Habari

Kuelekea Msimu wa Sikukuu za Mwisho wa Mwaka, Bei ya Petroli Yapungua Dar es Salaam

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei elekezi za bidhaa za mafuta ya petroli. Bei hizi zitaanza kutumika kuanzia Jumatano, Disemba 2, 2020

Ikiwa ni kuelekea mwisho wa mwaka, watumiaji wa vyombo vya moto jijini Dar es Salaam wanaelekea kumaliza mwaka na kuingia kwenye sherehe za Noeli na kufunga mwaka huku wakishuhudia punguzo la bei ya mafuta.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei elekezi za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini. Bei hizi zitaanza kutumika kuanzia Jumatano, Disemba 2, 2020.

Bei za rejareja na jumla za mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa yaliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimebadilika ikilinganishwa na bei zilizotangazwa Novemba 4, 2020.

Kwa mwezi Desemba 2020, bei za rejareja za Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimepungua kwa Shilingi 37/lita (sawa na asilimia 1.97) na Shilingi 47/lita (sawa na asilimia 2.71) na Shilingi 86/lita (sawa na asilimia 5.05).

Vilevile, ikilinganishwa na bei za mwezi uliopita, bei za jumla za Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimepungua kwa shilingi 37.36/lita (sawa na asilimia 2.11), shilingi 46.81/lita (sawa na asilimia 2.92) na shilingi 86.02/lita (sawa na asilimia 5.44).

Punguzo hili litafanya watumiaji wa vyombo vya moto wa jiji la Dar es Salaam kununua Petroli kwa Sh 1,865 kwa lita, Dizeli kwa Sh 1,687 na Mafuta ya Taa kwa Sh 1,621.

 

Bei Mikoa Kaskazini

Kwa mwezi Desemba 2020, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya Petroli na Dizeli kwa Mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara) zimebadilika ikilinganishwa na bei zilizotolewa Novemba 4, 2020. Bei za rejareja za Petroli na Dizeli zimepungua kwa shilingi 107/lita (sawa na asilimia 5.60) na shilingi 27/lita (sawa na asilimia 1.59).

Vilevile, ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei ya jumla ya Petroli na Dizeli imepungua kwa shilingi 106.40/lita (sawa na asilimia 5.99) na shilingi 27.28/lita (sawa na asilimia 1.71)

Hata hivyo, bei za Mafuta ya Taa hazina mabadiliko na zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la Novemba 4, 2020. Hii ni kwa sababu, kwa mwezi Novemba 2020 hakuna shehena ya Mafuta ya Taa iliyopokelewa kupitia bandari ya Tanga.

Bei Mikoa ya Kusini

Kwa mwezi Desemba 2020, bei za rejareja na jumla kwa bidhaa za mafuta ya Petroli na Dizeli kwa Mikoa ya Kusini (Mtwara, Lindi, and Ruvuma) zimebadilika ikilinganishwa na bei zilizotolewa tarehe 4 Novemba 2020.

Bei za rejareja za Petroli na Dizeli zimepungua kwa shilingi 70/lita (sawa na asilimia 3.65) na Shilingi 4/lita (sawa na asilimia 0.25), mtawalia.

Vilevile, ikilinganishwa na bei za mwezi uliopita, bei za jumla za Petroli na Dizeli zimepungua kwa shilingi 69.38/lita (sawa na asilimia 3.91) na Shilingi 4.32/lita (sawa na asilimia 0.27).

Mabadiliko haya ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji (BPS Premium).

 

Kampuni za Mafuta zaonywa

EWURA imesema kuwa kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei elekezi (price cap) kama ilivyokokotolewa na kanuni (formula) iliyopitishwa na EWURA na ambayo ilichapishwa katika Gazeti la Serikali Na. 656 la tarehe 21 Agosti 2020.

EWURA imesisitiza vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika.

Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani.

Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja. Adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika.

Lazima kutoa Risiti

Pia EWURA imesisitiza wauzaji wa mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa risiti za mauzo kutoka kwenye mashine za EFPP (Electronic Fiscal Pump Printers) na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita. Stakabadhi hizo za malipo zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya aidha kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora kinachofaa, na pia, risiti hizo zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya mafuta ya petroli.