Afya

Maji yasiyo na Vijidudu Yanaweza Kutokuwa Salama kwa Kunywa

Na Ahmada Yahaya

Maji ni sehemu ya kundi la chakula na yana umuhimu mkubwa sana kiafya katika kufanikisha kazi mbalimbali mwilini. Viungo vingi vya mwili ili viweze kufanya kazi vizuri vinahitaji maji, wakati zaidi ya asilimia 60 ya uzito wa mwili wa binadamu ni maji. Maji husaidia mwili kufanya kazi mbalimbali. Kiafya, mtu mzima anashauriwa kutumia walau kiasi cha lita moja na nusu kwa siku huku watoto wanapaswa kupewa maji kulingana na uhitaji.

Kuna faida nyingi kiafya zitokanazo na matumizi ya maji safi na salama. Unywaji wa maji ya kutosha hupunguza hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo. Utafiti uliofanywa nchini Marekani kwa muda wa miaka sita unaonesha watu wanaotumia maji ya kutosha walau glasi tano kwa siku hujiepusha na hatari ya kupata maradhi ya moyo kwa asilimia 41 zaidi ya wale wanaokunywa glasi mbili au chini ya hapo.

Maji pia husaidia kuondoa sumu mwilini kwa kuondoa uchafu wote kwa njia ya haja kubwa na ndogo, mwili unapokuwa na maji ya kutosha humfanya mtu kufanya mazoezi ya kutosha na hivyo kupata faida ya mazoezi ipasavyo. Maji pia husaidia kupunguza uzito kwa sababu maji hayana mafuta, kalori wala sukari.

Lakini muhimu hapa si maji tu bali maji yanayofaaa kwa matumizi ya bindamu. Ni muhimu kutumia maji safi na salama ili kulinda afya yako kwani matumizi ya maji yasiyofaa huweza kuleta athari kiafya ikiwemo kupatwa na maradhi, huku watoto wakiwa wahanga wakubwa zaidi. Ripoti ya Umoja wa Mataifa inakadiria kuwa watoto 4,000 hufariki kila siku kutokana na kutumia maji machafu.

Edward Machege ni daktari bingwa wa afya na magonjwa ya wototo. Anasema kuna uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya maji yasiyofaa pamoja na kudorora kwa afya za watu kunatokana na dhana kuwa watu hufikiri kuwa maji ni salama kwa kuwa tu hayana wadudu.

“Watu hufikiria maji ni salama iwapo tu hayana wadudu lakini kuna kemikali zingine ambazo hazihitajiki hata kidogo kwenye maji anayopaswa kutumia biandamu ambazo huingia katika maji kutokana na shughuli mbalimbali za binadamu hivyo yakitumika huweza kuleta athari za kiafya kwa binadamu,” anasema Dkt. Machege.

Dkt. Machege anabainisha pia kuwa wakati mwingine maji huonekana safi na salama ilihali sio salama kwa matumizi  yanaweza kuwa na wadudu lakini pia kemikali ambazo sio rahisi muda mwingine kutambua hilo, hivyo anaitaka jamii kuwa makini kuhakikisha wanapata na kutumia maji safi na salama yanayofaa kwa matumizi ya binadamu.

Maradhi yanayowakumba watu wengi, hasa watoto kutokana na kunywa maji yasiyo salama ni pamoja na typhoid, kipindupindu, kuhara na polio. Dkt. Machege anawashauri wazazi, walezi na jamii kuhakikisha kila mmoja anahakikisha watoto wanapata na kutumia maji safi na salama ili kuwalinda watoto ambao ni taifa la kesho.

Kumekuwa na jitihada nyingi za kupambana na uchafuzi wa mazingira ambao huwa chanzo ya kutopata maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu lakini bado tuna safari ndefu ya kwenda kabla ya kufikia tunapopahitaji.

Tunahitaji mazingira safi kwa hewa tunayovuta, maji tunayokunywa na udongo tunaopandia chakula chetu. Wakati rasilimali hizi zinapochafuliwa ardhi yetu na maisha yetu yanakua hatarini muhimu ni kila mmoja kuhakikisha anayalinda mazingira ili yawe salama kwa watu wote