Duniani

Kutapika Wakati wa Ujauzito Huashiria IQ Kubwa kwa Mtoto

Watoto 121 ambao mama zao walikuwa wanapata homa za asubuhi na kutapika walichunguzwa ambapo walionekana kuwa na kiwango kikubwa cha IQ

Utafiti umebaini kuwa ikiwa unasumbuliwa na homa za mara kwa mara kipindi cha ujauzito, unaweza pata na mtoto mwenye IQ kubwa tofauti na watoto wengine wa rika lake

Kawaida, akina mama wengi huwa na wasiwasi kwamba homa hizo huharibu virutubisho ambavyo mtoto hupokea. Wana wasiwasi kuwa inaathiri ukuaji wa jumla wa mtoto.

Jambo la kushangaza ni kwamba, Watafiti katika Hospitali ya Watoto Wagonjwa huko Toronto, Canada, wamegundua kuwa badala ya homa hizo kumuathiri mtoto kwa njia mbaya, homa  na kutapika huongeza akili ya mtoto.

Kutapika wakati wa ujauzito ni ishara mtoto wako anaweza kuwa na IQ kubwa

Kwa utafiti, wanasayansi waliwachunguza watoto 121, watoto hawa walikuwa kati ya miaka mitatu hadi saba. Mama zao walipata homa za asubuhi na kutapika wakati wa ujauzito, iligundulika kuwa watoto hawa walikuwa na uwezo wa kupata alama za juu kwenye vipimo vya IQ, kumbukumbu na ustadi wa lugha.

Mtafiti kiongozi, Dk Irena Nulman, aliiambia Reuters Health kwamba matokeo hayo yanaonyesha kuwa kichefuchefu na kutapika wakati wa ujauzito sio hatari na kwa kweli kunaweza kukuza ukuaji mzuri wa akili wa watoto kwa muda mrefu.

Ingawa bado haijulikani sababu ya kichefuchefu na kutapika kwa wanawake wajawazito ni nini. Lakini ni kawaida sana kwa mama wanaotarajia, hasa miezi mitatu ya awali ya ujauzito. Imekuwa ikihusianishwa na homoni ambazo zinahusika na ukuaji wa mtoto.

Vidokezo vifuatavyo husaidia kushinda homa za asubuhi na kutapika wakati wa ujauzito.

 

Tangawizi

Tangawizi ni moja ya njia za kupambana na homa za asubuhi na kichefuchefu ukiachana na urahisi wake katika kuandaa. tangawizi huchemshwa katika maji au huchanganywa katika chai 

Kuwa na vitafunwa (Bytes) karibu

Hii ni muhimu sana kwa sababu wakati mwingine kichefuchefu kinaweza kuja wakati hauko nyumbani na kwa hivyo sio karibu na chakula. Hisia ya kichefuchefu ni mbaya kama tumbo halina kitu. 

Kujimwagia Maji Baridi

Kujimwagia maji baridi kichwani kunaweza epusha kuchefuchefu. Kwa hivyo ikiwa unahisi kutapika, jaribu kuoga na maji baridi. Sio lazima maji ya bomba la mvua ila hakikisha unajimwagia maji kichwani kwa njia yeyote ile.

Kula kidogo lakini mara nyingi zaidi kwa siku

Ni vizuri kula kidogo kidogo lakini mara kwa mara kuliko kula chakula kingi kwa milo mitatu kwa siku. Kula mara kwa mara husaidia kuongeza sukari mwilini sababu hali ya uchovu na homa huweza kusababishwa na kutokuwa na sukari ya kutosha kwenye damu. Sukari ndio chanzo cha nguvu mwilini. Chakula cha mara kwa mara humpa mama kiasi cha nguvu za kutosha kwake na kwa mtoto kwa muda wote.

Kula vyakula venye protini na vitamin B6

Vyakula venye protini kwa wingi na vile vyenye vitamin B6 humfanya mama apunguze hali ya kichefuchefu. Inashauriwa mama mjamzito aepuke kula vyakula venye viungo vingi, mafuta au vilivyokaangwa kwa muda mrefu sana. Vyakula hivi huweza kuzidisha hali ya kichefuchefu na kutapika balada ya kuiondoa.

Pata kifungua kinywa kabla ya kutoka kitandani

Mama mjamzito anashauriwa apate kifungua kinywa akiwa bado kitandani. Hali ya kuamka na tumboni hakuna kitu huweza kuwa chanzo cha kuhisi kichefuchefu na kutapika. Sasa ni vizuri ukapata kifungua kinywa ukiwa bado umepumzika. Kula mkate mkavu, cereals kavu au kitafunwa chochote. 

Tumia limao au ndimu

Limao au ndimu vina uchachu ambao husaidia kukata hali ya kichefuchefu. Kata limao na nusa, harufu ya limao itasaidia kupunguza hii hali ya kutapika. Pia unaweza ukakamulia limao kwenye chai au maji ukanywa. Unaweza pia kunusa maganda au majani ya limao maana husaidia pia kupunguza hali ya kichefuchefu.

Pumzika muda mrefu inavyowezekana

Haijalishi unabanwa kiasi gani na shughuli za kila si, lakini inapopatikana nafasi ya kupumzika ni vizuri mama apumzike. Uchovu unaweza kusababisha mama kuzidi kujisikia vibaya na hali ya kuumwa ikawa palepale.

Kunywa maji mengi

Kunywa maji mara kwa mara ili kuzuia mwili kuishiwa na maji (dehydradtion). Ni vizuri kunywa lita 2.5 kwa siku ikiwa pamoja na maji, chai au juice za matunda zisizo na sukari ya kuongeza au kemikali za viwandani.

Kunywa pregnancy multivitamin

Wakati mwengine ni vizuri kumuona daktari ili kupata maelekezo ya dawa ambazo ni salama kuzitumia kupunguza hali ya kutapika. Pia kama kuna uwezekano wa kupata dawa zinazoweza kurudisha virutubisho muhimu mwilini, ikiwa ni pamoja na folic acid na vitamin D. Kumbuka kupata ushauri wa daktari kabla ya kutumia.

Preggie pops

Hizi ni pipi ambazo hushauriwa kwa wajawazito. Hazina madhara yoyote kwenye ujauzito lakini ni vizuri pia kupata ushauri wa daktari kabla ya kutumia. Pipi hizi humsaidia mama kupunguza kichefu chefu na hazina madawa. Zinapatikana kwenye ladha mbalimbali.

Mazoezi

Mazoezi husaidia kupambana na homa za asubuhi na hisia hiyo ya kutaka kutapika. Tumia muda wa asubuhi au jioni kutembea nje ili kupata hewa kidogo.

Ni hakika kuwa kutapika wakati wa ujauzito hakutamdhuru mtoto wako kimwili lakini shida ni kuvimba kwa misuli ya tumbo. Lakini ikiwa kutapika kunaendelea kwa muda mrefu unashauriwa kumuona daktari.