Maoni

MAONI: Wasanii wa Nigeria Wanavyoacha Alama Katika Taifa lao; Je Wasanii wa Tanzania Wanatimiza Wajibu wao Kwa Jamii?

Na Michael Mallya

Nimetamani kuandaa makala iliyojaa maswali juu ya maswali walau nipunguze maoni yangu katika mada hii lakini bado kiu yangu ya kutoa maoni imenisukuma kutema nyongo.

 

Ndiyo! Ni rahisi kuwazungumzia wengine na kuchambua mchango wao bila kujali sisi tunafanya nini lakini ni lazima tukubaliane kwamba kila mmoja wetu ana wajibu kwa jamii. Wajibu kwa jamii ni hali ya kufanya jambo linalolinda maslahi ya umma bila kujali zaidi faida ya mtu binafsi.

 

Kila mmoja wetu ana wajibu kwa jamii na nchi yake na hata mamlaka za nchi zimekuwa zikisisitiza kila raia kutimiza wajibu. Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kutoa nukuu kwamba kama mtu atasomeshwa na wananchi/serikali na akashindwa kutumia maarifa aliyoyapata kuisaidia jamii/nchi yake basi mtu huyo anakidhi vigezo vya kuwa msaliti. Huu ulikuwa mfano wa elimu pekee, tukienda kwenye masuala mengine ya kijamii ni wazi kwamba kila ambacho mtu anakivuna kutoka kwa jamii kinamvisha jukumu la uwajibikaji kwa jamii hiyo. Mfano, mtu anapochaguliwa kuwa kiongozi katika jamii fulani, mtu huyu anavikwa taji la wajibu kwa jamii yake. Taji hili haliishii kwa viongozi pekee bali kwa kila mtu anayetegemea umma kujenga hadhi yake – kuanzia mfanyabiashara, msanii, mwanazuoni, mwanasiasa, mwanamichezo na wengine.

 

Kuna mambo kadhaa ambayo mtu akiyafanya yanaweza kuhesabika kwamba anawajibika kwa jamii. Mfano, kwa mfanyabiashara kuhakikisha bidhaa au huduma unayotoa haiathiri afya ya umma. Mwekezaji kuhakikisha uwekezaji wako hauharibu mazingira na kuhakikisha kuna afua kwa wahanga wa madhara yoyote yanasababishwa na uwekezaji wako. Mwanahabari kuhakikisha unaandaa habari zitakazodumisha maendeleo ya kweli ya nchi yako na kuepuka kunufaisha watu wachache.

 

Kwa vile makala hii imejikita katika sanaa ni muhimu kutazama uwajibikaji kwa jamii kwa upande wa wasanii unaweza kupimwa vipi. Kabla ya kuangalia uwajibikaji wa wasanii naomba nikiri kwamba wasanii ni moja ya kundi kubwa ambalo lina ushiwishi mkubwa mtu mmoja mmoja na kwa jamii nyingi kama sio jamii zote. Wasanii hutumia njia za kibunifu kufika katika mioyo ya watu na kufungua vifungo vya hisia zao bila kutumia nguvu kubwa ya ushawishi. Wasanii hugusa hisia za wengi kwa kazi zao za muziki, uchoraji, densi, maigizo, ushairi, na nyinginezo. Uwezo wao wa kuamsha na kuchochea hisia za wengine umewafanya wasanii kuwa maarufu na hata kuwa na nguvu kubwa ya kushawishi maamuzi ya wengi hasa kwa kuzingatia kwamba kila binadamu ni dhaifu linapokuja suala la hisia.

 

Wasanii kote duniani hupata umaarufu mkubwa na kuwa na wafuasi halisi hata kuzidi viongozi wa kisiasa. Nguvu hii imewafanya wasanii kuwa mawakala wa mabadiliko ya tamaduni na mifumo mbalimbali ya maisha. Mfano wasanii wengi wamekuwa mawamakala wa mitindo ya mavazi, mionekano na hata maamuzi ya manunuzi na maamuzi ya kisiasa na kijamii. Tumeshuhudia wasanii wakitumika kama mabalozi wa bidhaa na huduma mbalimbali na kwingineko wakitumika kama mabalozi wa wanasaisa, vyama vya siasa, vilabu vya michezo, taaisisi na makampuni kwa lengo la kuwashawishi watu kuwa wafuasi.

 

Tukumbuke kwamba nguvu hii ya ushawishi hujengwa na wanajamii wanaomzunguka msanii bila kujali mikakati inayotumia na msanii husika. Watu au jamii ndio nguvu ya kila msanii nah ii ndio sababu hasa kwa wasanii wa sasa wamekuwa wakijipima kwa idadi ya wafuasi walionao katika mitandao au hata idadi ya mashabiki wanaojitokeza katika majukwaa ya ana kwa ana na majukwa ya mtandao. Watu wamekuwa ni mtaji mkubwa kwa wasanii kama ilivyo kwa makundi mengine kama wanasiasa na wafanyabiashara na hii ndio sababu kubwa inayonifanya kuwakumbusha wasanii jukumu lao la kuwajibika kwa jamii.

 

Kuna mabadiliko mengi ambayo yamepiganiwa na wasanii katika maeneo na Nyanja mbalimbali kote duniani. Tumekuwa na wasanii ambao walipigania utu wa binadamu kwa kupinga utumwa, ubaguzi wa rangi na utawala wa kikoloni. Majina kama Bob Marley, … ni baadhi ya majina makubwa kimataifa ambayo sauti zao ziliunguruma katika kupigania utu na alama yao imebaki. Nchini Marekani ambako biashara ya muziki ilizaliwa na kuendelezwa, wanamuziki wengi mpaka leo wameendelea kutumia talanta zao kutetea maslahi ya umma kwa kutetea mambo yenye maslahi kwa umma na kupinga mambo yasiyo na maslahi kwa Wamarekani ikiwemo ubaguzi wa rangi.

 

Tukirudi barani Afrika, tumekuwa na wasanii kama Fela Kuti wa Nigeria na Youssou N’Dour wa Senegal ambao wametumia sanaa na umaarufu wao kupigania maslahi ya umma ikiwemo haki za kiraia na kisiasa katika nchi zao. Nchini Afrika Kusini ambako ubaguzi wa rangi ulishamiri kwa kipindi kirefu wamekuwepo wasanii kama Hugh Masekela, Miriam Makeba, Brenda Fassie na wengine ambao walitumia kipaza sauti kupinga udhalimu dhidi ya watu weusi.

 

Nyumbani Tanzania tumekuwa na wasanii wachache ambao wamekuwa wakipinga vitendo vinavyodhoofisha maslahi ya umma ikiwemo rushwa, ukatili, utawala usiozingatia sheria na haki sambamba na kutokuwajibika kwa watu walio katika mamlaka. Majina ambayo mpaka sasa yamebaki ni pamoja na Vital Maembe na Roma Mkatoliki.

 

Nchini Nigeria, taifa lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika wasanii hasa wa kizazi kipya wametumia nguvu yao vyema kuwajibika kwa jamii kwa kujitosa barabarani na kutumia mitandao yao ya kijamii kupinga ukatili wa polisi nchini humo. Hivi karibuni wananchi wa Nigeria walichukizwa na tukio la mauaji yaliyofanywa na kikosi maalumu cha kupambana na wahalifu Special Anti-Robbery Squad (SARS) na kuamua kuchukua hatua kwa kuandamana kuzitaka mamlaka zifute kitengo hicho. Katika hali ambayo haikutarajiwa na wengi wasanii wakubwa kwa wadogo nchini humo walishiriki maandamano hayo wakiwaunga mkono raia wenzao kupingana na ukatili uliofanywa na SARZ na kupelekea serikali kuwajibika kwa wananchi kwa kufuta kitengo hicho.

 

Jambo hili si geni kwa mataifa ya magharibi kwani wasanii wengi wanatambua wajibu wao kwa umma na wanawajibika pale linapojitokeza suala la maslahi ya umma. Kwa Afrika, wasanii wengi hasa wenye umaarufu mkubwa na ushawishi mkubwa kwa jamii zao, wamekuwa wakijitenga na masuala ya umma hasa inapohitajika serikali kuwajibika. Wasanii wengi hasa Tanzania wamekuwa wakijituma kwenye kampeni zenye maslahi ya kifedha au umaarufu kwao binafsi na kujikuta wakikaa kimya pale maslahi ya umma yanaposiginwa.

 

Wasanii wetu wa Tanzania wanaweza kuwa na maelezo mengi katika hili lakini hawawezi kuepukana na rungu la wakosoaji kama mimi kwamba wasanii wamejikita katika maslahi binafsi zaidi. Wasanii wengi wamekulia katika mazingira ya kawaida hivyo wanatambua changamoto zilizopo mtaani, wengi ni wahanga wa vitendo kama rushwa, uporaji wa haki kama haki za hatimiliki na hata ukatili wa aina mbalimbali lakini wasanii wetu wamechagua kulinda maslahi binafsi na kuachana na mambo ya umma. Wananchi wamewapa nguvu kubwa lakini wanaitumia nguvu hii kwa matakwa yao.

 

Staa wa muziki, Wizkid akiwa kwenye maandamano ya #EndSARS

Hili la wasanii wakubwa wa Nigeria kama kina Davido, Wizkid, Yemi Alade, Patoranking na wengine waliojitokeza mtaani na kupitia mitandao kupinga ukatili wa polisi nchini humo na kuisukuma serikali kuchukua hatua za mageuzi ya utendaji wa jeshi la polisi nchni humo ni somo kubwa kwa wasanii wetu kwamba mbali na kufanya muziki kwa lengo la kujikwamua na umasikini, wasisahau wajibu wao wa kusimamia maslahi mapana ya jamii.