Duniani

Maisha Ndani ya Chumba Chenye Ukimya Zaidi Duniani

Na Daniel Filbert

Kila kukicha mwanadamu anaendelea kufanya mambo makubwa ambayo yanayoushangaza ulimwengu hasa katika suala la usanifu wa majengo. Yapo majengo ya kustaajabisha duniani ambayo ubunifu wake unaweza kukuachia mshangao, mfano jengo la Hagia Sophia lililopo Instabul Uturuki au Taj Mahal, jengo kubwa la kihistoria lililopo India, ambalo lilijengwa kwa amri ya mtalawa Shah Jahan miaka ya 1931 kama zawadi kwa mkewe kipenzi. Si hayo tu, bali kuna majengo mengi sana mpaka leo usanifu wake ni wa kusataajabisha.

Hivi karibuni jarida maarufu la The Guinness Book of Records, kitabu pekee kinachotunza kumbukumbu za mambo yanayostaajabisha ulimwenguni, kimeongeza orodha yake baada ya kuthibitisha kuwa chumba kimoja kilichomo ndani ya ofisi za Makao Makuu ya Microsoft, Washington ndicho chumba kinachoongoza kwa kuwa na hali ya ukimya na utulivu uliokithiri kuliko chumba chochote duniani.

Vyombo vya habari BBC na CNN vimeripoti kuwa kuwa ukiingia ndani ya chumba hiki kisha ukakaa kwa muda mrefu, basi utaanza kuyasikia mapigo ya moyo wako kupitia masikio yako bila hata ya msaada wa vifaa vya kitaalamu ambavyo madaktari hutumia. Vilevile utasikia hata msuguano wa mifupa ndani ya mwili wako pindi ukiwa unajongea ndani ya chumba hicho.

Katika ripoti iliyotolewa na mwanasayansi wa masuala ya sauti na matamshi, Hundraj Gopal, ambaye pia amehusika katika kukisanifu chumba hicho mpaka kukamilika kwake, aliandika, “muda mfupi tu baada ya mtu kuingia ndani ya chumba hiki basi ataanza kujisikia hali ya utofauti kabisa ikiambatana  na hisia za kipekee ambazo ni ngumu kuzielezea.”

Watu wengine wakiingia huanza kuhisi kama hakuna sauti kabisa, wengine huhisi masikio yao yameziba au wamekuwa viziwi, lakini pia kutokana na ukimya uliopo ndani ya chumba hiki waweza kuisikia sauti ya mifupa yako pindi unapokuwa unageuza shingo yako,” aliandika.

Mwanasayansi Gopal anaeleza kuwa tunapokuwa katika sehemu ya kawaida (duniani) masikio yetu huwa chini ya kiwango fulani cha sauti, kwa hivyo kila wakati kuna shinikizo la hewa kwenye ngoma za masikio yetu, lakini ndani ya chumba hiko shinikizo la hewa kwenye masikio yetu halipo kabisa, kwa sababu hakuna mrejesho wa sauti kutoka katika kuta zinazozunguka chumba hicho.

Nini kimesababisha ukimya huu?

Mwanasayansi Gopal anasema kuwa wakati wakiwa wanafanya usanifu wa chumba hicho waliamua kijengwe na malighafi ambazo zitakuwa na uwezo wa kuzuia sauti yoyote itokayo nje ya chumba hicho isiweze kuingia ndani, pia sauti iliyopo ndani iwe tulivu bila mjongeo wowote kitaalamu chumba hicho kinaitwa “anechoic chamber” yaani chumba ambacho hakiwezi kutengeneza mwangi wowote.

Upande wa juu wa chumba hicho sauti ni ya chini mno kiasi kwamba wanamahesabu wanasema inaweza kufikia desibeli sifuri ambayo maana yake ni sawa na hakuna sauti kabisa.

Upande wa chini wa chumba hicho hakuna sauti kabisa kitaalamu huitwa ‘vacuum space’, yaani sehemu iliyo tupu ama isiyo na sauti kabisa.

Na ili kufikia ukimya uliokithiri chumba hicho kimejengwa kwa muundo kama kitunguu huku kuta zake zikitenganisha vyema chumba hicho na vyumba vingine vya kawaida ndani ya jengo hilo.

Ukuta wa chumba hicho una matabaka sita yaliyojengwa kwa kutumia saruji pamoja na chuma, huku kuta hizo zikiwa zimeachanishwa moja badala ya nyingine ili kuzuia mrindimo wa sauti inayotoka nje kuingia ndani. Sakafu yake imejengwa kwa kioo na gridi za nyaya zinazowesha kusimamisha sauti ili kuzuia mwangwi usijitokeze.

Gopal anaendelea kwa kusema kuwa kiwango cha kelele kilichopimwa ndani ni desibali -20.3 Hii ikimaanisha kuwa kelele ilyoko ndani ya chumba ni desibali 20.3 chini ya kizingiti cha kusikia kwa mwanadamu.

“Usanifu wa chumba hicho pamoja na ujenzi wake umeweza kuchukua takribani mwaka mmoja na nusu mpaka kukamilika kwake” amethibitisha Gopal.

Chumba hiki kilipewa heshima ya kuwa chumba kilicho kimya zaidi duniani mwaka 2015 Baada ya kuandikwa kwenye ripoti iliyotolewa na kitabu cha The Guiness World Records, ambapo kabla ya hapo chumba ambacho kilikuwa kikishikiria rekodi hiyo ni Maabara ya Orfield iliyoko Minneapolis ikiwa na desibali -9.4, hivi  sasa inatumika kama kivutio cha watalii.


Daniel Filbert ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu

cha Tumaini Dar es salaam College TUDARCo

akichukua Shahada ya kwanza ya Sanaa

katika Mawasiliano ya Umma pia ni mwandishi

wa Hadithi na Makala mbalimbali za kijamii 

Mfuate katika mtandao wa Facebook @Daniel Talking