Habari

Muhubiri Shepherd Bushiri Atoroka Mkono wa Sheria Afrika Kusini na Kukimbilia Malawi

Yeye na mkewe walikamatwa mnamo Oktoba kwa madai ya ulaghai, wizi na utapeli wa pesa, ubadhirifu na utakatishaji fedha wenye thamani ya zaidi ya TZS bilioni 15 pamoja na washtakiwa wenzao watatu.

Muhubiri wa milionea ambaye Maisha yake binafsi na utumishi wa kiimani umegubigwa na utata Shepherd Bushiri, ambaye alikuwa nje kwa dhamana nchini Afrika Kusini katika kesi ya madai ya ulaghai na utapeli wa pesa, amekimbia nchi na kuelekea Malawi, nchi aliyozaliwa.


Bushiri ambaye anafahamika zaidi kama Nabii, cheo ambacho alijipa mwenyewe anajulikana kwa "miujiza" yake na maisha ya kifahari na amefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya madini, mawasiliano ya simu na starehe.


Mnamo mwezi Oktoba, Bushiri alikamatwa kwa madai ya ulaghai na utapeli wa fedha, katika kesi iliyohusisha mamilioni ya dola lakini alipata dhamana mnamo Novemba.


Kiongozi huyo wa Kanisa la Christian Gathering Church (ECG) na mkewe walikamatwa mnamo Oktoba kwa madai ya ulaghai, wizi, na utapeli wa pesa, ubadhirifu na utakatishaji fedha wenye thamani ya zaidi ya TZS bilioni 15 pamoja na washtakiwa wenzao watatu.


Wanandoa hao waliachiliwa kwa dhamana ya TZS milioni 29 kila mmoja zaidi ya wiki moja iliyopita na Mahakama ya Hakimu wa Pretoria.


Utajiri wake unatokana na michango kutoka kwa wafuasi wa kanisa lake la Enlightened Christian Gathering lililopo kwenye mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria.

Bushiri na mkewe, Mary, walipewa dhamana kwa sharti kwamba hawatotoka kwenye eneo jimbo la Gauteng, Afrika Kusini.


Bushiri, katika taarifa yake Jumamosi, alisema amekimbia Afrika Kusini kwani anahofia maisha yake.

"Kumekuwa na majaribio ya wazi na dhahiri ya mimi mwenyewe, mke wangu na familia yangu kuuawa na ... hakujawahi kuwa na ulinzi wa serikali," alisema.

"Kwahiyo, kuja kwetu Malawi, ni kujiondoa kwa busara kutoka Jamhuri ya Afrika Kusini ili maisha yetu yawe salama," ameongeza Bushiri.


"Lazima tuwe hai kushuhudia.", amesema.


Kumekuwa na madai kwamba Bushiri alikimbia Afrika Kusini kwenye ndege ya Rais wa Malawi Lazarus Chakwera, ambaye alikuwa katika ziara rasmi ya siku mbili nchini Afrika Kusini na kurudi Jumamosi.

Lakini msemaji wa Chakwera Brian Banda alisema Nabii huyo hakuwa kwenye ndege ya Rais.


"Madai kwamba Nabii Shepherd Bushiri alikuja kwa ndege moja na Rais ni ya uwongo," alisema.


Hii ni kesi ya pili ya utakatishaji fedha ambayo mashirika ya kutekeleza sheria ya Afrika Kusini yanafuatilia dhidi ya kiongozi huyo wa kanisa anayetajwa kuwa miongoni mwa wahubiri matajiri wa bara la Afrika.


Bushiri amekuwa akiandamwa na kashfa na uchunguzi tangu kuzindua kanisa la haiba lenye mafanikio linaloitwa Enlightened Christian Gathering (ECG).


ECG ilitaja kukamatwa kwa Bushiri anayeitwa 'Meja One' au 'Papa' na mkewe kama "vita" lakini akasema atatii sheria za nchi hiyo.