Afrika

Mfahamu Mwanamama Diezani Alison-Madueke wa Nigeria, Anayetafutwa Kwenye Nchi Tatu kwa Makosa ya Ubadhirifu Mkubwa Katika Historia

Alison-Madueke anatuhumiwa kwa ufisadi, matumizi mabaya ya zaidi ya dola bilioni 20 sawa na takribani TZS trilioni 46.3 na matumizi mabaya ya madaraka wakati alikuwa Waziri wa Mafuta

Mwanasiasa wa Nigeria na Rais wa kwanza mwanamke wa Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC), Diezani K. Alison-Madueke amekuwa kwenye habari kote duniani kufuatia madai ya mwenendo wa kifedha ambao umekuwa ukimzunguka kwa muda sasa.

 

Kuibuka kwake hadi kuwa Rais wa OPEC hakukutokea kwa bahati. Mwaka 2007 alikua Waziri wa Uchukuzi wa Nigeria. Miaka iliyofuata alifanya kazi katika Wizara ya Madini na Maendeleo ya Chuma na mnamo 2010, aliteuliwa kuwa Waziri wa Rasilimali za Mafuta.

 

Walakini, tangu aachie madaraka mnamo 2015, Allison-Madueke amehusishwa katika visa vya udanganyifu na matumizi mabaya ya fedha za umma huko Nigeria, Uingereza, Italia na Marekani.

 

Kwa mujibu wa Taasisi ya Kukabiliana na Ufisadi ya Nigeria, alihusika katika vitendo vya ulaghai na ubadhirifu wakati wa uwaziri wake huku mashtaka kadhaa yaliyotolewa dhidi ya Alison-Madueke yamejikita juu ya wakati akishikilia nyadhifa ya usimamizi wa sekta ya mafuta ambayo ni chanzo kikubwa cha ukuzaji uchumi kwa taifa la Nigeria.

 

Madai haya yanaungwa mkono na Idara ya Haki ya Marekani (US Justice Department) ambayo imemtaja Alison-Madueke kama sehemu ya kesi inayotaka kurudisha mali yenye thamani ya TZS bilioni 334 inayodaiwa kutokana na vitendo vya rushwa na ufisadi. Mali hizo ni pamoja na ghorofa ya kifahari TZS bilioni 116 lililopo huko New York na boti binafsi la kifahari lenye thamani ya TZS bilioni 186.

 

Vilevile, Alison-Madueke anatuhumiwa kwa ufisadi, matumizi mabaya ya zaidi ya dola bilioni 20 sawa na takribani TZS trilioni 46.3 na matumizi mabaya ya madaraka wakati alikuwa Waziri wa mafuta nchini Nigeria na uchunguzi umekuwa ukiendelea kwa miaka minne sasa.

 

Kwa mujibu wa Tume ya Uhalifu wa Kiuchumi na Fedha ya Nigeria (EFCC) jumla ya Naira bilioni 47.2, sawa na TZS bilioni 288 pamoja na kiasi kingine cha dola milioni 487.5 sawa na TZS trilioni 1.1 tayari zimepatikana kwa Waziri huyo wa zamani. Yapo madai pia kuwa anamiliki kiasi kingine cha Naira 23,446,300,000 sawa na TZS bilioni 143 katika mabenki mbalimbali ya Nigeria, huku akitajwa kumiliki vito vya thamani mbalimbali vyenye thamani ya dola milioni 5, sawa na takribani TZS bilioni 11.6, fedha za madafu.

 

Mnamo mwezi Juni, wapelelezi kutoka Uingereza walifika Nigeria kwa kile kilichoonekana kama kukamilisha uchunguzi kabla ya maandalizi ya kesi ya ufisadi na ubadhirifu dhidi ya Alison-Madueke.

 

Tayari baadhi ya mali za mwanamama huyo, kama majumba yaliyopo Banana Island yenye thamani ya TZS bilioni 87, Heritage Court Estate, Plot 2C, Omerelu Street, Diobu Port Harcourt; 135 Awolowo Road/ Plot 808 Awolowo Road, Ikoyi; na 7, Hurnburn Street na 5, Raymond Street, Yaba, Lagos zimeshataifishwa na mamlaka tayari kwa kupigwa mnada, kwa mujibu wa ripoti.

 

Vito vya thamani vyenye thamani ya TZS bilioni 93 vinavyojumuisha bangili, pete, na saa za mkononi zilipatikana kutoka kwenye nyumba zinazohusishwa kumilikiwa na Waziri huyo wa zamani aliyekuwa mwenye nguvu kubwa Nigeria hadi kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Nchi zinazoongoza Uzalishaji mafuta duniani (OPEC).


Inaripotiwa kuwa vito vya thamani vya Alison-Madueke vilivyotaifishwa tayari vipo mnadani kuuzwa na madalali wa Kimataifa watauza vito hivyo, na vile vile, nyumba za kifahari zilizopatikana, kwa mujibu wa Kaimu Mwenyekiti wa EFCC, Ibrahim Magu.

 

Kwasasa Diezani yuko wapi? Inaweza kuwa jambo la kushangaza, lakini katika nyakati za mwisho akiwa madarakani Rais wa zamani wa Nigeria, Dr Goodluck Jonathan, Diezani naye alikuwa ameshanusa harufu ya kushitakiwa kwa ufisadi wake uliokubuhu na kuvunja rekodi nyingi.

 

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na vyombo mbalimbali na nyaraka za Mamlaka ya Kukabiliana na Makosa ya Kiuchumi na Ufisadi Nigeria, Mwanamama Diezani Alison-Madueke alishawishi na baadaye kukubaliwa na Serikali ya Dominica ili awe raia wan chi hiyo, na cha ziada akapewa cheo kama Kamishna wa Biashara na Uwekezaji wa Taifa hilo la Amerika ya Kusini. Cha ziada, Alison-Madueke alifanikiwa kushawishi na kupatiwa hati ya kusafiria (Passport) ya kidiplomasia inayofanya asiweze kukamatwa na chombo chochote cha dola ikiwamo Interpol ili kurudishwa Nigeria kujibu mashtaka.

 

Inaripotiwa kuwa, kabla ya kuachia ngazi na kuondoka tarehe 28 Mei 2015, Diezani alishaingia makubaliano na ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Dominica na hivyo kujihakikishia usalama wake. Anaimarishwa na ngao ya kidiplomasia ambayo hakuna mamlaka ya usimamizi wa sheria ulimwenguni inaweza kupuuza. Mbali na hilo, uraia wake wa Uingereza ni kinga ambayo amekuwa akitumia dhidi ya kurudishwa kwao Nigeria, kujibu mashtaka mengi ya ufisadi dhidi yake