Habari

Marekani Yaweka Vikwazo vya Viza kwa Maafisa wa Tanzania

Bila kutaja majina ya maafisa waliowekewa vikwazo, Marekani inawatuhumu maafisa hao kwa kuingilia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020

Marekani imetangaza kuwawekea vikwazo vya kuingia nchini humo maafisa wa Tanzania ambao nchi hiyo inawatuhumu kwa kile wanachokitaja kuwa kuingilia uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka 2020.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo, Waangalizi wa uchaguzi na mashirika ya kiraia wanadai kuwepo kwa udanganyifu katika uchaguzi huo pamoja na uvunjifu wa haki za binadamu wakati na baada ya uchaguzi.


Taarifa hiyo imeongeza kuwa Marekani itaendelea kufuatia kwa ukaribu mwenendo wa mambo nchini Tanzania na haitasita kuwachukulia hatua wale wote inaodai kuwa wanaminya demokrasia na haki za binadamu.

Taarifa hiyo inakuja siku moja kabla ya utawala wa Rais anayemaliza muda wake, Donald Trump, kumalizika, ikiacha wasiwasi ikiwa utawala mpya wa Joe Biden utatekeleza hatua hiyo. Katika hali inayoonesha msuguano dhahiri baina ya viongozi hao wawili, ofisi ya Biden imesema kuwa itatengua sera kadhaa za Trump mara tu baada ya kuingia ofisini.


Utawala wa Trump utakumbukwa kwa kuwekea vikwazo vya usafiri mataifa ya Afrika pamoja na baadhi ya viongozi wa mataifa ya Afrika, akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwa kile Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilichokiita "kuwalenga watu waliotengwa katika jamii wakiwemo mashoga, kuukandamiza upinzani pamoja na uhuru wa kujieleza."