Tanzania

Mambo 7 Muhimu Aliyoyasema Jaji Warioba kwenye Maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu

''Mchakato wa uchaguzi ni njia ya kutekeleza haki za raia. Uchaguzi wa mwaka huu umekuwa na udhaifu katika utekelezaji katika maeneo fulani fulani''

Desemba 10 kila mwaka dunia huadhimisha siku ya kimataifa ya haki za binadamu. Kila Mwaka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, LHRC, huungana na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kuadhimisha siku ya kimataifa ya haki za binadamu.

Mwaka huu kauli mbiu ya siku ya maadhimisho ya haki za binadamu inahusiana na janga la virusi vya corona na imejikita katika mwelekeo wa kujenga matumaini na kuhakikisha haki za binadamu zinakuwa sehemu muhimu kwenye ujenzi wa jamii baada ya corona.

Maadhimisho ya mwaka huu yalifanyika katika ukumbi wa Golden Jubilee jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Waziri Mkuu wa Awamu ya Pili, Jaji mstaafu, Joseph Sinde Warioba. Katika hotuba yake aligusia mambo kadhaa kuhusu masuala mbalimbali lakini hasa alisisitiza kuhusu amani ya nchi.

Tunakuletea mambo saba muhimu aliyoyasema Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba kwenye maadhimisho hayo ya siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu;

 

AMANI NI TUNDA LA HAKI

Jaji Warioba amesema msingi wa haki za binadamu katika nchi yoyote duniani ni amani, amegusia kuwa amani ikitoweka haki za binadamu haziwezi kuwepo.

“Leo nataka kuzungumzia amani, amani ifahamike kuwa ni tunda la haki palipo na haki kutakuwa na amani lakini pia ni ukweli kwamba bila amani hakuwezi kuwa na haki za binadamu.”

Waziri Mkuu huyo wa zamani amesema vyanzo vya vurugu kwenye nchi nyingi duniani ni vingi lakini chanzo kimojawapo kikubwa cha kutoweka kwa amani ni siasa. Warioba amesema katika miaka 10 iliyopita dunia imeshuhudia vurugu za kisiasa ambazo zimeingilia sana haki za binadamu.

"Kati ya mwaka 2010 na 2012 yalitokea matukio mengi ya kisiasa katika nchi za Arabuni ambayo yaliitwa Arab Spring. Nchi nyingi zilihusika Tunisia, Libya, Misri, Yemen, Syria na nyingine. Kulikuwa na maandamano mengi na watu wengi walipoteza maisha. Inakisiwa watu zaidi ya laki moja kutoka nchi hizo walipoteza maisha na wengi zaidi walipata madhara ya aina mbalimbali."

Aligusia pia vurugu zinazoendelea hivi sasa katika baadhi ya nchi duniani.

"Tunavyozungumza katika nchi za Belarus, Armenia, Azerbaijan, Thailand, Hong Kong, Ethiopia, Myanmar na kadhalika. Vurugu zinazotokana na uchaguzi nazo zinatokea katika nchi nyingi. Hivi karibuni tumeona vurugu zimetokea Malawi, Senegal, Mali, Uganda, Marekani na sehemu nyingine. Watu wamepoteza maisha kupata madhara mengine. Hivi sasa Uganda iko kwenye kipindi cha kampeni na tayari watu karibu 50 wamepoteza maisha"

 

CHAGUZI ZANZIBAR

Mwenyekiti huyo wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba amezungumzia pia siasa za Zanzibar na chaguzi zake ambazo tangu enzi za ukoloni kunapotokea uchaguzi lazima kuwe na vurugu.

"Hapa nyumbani tunazo changamoto, hasa wakati wa uchaguzi, Zanzibar imekuwa na changamoto hizi tangu wakati wa ukoloni. Uchaguzi wa Zanzibar kabla ya uhuru ulikuwa na matatizo. Baada ya kurudisha mfumo wa vyama vingi matatizo yalizuka tena. Uchaguzi wa 1995 uliwagawa wananchi wa Zanzibar mpaka wakafikia hatua ya ndugu kususiana. Baada ya uchaguzi wa 2000, zilitokea vurugu, watu walipoteza maisha na wengine wakakimbia nchi. Uchaguzi wa 2015 ulifutwa na vurugu za 2020 zilikuwa chanzo cha watu kupoteza maisha pemba na Unguja.

 

UCHAGUZI TANZANIA BARA

Jaji Warioba amesema kwa upande wa Tanzania Bara hakukuwa na matatizo makubwa kwa muda mrefu, kila baada ya uchaguzi tathmini ilifanywa ili kubaini udhaifu uliojitokeza na marekebisho yalifanywa. Kwa miaka mingi hazikutokea vurugu za kuleta madhara makubwa, lakini uchaguzi wa mwaka huu umekuwa chanzo cha vurugu katika sehemu mbalimbali. Watu wamepoteza maisha Tarime, Tunduma na Ukerewe na wengine wameumiza na mali kuharibiwa.

Warioba asema kuna haja ya kufanyika tathmini kila baada ya uchaguzi ili kubaini kama kuna haja ya kufanya mabadiliko ya sheria na kanuni au taratibu za mchakato wa uchaguzi.

"Naamini wanaohusika watafanya tathmini ili kugundua udhaifu uliojitokeza na baada ya hapo mabadiliko yatafanywa kwenye kanuni, taratibu na sheria za uchaguzi. Jmabo hili ni muhimu kwa sababu kama hatua zisipochukuliwa uchaguzi utakuwa chanzo cha vurugu na kuhatarisha amani ya nchi."

 

HAKI YA RAIA KUCHAGUA

Jaji Warioba katika suala hili alianza kwa kuitaja Ibara ya 5 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa Ibara hiyo inaeleza haki ya kila raia mwenye umri wa miaka 18 kupiga kura.

"Mchakato wa uchaguzi ni njia ya kutekeleza haki za raia. Uchaguzi wa mwaka huu umekuwa na udhaifu katika utekelezaji katika maeneo fulani fulani."

Amesema kwa hali ilivyo sasa matakwa ya wananchi hayazingatiwi sana, vyama vinajali zaidi maslahi yao na pia kuna matumizi makubwa ya fedha, yaani rushwa, matokeo yake ni kwamba watu wengi wanaokubalika na wananchi hawateuliwi.

"Kwa taratibu za sasa watu wasiokubalika huteuliwa, hali ndivyo ilivyo kuhusu uongozi mzima wa Vijiji na Mitaa, Kata na hata Jimbo. Matokeo yake wananchi wanapoteza imani na baadhi yao wanasusa kupiga kura na wengine wanakuwa wepesi kufanya fujo wakishawishiwa."

 

HAKI YA RAIA KUCHAGULIWA

Warioba amesema ili mtu ateuliwe kuwa mgombea ni lazima awe na sifa za msingi, sifa hizo ambazo ziko kwenye kifungu cha 67 cha Katiba kuhusu Wabunge ni pamoja na kuwa raia mwenye umri wa miaka 21 au zaidi, anajua kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza, amependekezwa na chama cha siasa, hana ugonjwa wa akili na kadhalika.

Ghafla mwaka 2019 kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa wagombea wengi walienguliwa. Mwaka huu Tume iliengua wagombea wengi sana, taarifa zinaonyesha kwamba wagombea walienguliwa kwa makosa madogo madogo ya kujaza fomu.

"Tume ya uchaguzi ina jukumu la kutafakari sana suala hili na kufanya mabadiliko, la sivyo itaonekana Tume imeweka pembeni masharti ya Katiba na kujitungia ya kwake, imani ya wananchi itapungua na wanaweza kuingia kwenye vitendo vya kuleta vurugu."

 

HAKI YA MGOMBEA KUWA NA WAKALA

Jaji Warioba alisema kwamba Mgombea ana haki ya kuwa na wakala kwenye kila kituo cha kupigia kura, wakala anateuliwa na mgombea au chama chake. Kazi ya Tume ni kuthibitisha kwamba wakala anakubalika na mgombea na chama chake.

"Katika uchaguzi uliopita Tume iliengua mawakala wengi, Mgombea ana haki ya kuwa na wakala kwenye kituo cha kupigia kura, huyu ni mwakilishi wa mgombea sio mwakilishi wa Tume ya Uchaguzi, lakini safari hii mawakala wengi sana wameenguliwa na sio kwa sababu Wagombea wamesema sio wa kwetu hawa ni kwa taratibu nyingine za Tume ya Uchaguzi."

Jambo hili lisiporekebishwa linaweza kuwa chanzo cha baadhi ya wananchi kutoridhika na kujiingiza kwenye vitendo vya kuhatarisha amani.

 

MALALAMIKO WAKATI WA KAMPENI

Warioba amegusia kwa kusema Tume ya Uchaguzi imeunda chombo cha kupokea malalamiko kuhusu makosa yanayotendwa na wagombea wakati wa kampeni. Chombo hicho ni kama mahakama, wajumbe wake ni pamoja na wawakilishi wa vyama vya siasa. Mahakama hii inatoa adhabu, ikiwa ni pamoja na kumfungia mgombea asiendeshe kampeni kwa muda fulani.

"Ni vigumu kuamini kwamba chombo ambacho wajumbe wake ni washindani kinaweza kutenda haki, ni vema Tume ikaweka utaratibu mwingine ambao utaonekana kutenda haki bila mashaka."

Amesema amegusia hayo ili tuweze kuimarisha amani tuliyonayo kwa sababu kama Taifa tukishindwa kufanya hayo inaweza kutokea vurugu na kuingiliwa kwa haki za binadamu.