Michezo

Kwanini Liverpool na Manchester United Zimependekeza Kufutwa kwa Ngao ya Jamii Uingereza?

Kufutwa kwa kombe la ligi na timu zinazoshiriki ligi kuu kubaki 18 ni kati ya mapendekezo yaliyomo kwenye mpango uitwao 'Project Big Picture'

'Project Big Picture' ni mpango mahususi wa kunusuru hali mbaya ya kifedha ambayo vilabu vingi vya soka vinaipitia nchini Uingereza kutokana na Janga la Corona. Mpango huu ambao ambao ulivuja na  habari yake kuchapishwa kwa mara ya kwanza kwenye tovuti ya Telegraph unapigiwa chapuo na klabu ya Manchester United na Liverpool.

Inaelezwa kwamba iliyovuja ni rasimu ya 18 ya mpango huo na itahitaji marekebisho mengi ili mpango huo uweze kukubalika na kuanza kufanyiwa kazi. Lakini mpango huo unahusu nini zaidi? Na kwanini umezua mjadala mkubwa baina ya vilabu na wadau wa mpira wa miguu nchini Uingereza?

Kujibu maswali hayo Serengeti Post tunaangazia mambo muhimu yaliyosisitizwa kwenye mpango wa 'Project Big Picture';

Asilimia 25% ya mapato ya ligi kuu uingereza (Premier League) kwa mwaka yatagawiwa kwa vilabu vyote vya soka nchini Uingereza pia kutakua na Pauni milioni 250 itakayogawiwa ili kuokoa hali mbaya ya uchumi iliyosababishwa na janga la Corona kutokana na kukosa mapato ya mlangoni baada ya mashabiki kuzuiliwa kuingia viwanjani.. Pia kutakua na nyongeza ya pauni milioni 100 kwa ajili ya Shirikisho la mpira wa miguu (FA).

Kuanzia msimu wa 2024-25 timu zitakazoshiriki ligi kuu Uingereza (Premier League) zitapungua kutoka klabu 20 hadi 18 huku katika ngazi ya 'Championship' na 'league one' na 'league two' kutakua na timu 24. Kupunguza idadi ya timu kutazipa nafasi klabu zinazoshiriki michuano ya ulaya (UEFA na EUROPA) kupata muda zaidi wa kujiandaa pia vilabu vitapata nafasi ya kucheza mechi za kujiandaa na ligi (Pre-season) huko Asia na Amerika Kaskazini.

Pendekezo jingine ni kwamba, idadi ya timu zitakazoshuka daraja itasalia ile ile (timu mbili) lakini timu itakayoshika nafasi ya 16 kwenye ligi kuu moja kwa moja itacheza michezo ya Play-off na timu zilizoshika nafasi ya 3 hadi ya 5 kwenye championship. Katika hili kuna uwezekano wa timu tatu kutoka ligi kuu zikashuka daraja.

Ngao ya jamii na kombe la ligi maarufu kama 'Carabao Cup' yatafutwa na kutakua na mechi za marudiano katika kombe la Shirikisho (FA Cup) ambazo pia hazitachezwa katika majira ya baridi. Pia kutaundwa kikundi kitakachosimamia ligi ya mpira wa miguu kwa wanawake ambayo haitakua chini ya usimamizi wa Shirikisho la soka na ligi kuu.

Licha ya Manchester United na Liverpool kuupigia chapuo mpango huo, jitihada zao hazikufua dafu na siku ya jumatano wiki hii mpango huo ulipingwa vikali katika mkutano wa dharura wa vilabu vinavyoshiriki ligi kuu Uingereza huku vikipendekeza kuwa na mpango madhubuti wa pamoja utakao kuwa na faida kwa vilabu vyote.

Mpango wa 'Project Big Picture' ungevipa vilabu 9 (Vilabu sita bora, Everton, West Ham na Southampton) nguvu ya kufanya maamuzi  juu ya vilabu vingine kadhalika pia vitapata nafasi ya kujiongezea mapato.

Taarifa iliyotolewa na ligi kuu Uingereza ilisema "Vilabu vyote 20 vya ligi kuu kwa pamoja vimekubaliana kutokuunga mkono mpango wa 'Project Big Picture'. Kadhalika wadau wa Ligi kuu wameazimia kufanya kazi kwa pamoja ili kuwa na mpango wa pamoja wa maswala ya fedha ili kuendeleza hali ya ushindani kwa vilabu vyote vinavyoshiriki ligi kuu".


Licha ya mpango huo kupigwa chini, Serengeti Post inaelewa kwamba mpango huo unaweza kupitiwa upya na kufanyiwa marekebisho ili uje uletwe tena mbele ya vilabu vyote.

Hakukuwa na nafasi yoyote ile ya mpango huo kuweza kukubaliwa tangu ulipovuja kutokana na mgawanyiko uliouleta kwa mashabiki, vilabu na wadau mbalimbali wa mpira wa miguu nchini Uingereza.