Tanzania

Kolabo 10 za Bongo Fleva Zilizotikisa 2020

Ngoma hizi ni zile ambazo zilitikisa anga la muziki kabla, wakati na hata baada ya Covid-19

Twenti twenti mwaka uliojawa na mambo mengi ya kufurahisha na kuhuzunisha. Mwaka wa Uchaguzi Mkuu Tanzania, mwaka uliogubikwa na mlipuko wa Covid-19 na kusababisha mtindo wa maisha kubadilika kuendana na utamaduni mpya ikiwemo kufanya kazi kutoka nyumbani na kuepuka mikusanyiko.

Kwa upande wa burudani mambo pia yalibadilika, kwa kipindi ambacho Covid-19 ilishamiri hakukuwa na matamasha ya ana kwa ana kama ilivyozoeleka kwani watu walijifungia ndani wakihofia uhai wao. Wadau wa sanaa walibuni njia za kibunifu kama wasaniii kufanya matamasha kupitia mitandao kuhakikisha burudani ya muziki inawafikia watu wakiwa majumbani na hata karantini. Wakati wasanii wakipoteza fursa ya kuwatumbuiza mashabiki katika majukwaa ya ana kwa ana, hasira yao ilihamia studio kwa kuandaa maudhui mbalimbali na kuwafikia wapenda muziki kupitia majukwaa mbalimbali ya muziki ya kimtandao.

Kupitia makala hii, Wizara ya Burudani hapa Serengeti Post inakuletea ngoma kali ambazo wasanii walishirikiana katika kuonesha ufundi wa kutunga na kuimba. Ngoma hizi ni zile ambazo zilitikisa anga la muziki kabla, wakati na hata baada ya Covid-19. Orodha hii iko kwa mpangilio wa kuanzaia namba10 hadi namba moja.

Tumekuwekea hapa kolabo hizi 10 na maelezo mafupi ya kila kolabo ili kufahamu maudhui ya nyimbo husika na namna ambayo nyimbo hizo zilipokelewa na wapenzi wa muziki:

Namba 10: Ibraah Ft. Harmonize - One Night Stand


Kutoka Konde Gang, Ibraah ni moja ya chipukizi aliyeibuka na kufanya vizuri katika soko la muziki wa Bongo kwa mwaka 2020. Ibraah aliachia EP yake lakini nyimbo yake iliyoibuka kupendwa zaidi na kusikilizwa zaidi ni hii ya One Night Stand aliyomshirikisha kiongozi wake – Harmonize.

One Night Stand kwa vijana wa mjini inamaanisha hakuna kugandana katika mahusiano hasa kwa sababu kama mauongo yaliyoko kwenye mahusiano mengi. Ibraah ameimba kwa ukomavu akisindikizwa na Harmonize ambaye tayari ni msanii mkubwa katika tasnia. Utenzi, melodi na mdundo vyote vinatoa kibali kwa wimbo huu kuingia katika orodha ya kolabo 10 za 2020.

Namba 9: Nandy Ft. Harmonize – Acha Lizame


Nandi ni moja ya wanamuziki wa kike walioutendea haki mwaka 2020, mashabiki wengi wa Nandi ni wenye furaha kwani amewafanya kuwa bize wakiburudika. Nandi ameachia kolabo kadhaa na katika hii aliwachota mashabiki wa Harmonize kwa kuwachombeza kwa utenzi wa Acha Lizame.

Wimbo huu ulipokelewa vizuri na mashabiki; mdundo, utenzi na melodi yake vimekubalika kwa walaji wa muziki wa Bongo. Wizara ya Muziki ya Serengeti Post imeipitisha hii kukamatia nambari tisa katika orodha ya kolabo kali za 2020.

Namba 8: Zuchu Ft. Diamond Platnumz – Litawachoma


Zuchu ni mwanamuziki aliyeupania mwaka 2020. Amefanya kazi nyingi za kutosha kuonesha uwezo na kipaji chake, walaji wengi wa muziki wanamtabiria kuwa mwanamuziki mkubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Zuchu amefanya kolabo mbili na bosi wake Diamond Platnumz na kolabo zote zimepokelewa vizuri na mashabiki wa muziki. Litawachoma ni moja ya kolabo hizo na tumeipa nafasi ya kuingia katika orodha ya kolabo 10 zilizofanya vizuri mwaka 2020. Litawachoma ni utenzi wa mapenzi ambao wapenzi wanaeleza hisia nyingi za upendo na kujaribu kujihami na watu wenye nia mbaya ya kuharibu penzi lao.  

Namba 7: Rayvanny Ft. Zuchu – Number One


Rayvanny ni mwakilishi mwingine wa lebo inayofanya vizuri nchini Tanzania, WCB, ambaye tunaweza kusema muziki wake umetamba kuliko jina lake. Imekuwa ni kawaida kwa Rayvanny kufanya vizuri zaidi pale anapowashirikisha wasanii wengine kwenye kazi zake na katika wimbo huu Namba One amemshirikisha Zuchu.

Namba One ni wimbo wa kusifu na kueleza hisia za upendo kwa mpenzi, Rayvanny na Zuchu wanashea hisia zao za mapenzi dhidi yao, kila mmoja akimwita mwingine Namba One na kuonesha jinsi anavyomthamini mwenzie. Utenzi na melodi vimetosha kuwakuna mashabiki na kupitiliza hadi katika spika za Wizara ya Burudani hapa Serengeti Post.

Namba 6: Nandy Ft. Ali Kiba – Nibakishie


Nibakishie ni utenzi wa Nandy akimshirikisha nguli wa Bongo Fleva, Ali Kiba, utenzi huu wa mapenzi unaeleza hisia za wapenzi wawili waliokolea penzini kiasi cha kutamani kumega penzi kidogo kidogo na kubakisha ili ladha isiishe mapema. Nibakishie ni moja ya kolabo iliyopata mapokezi makubwa hasa kwa vijana ambao wamekuwa wateja wakubwa wa muziki wa kizazi kipya. Kwa waliobahatika kusikiliza wimbo huo na kutazama vidio yake wamepiga kura ya ‘ndio’ na kuifanya kolabo hii kuwa moja ya kolabo kubwa 10 kwa mwaka 2020.

Namba 5: Rayvanny ft Messias Maricoa – Teamo


Nabii kutoka falme za WCB, Rayvanny amejinyakulia nafasi nyingine kama mmoja ya wasanii waliofanya kolabo kali kwa mwaka 2020. Teamo ambayo amemshirikisha mwanamuziki kutoka Msumbiji Messias Maricoa ni moja ya wimbo uliopendwa na wapenzi wa muziki wa Bongo Fleva na nje ya Bongo.

Teamo ni neno la kihispaniola linalomaanisha Nakupenda, ni utenzi wa mapenzi ambapo Rayvanny anaelezea hisia zake kwa mpenziwe. Utenzi na melodi nzuri vimetosha kuwachanganya mashabiki wa muziki na Wizara ya Burudani hapa Serengeti Post kuridhia kuiweka nambari tano kwenye orodha ya kolabo kali.

Namba 4: Zuchu Ft. Diamond Platnumz – Cheche


Moto wa Zuchu tangu azindue EP yake chini ya lebo ya WCB umekuwa mkali na unatoa cheche ambazo zinawashtua wanamuziki wa kike katika tasnia ya muziki wa Bongo. Zuchu amekuwa na mwaka bora zaidi wa maisha yake katika mwaka wake wa kwanza wa utambulisho. Zuchu amepokelewa vizuri kufuatia uwezo wake wa kutunga na kuimba melodi zenye mvuto kwenye masikio ya wengi.

Cheche ni moja ya kolabo nyingi alizofanya Zuchu kwa mwaka 2020. Akiwa amemshirikisha kiongozi wake Diamond Platnumz, Zuchu na Diamond wameonesha uwezo wa kutosha kuonesha namna ambavyo penzi baina ya wawili wapendanao linaweza kunoga mpaka kutoa cheche.

Namba 3: Darasa Ft. Sho Madjoz – I like It


Darasa ameweza kupenya katika orodha ngumu ya kolabo zilizoachiwa 2020 kupitia ngoma yake ya ‘I Like It’ aliyomshirikisha mwanadada kutoka Afrika Kusini, Sho Madjoz. Wimbo huu ulipata mapokezi makubwa hasa kwa utenzi na namna ambavyo Darasa alimshawishi Sho Madjoz kwa kumsifia na kuonesha hisia za mapenzi ya kweli. Darasa amekuwa mkali wa kutengeneza rap zinazokubalika na kuchezeka lakini katika hii umachachari wa Sho Madjoz ulizidisha ladha na kujikuta ngoma ya ‘I Like It’ inatamba katika chati mbali mbali za muziki.

Namba 2: Diamond Platnumz Ft. Kofi Olomide - Waah


Diamond Platnumz ameendelea kuvunja rekodi zake mwenyewe. Kutoka Yope Rmx mpaka Waah ambapo amemshirikisha gwiji wa muziki wa Bolingo barani Afrika, bosi ya mboka – Koffi Olomide. Waah inaweza kuwa funga mwaka kwa 2020, si wengi walitarajia Diamond kufanya kazi na Koffi Olomide na hata baada ya wawili hao kutangaza kufanya kazi mashabiki walishakuwa na matarajio makubwa ambayo yalijibiwa kupitia Waah.

Waah haijatamba kwa utunzi bali kwa mdundo mkali na ustadi wa kuimba na kucheza uliioneshwa na ‘Mopao’ – Koffi Olomide pamoja na jenerali ‘Dangote’ – Diamond Platnumz.

Namba 1: Roma Ft. Stamina (Rostam) – Kaka Tuchati


Roma na Stamina ambao kwa pamoja wanajiita Rostam ni wakali wa michano ambao wamefanikiwa kujitengenezea sehemu ya pekee katika mbingu ya muziki wa Bongo. Wawili hawa ni wakali wa kutumia tamathali za usemi katika kufikisha ujumbe uwe ni wa mapenzi, mambo ya kijamii au hata mambo magumu ya kisiasa.

Kaka Tuchati ni utenzi uliotungwa wakati Tanzania na Dunia ikiwa katika mkwamo wa mlipuko wa Corona. Kupitia wimbo wa Kaka Tuchati, Rostam waliweza kuelimisha jamii namna ya kukabiliana na janga la Covid-19 huku wakizikumbusha mamlaka umuhimu wa kuchukua hatua thabiti katika kukabiliana na corona.

Wizara ya Burudani ya Serengeti Post tunakukaribisha kufurahia kolabo hizi za kukumbukwa kwa mwaka 2020 na ukiwa na maoni basi usisite kutuchatisha kupitia mitandao yetu ya kijamii.