Maendeleo Endelevu

Maendeleo Endelevu: Fahamu Mfumo wa Ufuatiliaji wa Miradi Katika Jamii Yako

Miradi na huduma mbalimbali hutekelezwa na kutolewa kwa faida ya wananchi. Kuna miradi kama ya miundombinu kama maji, zahanati, shule na miradi inayohusu utoaji wa elimu na uhamasishaji inayolenga kubadilisha tabia au kuwajengea uwezo wananchi katika maeneo mbalimbali kama uwajibikaji, matumizi mazuri ya vyoo, utunzaji wa mazingira, afya, mabadiliko ya tabia nchi nakadhalika.

Miradi hiyo pamoja na huduma hizo hutolewa na mashirika, serikali, asasi za kiraia, makanisa na wadau mbalimbali wa maendeleo katika jamii. Mwisho wa utekelezaji wa miradi hiyo wananchi katika jamii husika hukabidhiwa ili kuendelea kutumika au kuhudumia jamii husika. Hivyo, miradi yote katika jamii inabaki kuwa mali ya jamii mara tu inapokabidhiwa.

Ni jukumu la wananchi kupitia serikali ngazi ya kijiji, kata, wilaya kusimamia miradi hiyo moja kwa moja ili iendelee kuhudumia wananchi kwa muda mrefu zaidi. Swali la msingi, ni je, ni mfumo gani utumike kufuatilia na kushirikisha jamii katika utekelezaji na utunzaji wa miradi hiyo?

Picha: Integrity Action

Ni jukumu la kila mwanachi kufanya ufuatiliaji wa mradi wowote katika jamii yake. Ufuatiliaji ni pamoja na kufahamu umuhimu wa mradi huo katika jamii yako, kufahamu mnufaika wa moja kwa moja wa huduma inayotolewa, kupata taarifa zikiwemo gharama za utekelezaji wa mradi husika kupitia kwa viongozi wa eneo lako. Pia ufuatiliaji unaweza kuwa ni kushiriki katika utatuzi wa changamoto zinazohusu mradi huo. Kama mwananchi katika jamii una wajibu kufahamu mambo yote hayo ili kuwa katika nafasi nzuri ya kutunza mradi huo. Ufuatiliaji wa miradi sio jukumu la viongozi pekee.

Kuna mifumo mingi ya kufanya ufuatiliaji wa miradi katika jamii yako. Mfumo moja wapo ni wa ‘’Kujenga Jamii yenye Uadilifu’’ (Community Integrity Building Model). Mfumo huu unalenga kuongeza uwajibikaji na uwazi katika utekelezaji wa miradi. Pia, mfumo huu unawezesha makundi ya watu kama wanawake, vijana na watu wanaoishi na ulemavu kushiriki na kutoa maoni yao kuhusu miradi. Je, unatoa maoni kuhusu mradi wowote unapokuja kwenye jamii yako?

Mfumo huu wa ‘’Kujenga jamii yenye Uadilifu’’ una hatua 5 za kufuata ili kuanza utekelezaji katika jamii. Kila hatua ni muhimu sana na mfumo huu unaweza kutumika kwenye jamii kabla mradi haujafika ili jamii iwe imejiandaa tayari kuupokea au kutumika wakati mradi ukiwa unatekelezwa au mradi ukiwa hatua ya mwisho. Mfumo huu ni sehemu ya maisha ya kila siku ya mwananchi katika jamii yake.

1. Kushirikisha Jamii.

Hatua ya awali ni kushirikisha jamii kuhusu mradi husika uliopo au unaokuja ili wananchi wote wafahamu na kuwa tayari kufanya ufuatiliaji. Ushirikishaji wa wananchi katika jamii ni pamoja na makundi lengwa mfano, wanawake, vijana, wazee na watu wanaoishi na ulemavu.

Ni lazima jamii kupitia viongozi kushirikisha kila mwananchi kupitia mikutano ya hadhara, matangazo ya nyumba na nyumba kwa wadau wote wa maendeleo. Hii husaidia kuwajengea wananchi uaminifu na nguvu ya kuhoji na kushiriki kutatua changamoto zitakapojitokeza.

2. Wananchi kuwa wafuatiliaji.

Jamii itachagua wawakilishi wawili kama wafuatiliaji (community monitors). Kupitia viongozi wa mtaa au kijiji / kata ni lazima kusimamia uchaguzi wa wafuatiliaji hao, inashauriwa kupata vijana wenye umri kuanzia 18 -35. Pia, kwa watakaochaguliwa ni lazima kuwa na uelewa kuhusu namna ya kufanya ufuatiliaji na kutoa ripoti kwa wananchi hivyo ni lazima wafahamu kusoma na kuandika. Pia, ni lazima kuzingatia jinsia ya ME na KE.

3. Wafuatiliaji kutenda.

Wafuatiliaji lazima wawezeshwe. Hii ni pamoja na kufahamu taarifa zote kuhusu mradi wanaoufatilia. Watekelezaji wa miradi, uongozi wa sehemu husika wana wajibu wa kuweka wazi nyaraka mbalimbali zinazohusu miradi ikiwemo tarehe ya kuanza na kumaliza mradi, wanufaika wa moja kwa moja, bajeti itakayotumika, gharama ya vifaa (BBQs) n.k.

Wafuatiliaji hawa ni sehemu ya jamii hivyo ni lazima wafahamike na jamii nzima na kupewa ushirikiano wa moja kwa moja. Ufuatiliaji wao katika mradi itategemea na aina ya mradi uliopo katika eneo lao mfano kama kuna mradi wa miundombinu ya kisima, wafuatiliaji watahakikisha kisima kinatumika vizuri kama ilivyoelekezwa na uongozi. Wafuatiliaji watahakikisha hakuna matumizi mazuri na kama kuna uharibifu wowot, wafuatiliaji hao wanaripoti tatizo kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi kwa njia ya ushirikishwaji.

4. Matatizo yanatatuliwa.

Endapo kuna changamoto yeyote kuhusu mradi, wafuatiliaji wanaripoti kwenye Kikundi Kazi (Joint Working Group)’ Je, hiki kikundi ni nini haswa? Kikundi kazi ni kikundi cha wananchi katika jamii kitakachochaguliwa na wananchi wenyewe kama wawakilishi kupokea changamoto zinazoibuliwa na wafuatiliaji wa jamii.

Changamoto hizo zitahusu miradi iliyopo kwenye jamii au huduma zinazotolewa kwenye jamii. Kikundi kazi kitajumuisha wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo viongozi (mtendaji wa kijiji/ mtaa na mwenyekiti). Pia, kikundi kazi kitajumuisha wawakilishi wa makundi ya vijana, wanawake na watu wanaoishi na ulemavu. Kazi ya ‘’Kikundi kazi’’ ni kutoa mapendekezo kuhusu changamoto zinazoibuliwa na wafuatiliaji na kupeleka mrejesho kwa wananchi wote. 

Kikundi kazi sio sawa na kamati za maendeleo zilizopo kwenye serikali za mitaa/ vijiji lakini wajumbe wa kamati hizo wanaweza kuwa sehemu ya kikundi kazi kwa ajili ya kutoa mawazo yao pia na kushirikisha kamati husika kuhusu changamoto zilizojadiliwa. Hivyo, kikundi kazi kitasaidia kupata mawazo mbadala ya wananchi wenyewe na sauti zao kusikika katika maamuzi na maendeleo ya jamii yao moja kwa moja.

5. Sambaza Neno

Ni jambo jema kama mfumo huu ukiendelea kutumika katika maeneo mengi au mashirika mengi yanayoendelea kuleta miradi mingi katika jamii. Jamii inapenda kuona miradi iliyokabadhiwa inabaki kuwa endelevu kwa kizazi mpaka kizazi. Je, nini kifanyike?.

Ni lazima mfumo huu tuendelee kusambaza kwa jamii zingine kwa kuonesha mafanikio ya mfumo huu kwenye jamii zingine. Hata Serikali kupitia Halmashauri za Wilaya na idara mbalimbali ikiwemo idara ya maendeleo ya jamii inayosimamia miradi inaweza kutumia mfumo huu unaolenga kushirikisha jamii kwa ujumla katika utunzaji na ufuatiliaji wa miradi ili ibaki endelevu.

Shirika la Integrity Action linatoa mafunzo ya namna ya kutumia mfumo huu kwa wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuwawezesha wananchi kuendelea kuitunza miradi yao lakini pia kuwawezesha wananchi kutoa maoni yao na kushiriki ipasavyo katika kuleta maendeleo katika jamii zao. Hapa Tanzania, shirika la Raleigh Tanzania linatekeleza mradi wa SAY kwa kutumia mfumo huu.

Ili uendelee kujifunza zaidi, pakua Mwongozo wa ‘’Kujenga Jamii yenye Uadilifu’’ bure hapa. Pia unaweza kutazama video fupi hapa 


Makala hii imeandikwa na Peter Lazaro