Habari

Magufuli Kuzikwa Chato Ijumaa, Machi 26

Mama Samia amechukua nafasi ya hayati Rais Magufuli kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Rais Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametangaza Machi 25, 2021 kama siku atakayozikwa hayati Rais John Pombe Magufuli huko wilayani Chato, mkoani Geita. Hata hivyo taarifa hiyo imebadilishwa kuwa Ijumaa Machi 26 kutokana na taarifa mpya iliyotolewa na Msemaji wa Serikali. Akihutubia taifa kwa mara ya kwanza baada ya kuapishwa kwake kuwa Rais wa sita wa Tanzania, Rais Samia amesema mwili wa hayati Magufuli utaagwa kitaifa katika mikoa minne ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Geita. (Ratiba hii pia ilibadilika na kuongeza Zanzibar)

 

Akitangaza ratiba ya kuaga mwili wa hayati Magufuli, Mama Samia amesema shughuli ya kuaga itafanyika Machi 20 na 21 jijini Dar es Salaam, Machi 22 jijini Dodoma, Machi 24 jijini Mwanza na Machi 25 Chato. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuungana katika kipindi hiki cha majonzi. (Baadae Zanzibar iliongezwa ambapo Wanzanzibari walipata nafasi ya kuaga mwili wa hayati Magufuli Machi 23)

 

Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli alifariki Machi 17, 2021 kutokana na tatizo la moyo. Mama Samia amechukua nafasi ya hayati Rais Magufuli kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.