Afrika

Moto Wamuwakia Askofu Uganda Baada ya Kuchepuka na Mke wa Mtu

"Ni kwa moyo mzito sana ninawaarifu kwamba mtangulizi wangu, Askofu Mkuu mstaafu Stanley Ntagali, amejihusisha na mapenzi ya nje ya ndoa na mke wa mtu na sasa Ntagali haruhusiwi kufanya sakramenti, kuhubiri, au kuwakilisha Kanisa la Uganda kwa njia yoyote hadi hapo itakapotangazwa tena," Taarifa ya kanisa ilieleza

Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la kianglikana Uganda, Stanley Ntagali amesimamishwa kutekeleza majukumu ya ukuhani baada ya kumsaliti mke wake na mke wa mtu.

Barua iliyotolewa na Askofu Mchungaji Stephen Samuel Kaziimba Mugalu kwa Maaskofu wa Anglikana mnamo Januari 13 wakati wa mkutano wa Kiinjili (GAFCON) ilithibitisha kusimamishwa kazi kwa Askofu Ntagali.

"Ni kwa moyo mzito sana ninawaarifu kwamba mtangulizi wangu, Askofu Mkuu mstaafu Stanley Ntagali, amejihusisha na mapenzi ya nje ya ndoa na mke wa mtu, suala ambalo hata yeye amekiri. Uzinzi huu ni usaliti katika ngazi nyingi. Askofu mkuu mstaafu Ntagali amemsaliti Bwana na Mwokozi wake, mkewe na nadhiri zao za ndoa, na pia imani ya Waganda wengi na Wakristo ulimwenguni ambao walitarajia angeishi kulingana na imani anayotangaza, " sehemu ya barua hiyo ilieleza.

Kaziimba alifafanua zaidi kuwa amemjulisha Ntagali kwamba haruhusiwi kufanya sakramenti, kuhubiri, au kuwakilisha Kanisa la Uganda kwa njia yoyote hadi hapo itakapotangazwa tena. Kaziimba pia alilihakikishia Kanisa kuwa sasa wamejikita zaidi katika uwazi na huduma za kichungaji kwa wahanga wote wa masuala kama haya.

Hata hivyo Askofu Ntigili amekiri kosa na kuomba asemehewe kwa tukio alilolifanya.