Habari

Mfahamu mshindi wa Tuzo ya Maji Maji 2020

Fatma Karume na Masoud Kipanya watambuliwa kwa kuingia tano bora

Usiku wa Disemba 10, 2020 ulishuhudia tukio la kihistoria la utoaji tuzo za Haki za Binadamu za Maji Maji tukio ambalo hufanyika mara moja kila baada ya miaka mitano. Usiku wa Tuzo ya Maji Maji ulikuwa pia kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu ambayo huadhimishwa Disemba 10 kila mwaka. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilikutanisha wadau wa haki za binadamu kushuhudia zoezi la kuwatambua watetezi wa haki za binadamu waliotetea haki za binadamu kwa ujasiri katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2015 mpaka 2020. 

 

Katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Hayati Godfrey Luena alitunukiwa tuzo hiyo baada ya kupata alama nyingi zaidi kutoka kwa jopo la majaji. Jopo la majaji lililoundwa na watu mashuhuri na wenye uzoefu mkubwa katika utetezi wa haki za binadamu lilipitisha majina matano kutoka katika majina 32 yaliyochujwa kutoka katika mapendekezo ya wananchi na baadae kutoa alama kwa wanaharakati hao walioingia tano bora na hatimaye kumpata Godfrey Luena.

 

Jopo la majaji ambalo liliongozwa na mwanaharakati nguli na Mkurugenzi Mtendaji Mstaafu wa LHRC, Dkt. Helen Kijo-Bisimba liliundwa na Dkt. Helen mwenyewe, Jenerali Ulimwengu (mwanahabari nguli na mtetezi wa haki za binadamu), Tom Bahame Nyanduga (Mwenyekiti wa Zamani wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na mtetezi wa Haki za Binadamu), Dkt. Benson Bagonza (Kiongozi wa dini na mtetezi wa Haki za Binadamu) pamoja na Aidan Eyakuze (Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza na mtetezi wa Haki za Binadamu). 

 

Watetezi wengine walioingia katika orodha ya tano bora ya majaji ni pamoja na Ally Masoud (Kipanya) – ambaye amekuwa akitetea haki za binadamu na kuhimiza utawala bora kupitia kazi yake ya uchoraji katuni na utangazaji. Fatma Karume ambaye amekuwa akitumia taaluma yake ya sheria kuhimiza utawala wa sheria pia aliingia tano bora. Roby Samwelly, mtetezi wa haki za wasichana na wanawake mkoani Mara pia aliingia tano bora. Vicky Ntetema ambaye ni mwanahabari nguli na mtetezi mashuhuri wa haki za watu wenye ualbino alihitimisha orodha ya tano bora. 

 

Wote walioingia tano bora walitunukiwa vyeti vya utambuzi kama watetezi wa Haki za Binadamu waliojitoa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kutetea haki za binadamu bila kujali vitisho.