Tanzania

Mtemvu; Wananchi Kagueni Miradi ya Maendeleo Jimboni, ni Wajibu Wenu

Ni muhimu nanyi mkague na kutoa maoni yenu kwa ajili ya maboresho

Mbunge wa jimbo la Kibamba, Dar es Salaam, Issa Mtemvu amewataka wananchi wa Kibamba kutimiza wajibu wao wa kukagua miradi inayoendelea katika maeneo ya jimbo hilo badala ya kudhani kazi hiyo ni ya mbunge, madiwani na viongozi wa serikali za mtaa pekee.

 

Mtemvu ameyasema hayo kwa wananchi wakati alipotembelea maeneo mbalimbali ya jimbo la Kibamba kwa lengo la kukagua miradi pamoja na kutoa shukrani kwa wakazi wa Kibamba kwa kumpigia kura katika uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, 2020. Katika ziara ambayo aliianza mapema mwezi Disemba, 2020, Mtemvu alitembelea kata zote sita za jimbo la Kibamba na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa ujenzi wa kituo cha afya kinachoendelea kujengwa katika kata ya Matangini, mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari Saranga, Ujenzi wa shule ya sekondari iliyopo katika mtaa wa Ukombozi, ukaguzi wa ofisi ya kata ya Saranga pamoja na ujenzi wa barabara kutoka Matangini kwenda King’ongo.

 

Akizungumza na wakazi wa kata ya Saranga, Mtemvu amewashukuru wananchi kwa kumchagua;

 

“Nawashukuru sana kwa kunichagua katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28. Nawashukuru kwa kuniamini. Kipimo chenu cha imani mlichonionesha ni kikubwa sana, sina cha kuwalipa zaidi ya kwenda kutekeleza yale niliyoahidi wakati wa kampeni. Kwangu ni heshima kubwa mmenipa na naahidi sitowaangusha Bungeni.” - Alisema Mtemvu.  

 

Mtemvu amewakumbusha wananchi kushirikiana na ofisi ya Mbunge na viongozi wote walio katika ngazi ya jimbo kuhakikisha kuna usimamizi imara wa miradi katika jimbo la Kibamba. 

 

“Nawasihi wananchi wa kibamba kuwa sehemu ya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa ndani ya jimbo na hata katika ngazi ya kata zenu. Mimi kama Mbunge mwenye jukumu hilo inawezekana kwangu nikaona kitu fulani kipo sawa kutokana na uelewa wangu kumbe kwenu wananchi mambo yakawa tofauti. Ni muhimu nanyi mkague na kutoa maoni yenu kwa ajili ya maboresho.” - Aliongeza Mtemvu. 

 

Wakati wa ukaguzi wa miradi, Mtemvu alionesha kutokufurahishwa na kasi ya utekelaji wa miradi hiyo na kuwataka wote waliopewa kandarasi hizo kuhakikisha wanaongeza kasi ya utekelezaji ili kuendana na mahitaji na kuharakisha maendeleo jimboni humo.  

 

Sambamba na hayo, Mtemvu alitoa maelekezo kwa watendaji wa kata kumfikishia taarifa muhimu za utekelezaji wa shughuli za maendeleo ikiwemo taarifa ya zoezi la urasimishaji wa ardhi katika mitaa yote ya jimbo la Kibamba ili kurahisisha zoezi la kufuatilia na kufanya tathmini. 


Baada ya uchaguzi  Mkuu wa Oktoba 2020, wabunge wameendelea kutekeleza wajibu wao wa kuwawakilisha wananchi. Hata hivyo, hatua ya Mtemvu kuwakumbusha wananchi wajibu wao ni muhimu sana hasa kwa kuzingatia mamlaka waliyonayo wananchi katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na ufanisi unaotakiwa.