Michezo

Mpira ni Maandalizi si Hamasa

Mpira wa miguu ni mchezo unaohitaji mbinu na ufundi mwingi ili kupata matokeo mazuri na kuweza kushindana katika ngazi za juu

Watanzania wengi wana kiu ya kuona timu yao ya taifa inacheza soka safi na kupata matokeo baada ya kuona timu ikidorora mara nyingi licha ya kufuzu katika michuano ya AFCON iliyopita.

Maandalizi si kwa ajili ya mechi tu, swala hili linajumuisha kuandaa vijana tangu wakiwa wadogo ili kuweza kuwa wachezaji wazuri katika timu ya taifa pindi wanapokuwa wakubwa kadhalika pia na kuwa na aina fulani ya soka.

Vijana chini ya miaka 23 na 20 wamekuwa wakifanya vizuri katika michuano mingi huku asilimia kubwa ya wachezaji hao wanaong'ara kwenye michuano hiyo ya vijana wamekuwa wakikosa mwendelezo wa vipaji vyao kutokana na usimamizi mbovu wa maendeleo ya vijana.

Hii imepelekea kutegemea wachezaji walewale kwenye kikosi cha timu ya taifa (Taifa Stars) ambao wengine umri umeshawatupa mkono na vipaji vimeshaanza kufifia hali inayopelekea kupata matokeo mabaya kwa timu ya taifa, ' Taifa Stars'

Maandalizi ya timu ya taifa mara nyingi yamekuwa yakiegemea katika kuhamasisha mashabiki kuujaza uwanja kuliko kutoa ya  nafasi ya kutosha kwa timu kukaa na kocha ili aweze kukaa na wachezaji na kuweka falsafa yake katika timu.

Kocha Etienne Ndayiragije baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Tunisia alinukuliwa akisema "Kila kitu kwenye mpira wa miguu kinaandaliwa kwahiyo maandalizi yetu yaliishia hapo, ikiwa tunahitaji kwenda mbele zaidi inabidi tuongeze maandalizi", kadhalika kocha huyo pia alidai amekua na siku tatu tu za kuiandaa timu.

Wizara ya Michezo ya Serengeti Post tumeangazia mwenendo wa kocha huyo tangu alipochukua majukumu ya kukinoa kikosi cha Taifa Stars.

Tangu kocha Etienne Ndayiragije achukue mikoba ya Amunike, amecheza mechi 12 na kushinda mechi mbili tu huku akitoa sare mechi 6 sawa na wastani wa asilimia 16.7%.

Ndayiragije ni kocha anayependa timu yake imiliki mpira na kukaba kuanzia juu (High Pressing) lakini falsafa yake bado haijaanza kuzaa matunda katika kikosi cha Taifa Stars na mara nyingi amekuwa mhanga wa mfumo wake mwenyewe.

Katika mechi mbili alizocheza dhidi ya Tunisia zimeonyesha mapungufu makubwa katika mfumo wake. Mechi ya kwanza alicheza kwa mfumo wa 4-1-4-1 na mechi ya pili 4-2-2-2 au 4-4-2 pindi timu inapojilinda. Mifumo hii imekua ikiacha nafasi kubwa katikati ya uwanja na ndipo Tunisia walipotumia kupeleka mpira mbele.


Hali hiyohiyo ilijirudia katika mechi ya marudiano iliyochezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa kama inavyoonekana hapo chini.


Hivyo basi ili kupeleka timu mbele kimafanikio maandalizi yanapaswa kuanzia katika ngazi ya vijana, vilabu viwape nafasi wachezaji wazawa na kocha wa timu ya taifa apewe muda wa kutosha wa kukutana na wachezaji ili kuweza kuweka falsafa zake sawa na kuweza kurekebisha makosa mbalimbali ya kimfumo.

(Picha: BeIn Faisal)