Tanzania

Maoni: Rich Mavoko, bidhaa adimu inayosuasua katika soko la muziki

Mavoko angeweza kuwa katika tatu bora ya wasanii wakubwa Tanzania kama angekubali kujipa changamoto

Richard Martin Lusinga maarufu zaidi kama Rich Mavoko ni kipaji kikubwa katika muziki wa kizazi kipya Tanzania. Kipaji cha Rich Mavoko kimejidhihirisha kupitia kazi nzuri ya muziki anayofanya. Tangu alipojitambulisha rasmi katika soko la muziki wa kizazi kipya, Mavoko ameendelea kuburudisha wapenda muziki bila kuchuja. 

 

Nimepata bahati ya kusikiliza muziki wake na kujiridhisha kwa sauti, uwezo wa kuandika na kuandaa melodi nzuri, hii inafanya muziki wake kutochosha kusikiliza. Hadi sasa ukisikiliza nyimbo za mwanzo kabisa za Rich Mavoko kama Marry Me, Silali, Pacha Wangu, Roho Yangu, One Time, Uzuri Wako na nyinginezo utakubaliana na mimi kwamba Rich Mavoko ni moja ya vipaji vikubwa katika muziki wa Tanzania. Miaka ya 2010, Rich Mavoko alishindanishwa na vipaji vilivyokuwa vikitikisa soko la Bongo Fleva kwa wakati huo. Rich Mavoko aliwekwa ngazi moja na majina makubwa kama Diamond Platnumz, Belle 9, Ben Paul na Ommy Dimpoz.

 

Ukiacha uwezo wa kuandika na kuimba, Rich Mavoko amejaaliwa uwezo wa kutumbuiza kwa kucheza mitindo mbalimbali ya muziki na huenda hili lilifanya mashabiki wa muziki kumshindanisha sana Rich Mavoko na Diamond Platnumz wakati huo wote wakiwa katika ubora wao. Hata hivyo, historia ya ushindani kati ya Rich Mavoko na Diamond Platnumz iliyeyuka mwaka 2016 baada ya Rich Mavoko kusaini mkataba na lebo ya WCB iliyo chini ya Diamond Platnumz.

 

Safari ya Rich Mavoko ndani ya WCB ilitabiriwa kuwa nzuri hasa kwa kutazama namna ambavyo lebo hiyo imesimamia wasanii kwa mafanikio. Ndani ya WCB kipaji cha Rich Mavoko kilizidi kukolea ladha akiachia vibao vikali kama Ibaki Story, Rudi, Kokoro, Sheri na Show Me. Akiwa WCB, Rich Mavoko aliendelea kudhihirisha kwamba kipaji huwa hakifichiki kwani ladha ya muziki wake ilipata upenyo bila kujali idadi ya wasanii walio chini ya lebo ya Wasafi. 

 

Wakati mashabiki wakisubiri makubwa zaidi kutoka kwa Mavoko, ghafla mwaka 2018, safari ya Mavoko ndani ya Wasafi ilifika mwisho bila kuwepo kwa maelezo yaliyonyooka kutoka kwa pande zote. Kama shabiki wa kweli kabisa wa Mavoko niliyeona umuhimu wa menejimenti nzuri kama WCB katika ukuaji wa Mavoko nilisikitika lakini sikumuhukumu kwani hakuna ajuaje kilichokuwa kwenye mkataba wake na WCB zaidi ya yeye mwenyewe Mavoko na uongozi wa WCB. 

 

Mashabiki wengi hawakumtabiria mazuri Mavoko baada ya kutoka WCB, ingawa wachache wanaoamini katika kipaji chake waliendelea kuamini kwamba Rich Mavoko hatapotea bali atatafuta namna ya kurejea katika chati. Haikuchuka muda, Rich Mavoko akaibuka na lebo yake ya Billioneakid, akaachia nyimbo kama Naogopa ambazo kiukweli hazikupokelewa kwa mshindo ambao Rich Mavoko anastahili. Ujio huu uliwafanya baadhi ya wapenzi wa muziki kukata tamaa na kuona kama Rich Mavoko alifanya kosa kutoka WCB.

 

Rich Mavoko hakukata tamaa, baadae alitangaza kuwa kimya katika mitandao ya kijamii kwa muda ili kujipanga upya na kurudi kwa kishindo ambacho wapenzi wa muziki wangeridhika nacho. Baada ya kimya cha muda, Agosti, 2020, Mavoko alizindua Mini Tape yake yenye jumla ya nyimbo nane. Katika uzinduzi huo Rich Mavoko alitangaza kusaini makubaliano kati ya lebo yake ya Billioneakid na Pili Pili Entertainment kwa lengo la kuongeza nguvu katika usimamizi wa kazi zake za muziki. Baada ya makubaliano hayo, Rich Mavoko amepata nguvu ya kusambaza mini tape yake kupitia vyombo vya habari na majukwaa mbalimbali ya muziki ikiwemo Apple Music, Boom Play, na You Tube. Pia, Mavoko amefanikiwa kutoa video zenye ubora unaokidhi viwango vya soko na kupata watazamaji wa kutosha kupitia jukwaa la You Tube. 

Wa Moto - moja ya video alizoachia Rich Mavoko hivi karibuni kutoka katika Mini Tape yake

Video alizoachia hivi karibuni zimepata watazamaji wanaotia moyo kwamba bado mashabiki wanaweza kufuatilia kazi za mavoko. Niwahi ni moja ya video mpya kutoka katika mini tape yake na tayari imefikisha zaidi ya watazamaji 1,000,000 baada ya miezi  mitatu katika mtandao wa You Tube. Katika mahojiano ya hivi karibuni, Rich Mavoko pia amebainisha kuwa na mipango ya kufanya ziara ya kimuziki ili kutambulisha ujio wake mpya kwa mashabiki wa muziki. Mipango hii ikisimamiwa vizuri naamini kila shabiki atamuona mavoko anayemtani. 

Niwahi - moja ya video mpya kutoka katika Mini Tape ya Rich Mavoko

Kama umepata bahati ya kusikiliza Mini Tape ya Mavoko utagundua ni kwa nini nasema Rich Mavoko ni bidhaa adimu inayosuasua katika soko la muziki. Mavoko ameonesha uwezo mkubwa wa kuandika na kuimba – uwezo ambao hakuna anayeutilia shaka. Shaka pekee iko katika soko, huenda Rich Mavoko akawa ni moja ya wasanii wachache wanaoamini katika kipaji pekee.

 

Kipaji katika muktadha wa muziki ni bidhaa – jinsi mwanamuziki anavyokuwa na uwezo mkubwa ndivyo anavyozidi kuwa na nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika soko. Jambo la kukubaliana hapa ni kwamba kuwa na bidhaa pekee haitoshi kumiliki soko bila kuwa na mikakati thabiti na uwezo madhubuti wa kusimamia mikakati hiyo ili bidhaa yako iweze kukubalika na kununulika. 

 

Rich Mavoko anajitosheleza kama bidhaa inayohitajika katika soko la muziki, wasiwasi wangu ni mikakati na uwezo wa kuitangaza bidhaa hiyo. Je, Billioneakid imejipanga kama ilivyo kwa WCB na Konde Gang kuwekeza kupambana na ushindani wa soko? Huenda swali hili likajibiwa na Mavoko na uongozi wake pekee lakini mimi kama mfuatiliaji wa nje naweza kuwa na machale kwamba bado nguvu ya uwekezaji kwa chapa ya Rich Mavoko haijitoshelezi. 

 

Mfano rahisi; ukitafuta taarifa muhimu kama wasifu wa Rich Mavoko na mpangilio wa nyimbo zake katika mitandao huwezi kupata – hii inaonesha ni jinsi gani timu yake bado haijajipanga kulimiliki soko la mtandao ambalo ndio soko rahisi zaidi. Mavoko angeweza kuwa katika tatu bora ya wasanii wakubwa Tanzania kama angekubali kujipa changamoto na kutafuta uwekezaji mkubwa zaidi kwa chapa yake.