Habari

Kauli za Umoja wa Ulaya, Marekani, Canada zamuibua Kabudi, Asema Tanzania ni Taifa Huru

"Tutafanya kazi na nchi zote ambazo zinatuheshimu, zinatutambua kama Taifa huru, kutuheshimu sisi kama binadamu wa mataifa mengine, hatutakubali kudharauliwa, kutokuheshimiwa utu wetu na kudharauliwa kwa sababu ya misaada au pesa’, amesema Prof. Kabudi


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amesema Tanzania itashirikiana na nchi yoyote duniani ambayo inatambua na kuheshimu Uhuru wa nchi na utu wa watu wake. 

 

Prof. Kabudi ametoa kauli hiyo jijini Dodoma alipozungumza na Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na taasisi zake tangu alipoteuliwa na Rais Magufuli kuwa Waziri wa Mambo ya Nje. 

 

"Tutafanya kazi na nchi zote ambazo zinatuheshimu, zinatutambua kama Taifa huru, kutuheshimu sisi kama binadamu wa mataifa mengine, hatutakubali kudharauliwa, kutokuheshimiwa utu wetu na kudharauliwa kwa sababu ya misaada au pesa’, amesema Prof. Kabudi 

 

Ameongeza kuwa Tanzania itasikiliza taifa lolote duniani na kujadiliana nalo kwa heshima kwani mapungufu hayapo upande mmoja tu. 

 

"Tuko tayari kuwasikiliza na kujadiliana nao kwa heshima na kama wanadhani kuna kitu kimepungua kwetu na sisi tunadhani kimepungua kwao," amesema Prof. Kabudi. 

 

Amesema Tanzania haiwezi kumruhusu mtu yeyote atumie misaada ya fedha kuondoa uhuru wetu na kutokuthamini utu wetu. 

 

Amesema Tanzania haiwezi kujitenga kama kisiwa na itaendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za kidunia kama vile kulinda amani, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kutunza mazingira. 

 

"Hatutajitenga katika dunia hii, tutaendelea kujumuika katika kazi mbalimbali kama vile ulinzi wa amani, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuhifadhi mazingira,’ alisema na kuongeza kuwa tumekuwa bandari ya amani kwa wakimbizi sio tu kutoka Afrika bali duniani kote na tutaendelea kuwa hivyo," Ameongeza Prof. Kabudi. 

 

Amesema jukumu la kuieleza dunia kuhusu takwimu za vitu mbalimbali ni la watumishi wa Mambo ya Nje na hawana budi kuhakikisha wanaliekeleza hilo kwa ufasaha. 


Mnamo Novemba 20, 2020, Wizara ya Mambo ya Nje ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari iliyokuwa na kichwa cha habari kilichosomeka, “Bunge la Umoja wa Ulaya Halijaiwekea Tanzania Vikwazo vya Kiuchumi na Haijaifutia Misaada, Mikopo”. Taarifa hiyo ilikuwa inakanusha uvumi ulioenea mitandaoni uliokuwa ukisema Umoja wa Ulaya umeiwekea Tanzania vikwazo vya kiuchumi pamoja na kuizuia kufanya biashara na nchi yoyote ya Ulaya.

 

Pia uvumi huo ulieleza kuwa Bunge la Umoja wa Ulaya limeazimia kuifutia Tanzania misaada na mikopo yote ambayo imeomba kwenye umoja huo na mashirika yake. Wizara ilikanusha vikali taarifa zote hizo kwa kusema iliyokutana Novemba 19, 2020 ni Kamati ya Bunge na sio Bunge la Umoja wa Ulaya na hakikutoa azimio lolote zaidi ya kutoa fursa kwa wajumbe wasiozidi 8 kutoa maoni kati ya wajumbe 71 wa Kamati hiyo.

 

Katika kikao cha Kamati baadhi ya Wabunge wa Umoja huo walikemea vitendo vinavyoendelea nchini Tanzania vya Ukiukwaji wa Haki za Binadamu na Misingi ya Demokrasia. Wabunge hao walitolea mfano kushikiliwa magerezani kwa baadhi ya viongozi na wafuasi wa Vyama vya Upinzani, ambao baadhi wanakabiliwa na mashtaka ambayo hayana dhamana.

 

Pia Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge hilo inayohusika na Mahusiano ya Kimataifa, David McAllister alitaka maelezo kuhusu Tanzania kupewa Euro milioni 27 takribani shilingi bilioni 74 ili kupambana na madhara ya janga la corona, Bw. McAllister alihoji kwa nini Tanzania ilipewa fedha hizo wakati tayari ilishatangaza kuwa hakuna corona baada sala za kitaifa za siku tatu. Kwa lugha ya ukali Mwenyekiti huyo alitaka maelezo ya kina kwanini fedha ambazo ni za walipa kodi wa Bara la Ulaya zimepelekwa kwa nchi ambayo tayari imesema haina maambukizi ya virusi vya corona na inakiuka maelekezo ya Shirika la Afya Duniani, WHO.

 

Hata hivyo Bunge la Umoja wa Ulaya sio la kwanza kutoa kauli za kukemea hali ya kidemokrasia hapa nchini. Marekani kwa kupitia Mabunge ya Kongresi na Seneti wameshanukuliwa mara kadhaa kupitia Kamati zake walitoa kauli za kukemea mambo mbalimbali yanayoendelea nchini.

 

Kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu baadhi ya Mabalozi wa nchi za Ulaya, Marekani, Japan na Canada walikuwa wakitoa kauli mbalimbali kukemea baadhi ya matukio yaliyokuwa yakiendelea kipindi cha kampeni hata kwenye zoezi la upigaji wa kura.

 

Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald J. Wright alikaririwa mara kadhaa akitoa kauli za kukemea ukiukwaji wa demokrasia kipindi cha uchaguzi. Mara nyingi alitumia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kukemea mambo mbalimbali ambayo aliona ni ukiukwaji wa demokrasia na misingi yake kipindi cha uchaguzi.

 

Pia baada ya Uchaguzi viongozi wa Upinzani walipokamatwa alituma ujumbe kwa njia ya Twitter akitaka waachiwe na pia aliongelea suala la kukosekana kwa intaneti.

 


Novemba 2, 2020 baada ya zoezi la Uchaguzi Mkuu Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Sweden aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter, akiongelea masuala ya idadi ndogo ya waangalizi wa uchaguzi, kukamatwa kwa viongozi wa upinzani baada ya uchaguzi mkuu kuwa ni kukiuka misingi ya demokrasia.


 

Pia Novemba 2 Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo aliandika pia kupitia ukurasa wake wa Twitter, akisema anasikitishwa na taarifa za kuwepo na mapungufu katika uchaguzi mkuu na kukamatwa kwa wanasiasa na kutokea kwa matukio ya fujo baada ya uchaguzi mkuu na aliongeza kuwa watafuatilia tuhuma za matumizi ya nguvu dhidi ya raia.