Habari

Pitso Mosimane Uso kwa Uso na "Total War" ya Msimbazi

“Hii ni sawa na mtu kuwa porini halafu akutane na Chui, lazima apambane bila kukata tamaa vinginevyo atauliwa" - Haji Manara

Shirika la habari la nchini Marekani CNN limemtaja kama Pep Gardiola wa mpira wa Afrika kwenye makala inayoelezea mchezo wa nusu fainali wa Mabigwa wa vilabu Duniani kati ya Al Ahly kutoka nchini Misri dhidi ya Bayern Munich ya huko nchini Ujerumani 

Kocha wa Al Ahly, Pitso Mosimane amekuwa na mvuto kwa makocha wengi barani Afrika kutokana na uwezo wake aliouonyesha kupitia klabu ya Mamelod Sundowns ya Afrika ya Kusini, timu ya taifa ya Afrika ya kusini (Bafana Bafana) kati ya mechi 23 alizoiongoza klabu ya Al Ahly ameshinda mechi 18, ametoka sare mechi 5 na kupoteza mchezo mmoja dhidi ya Bayern Munich. Mbali na Matokeo hayo kocha huyo amesema kuwa klabu ya Simba ni klabu bora na iliyojengeka kwasasa. 

Akizungumza baada ya kuwasili nchini Tanzania, Kocha huyo amesema kuwa mchezo huo utakua ni mgumu kutokana uimara wa timu zote mbili.

"Tutazungumza zaidi wakati wa mkutano na waandishi wa habari, lakini utakua ni mchezo mgumu Simba walitufunga wakati uliopita na tunakwenda kufanya marekebisho," amesema Pitso Mosimane.

Klabu ya Al Ahly ambao wameshinda mchezo wao wa kwanza, dhidi ya El Mellerk watakua ugenini siku ya Jumanne wakicheza na wenyeji wao klabu ya Simba ambao nao wametoka kushinda katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Ac Vita. Klabu ya Simba imeshinda michezo mitatu ya klabu bingwa kati ya mitano iliyocheza.

Hata hivyo klabu ya Simba imesema kuwa imejipanga kuhakikisha kuwa inapata ushindi katika mchezo huo ambapo baada ya kauli mbiu ya ‘War in Dar’ kufanikiwa kuwaongoza Simba kuibuka na ushindi wa bao 4-0 dhidi ya FC Platnum ya Zimbabwe na kufanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, klabu hiyo kupitia kwa Ofisa habari wake Haji Manara sasa imetangaza kauli mbiu ya Total War ili itumike kuwapa nguvu wanasimba wote kuelekea mchezo huo. 

“Hii ni sawa na mtu kuwa porini halafu akutane na Chui, lazima apambane bila kukata tamaa vinginevyo atauliwa, hiyo ndio maana halisi ya kauli mbiu yetu hiyo ambayo itawafanya wachezaji waingie uwanjani wakiamini kuwa hakuna nafasi nyingine zaidi ya kushinda,” amesema Manara.

Klabu ya Al Ahly ndio vinara wa Kundi A, huku klabu ya Simba ikishika nafasi ya pili na kufuatiwa na AS Vita na El Merekh ambao mpaka sasa bado hawajavuna alama hata moja. Mbali na ubora wa klabu ya Al Ahly mchambuzi wa masuala ya michezo nchini Gharib Mzinga anaamini kuwa Simba sio klabu ya kudharaulika kwa sasa katika michuano ya kimataifa. 

"Lakini huwezi kuidharau Simba Sports Club, Simba imeimarika sana sana na faida kwao ni ile mentality ya wachezaji na benchi la ufundi, uongozi pamoja na mashabiki kwamba katika uwanja wao wa nyumbani ndio sehemu ya kukusanya alama tatu" anasema Mzinga.

Mchezo wa Simba dhidi ya Ahly utakua wapili kwao kwenye michuano hiyo hatua ya makundi baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini DR Congo dhidi ya AS Vita.