Habari

Maandamano ya Kupinga Kukamatwa Bobi Wine Yaibuka Uganda, Watano Wafariki

Bobi Wine anayetokea Chama cha National Unity Platform (NUP) miaka ya karibuni amejizolea wafuasi lukuki kutokana na msimamo wake wa kumtaka Rais Museveni kung’atuka madarakani.

Maandamano yameibuka leo jijini Kampala nchini Uganda baada ya Jeshi la Polisi kumkamata mgombea Urais wa Upinzani, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Bwana Bobi Wine anagombea ili kumuundoa madarakani Rais Yoweri Kaguta Museveni aliyedumu madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu. Polisi wamemkamata kwa kile wanachodai ni kukiuka masharti ya Tume ya Uchaguzi.

Wafuasi wa Bobi Wine wamezuia baadhi ya barabara za Kampala na wengine wakichoma matairi wakitaka kiongozi wao huyo kuachiliwa. Hatua hii imepelekea Polisi kufyatua mabomu ya machozi na risasi za mpira ili kutawanya waandamanaji. Saa 9 mchana mwandishi wa kituo cha Televisheni cha NTV Uganda, Mujuni Raymond aliripoti vifo vilivyosababishwa na Polisi nchini humo vimefikia 5, 2 wakiwa wanawake na wanaume 3.

Maandamano yalianza baada ya Bobi Wine alipokamatwa katika mji wa Mashariki unaoitwa Luuka na kupelekwa katika kituo cha Polisi kwenye Jiji la Jinja.

Msemaji wa chama cha Mgombea Urais huyo, Joel Ssenyonyi amesema kuwa mpaka sasa hawajaruhusiwa wala hakuna sababu ya msingi waliyopewa ya kukamatwa kwa Bw. Wine.

Bobi Wine anayetokea Chama cha National Unity Platform (NUP) miaka ya karibuni amejizolea wafuasi lukuki kutokana na msimamo wake wa kumtaka Rais Museveni kung’atuka madarakani baada ya kukaa kwa miaka 36 tangu mwaka 1986 alipoingia kwa mtutu wa bunduki.

Robert Kyagulanyi, ‘Bobi Wine’ ambaye aliingia kwenye siasa mara ya kwanza mnamo 2017 kwa kugombea Ubunge wa Jimbo la Kyadondo Mashariki, alipoidhinishwa tu na Tume ya Uchaguzi kuwa mgombea Urais, Novemba 3, 2020 alikamatwa papo hapo na Polisi na kuachiwa baada ya muda mfupi.