Habari

Mamlaka ya Mawasiliano Uganda Yaamuru Kufungwa kwa Mitandao ya Kijamii

Watumiaji wameripoti kushindwa kutumia mitandao ya Facebook, Twitter WhatsApp na Signal tangu asubuhi, huku upatikanaji wa AppStore, PlayStore na YouTube ukiwa na changamoto pia

Mamlaka ya Mawasiliano nchini Uganda, UCC, imeamuru kufungwa kwa mitandao ya kijamii ikiwa zimesalia siku mbili tu kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini humo, gazeti la Daily Monitor limeripoti

Katika barua yake, Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Bi Irene Sewankambo ameagiza kampuni za mawasiliano nchini humo "kufunga kwa haraka upatikanaji na matumizi" ya mitandao ya kijamii. Watumiaji nchini humo wameripoti kushindwa kutumia mtandao wa Facebook, Twitter WhatsApp na Signal tangu asubuhi, huku upatikanaji wa AppStore, PlayStore na YouTube ukiwa na changamoto pia.

Chanzo cha habari kinaeleza kuwa mamlaka ya mawasiliano imetoa zaidi ya VPN 100 kwa makampuni ya mawasiliano kwa ajili ya kuhakikisha kuwa zinafungiwa nchini humo.

Mamlaka hiyo, hata hivyo, imekana kutoa agizo la kufunga mawasiliano kupitia msemaji wa UCC, Ibrahim Bbosa.

"Kumekuwa na tatizo la muunganiko hafifu wa intaneti, lakini inaweza kuwa ni kutokana na kuongezeka kwa watumiaji wakati tunaelekea katika zoezi la uchaguzi," Bbosa aliwaambia wanahabari.

Hatua hii inakuja kufuatia kauli ya Waziri wa Ulinzi na Masuala ya Maveterani kuwaambia wanahabari kuwa serikali inatafuta namna bora ya kudhibiti mitandao ya kijamii, ikidai kuwa inatumika vibaya wakati huu wa uchaguzi.

Mtandao wa Facebook umethibitisha siku ya Jumatatu kuwa umefungia baadhi ya akaunti za serikali ya Uganda kutokana na kutumiwa vibaya kwa akaunti hizo kushawishi maamuzi ya umma.

Mkuu wa Mawasiliano wa Facebook wa Ukanda wa Nchi za Kusini mwa Sahara, Kezia Anim-Addo amesema kuwa Facebook imechukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa baadhi ya akaunti za mtandao wa Facebook zimejihusisha katika jaribio la makusudi la kushawishi maamuzi ya umma, wakilenga mdahalo unaotarajiwa kufanyika kabla ya uchaguzi.

"Wametumia akaunti feki kuendesha kurasa na kuandika maoni katika machapisho ya watu, wakijivika uhusika wa watu wengine na kusambaza machapisho katika makundi na kuyafanya kuwa maarufu kuliko yalivyotakiwa kuwa," Kezia Anim-Addo alisema katika barua pepe, akiongeza kuwa mtandao wa akaunti hizo unahusishwa na Wizara ya Habari na Mawasiliano ya Uganda.

Hii ni mara ya pili kwa serikali ya Uganda kufungia mitandao ya kijamii, ambapo mwaka 2016, serikali ilifungia mtandao wa Facebook na Twitter kabla ya mgombea wa urais na mshindani wa Rais Museveni kuwahimiza wananchi kutumia VPN.