Asisitiza Matumizi ya Barakoa za Ndani, Awataka Watanzania Kuzidisha Maombi na Kujifukiza

"Ndugu zangu nchi nyingi zimeanza kuvaa barakoa, ninyi ni mashahidi katika vyombo vya habari nchi hizo ndizo zinaoongoza kwa watu wengi kufa" - Rais Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli amesema kuwa serikali haijakataza matumizi ya barakoa katika kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona bali Watanzania wachukue tahadhari kwa kutumia barokoa zinazotengezwa nchini ikiwemo zile zilizotengenezwa na Bodi ya Dawa (MSD) kwa kuwa barakoa zinazoagizwa kutoka nchi za nje zina mashaka ya kuwa sio salama.

Akizungumza hii leo katika Manisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amewataka Watanzania kuchukua tahadhari ya virusi vya corona hususani matumizi ya njia za asili ikiwa ni pamoja na kujifukiza katika kukabiliana na janga hilo.

“Serikali haijazuia barakoa, lakini tuwe waangalifu katika kuchagua barakoa ipi nina vaa, tutaangamia msifikiri tunapendwa mno vita ya kiuchumi ni mbaya, na ndio maana nawapongeza waliovaa barakoa walizojitengenezea wao,” amesema Rais Magufuli 

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kumtanguliza Mungu katika mapambano dhidi ya COVID-19, kwani njia za kibinadamu ikiwemo uvaaji wa barakoa, kutokugusana au kukabiliana, pamoja na kujifungia majumbani (lockdown) hazijasaidia kupambana na janga hilo kwani nchi nyingi zilizochukua hatua hizo bado zinaongoza kwa maambukizi ukilinganisha na Tanzania ambayo haikuchukua hatua hizo hapo awali.

“Ndugu zangu nchi nyingi zimeanza kuvaa barakoa, ninyi ni mashahidi katika vyombo vya habari nchi hizo ndizo zinaoongoza kwa watu wengi kufa wengi maelfu sijasema msivae barakoa na wala msini koti vibaya lakini kuna barakoa nyingine sio nzuri”amesema Magufuli.