Maendeleo Endelevu

Kampeni ya Uwajibikaji wa Jamii Kupitia Vijana yawanufaisha watu wanaoishi na Ulemavu Dodoma, Morogoro na Iringa.

Shirika la Raleigh Tanzania kupitia kampeni ya Uwajibikaji wa Jamii Kupitia Vijana yenye kauli mbiu #Nawajibika yaendelea kuwafikia wananchi katika mkoa wa Dodoma, Morogoro na Iringa. Kampeni hii yenye lengo la kuhamasisha wanachi hasa wanawake, vijana na watu waishio na Ulemavu kushiriki katika maendeleo ya jamii zao kwa kufuatilia miradi iliyopo na kupata taarifa mbalimbali, Pia, kupitia kampeni hii wananchi wanapata uwezo wa kutatua changamoto zinazohusu miradi kwa kuishirikisha jamii nzima kupitia vikundi kazi ambavyo vinaundwa kwa kujumuisha watu wenye uzoefu mbalimbali katika jamii hiyo watakochaguliwa na wanajamii wenyewe.

Ndugu Peter Lazaro, Afisa Mawasiliano na Kampeni ya Uwajibikaji wa Jamii Kupitia Vijana alisema, ‘’vijana ni nguvu ya taifa hili hivo wanapaswa kupewa nafasi kubwa katika kufanya maamuzi na kushiriki katika utatuzi wa changamoto mbalimbali pasipo kusubiri uongozi wa jamii yao kwa sababu wao pia ni sehemu kubwa ya jamii hiyo, hii itasaidia kila mwananchi katika jamii yake kuwajibika ipasavyo na kuwa na uhuru na nguvu ya kuwaajibisha wenye mamlaka katika jamii hizo,’’

Tulizungumza na wananchi wa Wilaya ya Chamwino, Kijiji cha Miganga ambapo kampeni hii imefika moja kwa moja, Ndugu Mussa, ambaye ni mzaliwa wa Kijiji hicho cha Miganga alisema kuwa yeye hajawahi kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto zozote na hajawahi kuwakilisha kundi lolote katika jamii yake. Mussa anaishi na ulemavu wa macho (kipofu)hivyo anasema aliona hana uwezo wa kushiriki katika maendeleo kwa sababu ana changamoto ya kutoona lakini baada ya kupewa ya kampeni hii kufika katika Kijiji cha Miganga na kupewa mafunzo ya namna ya kushiriki katika maendeleo licha ya kuishi na Ulemavu wa aina yake, Mussa sasa ni sehemu ya Kikundi Kazi katika jamii yake na anawakilisha kundi kubwa la watu wanaoishi na Ulemavu katika Kijiji chake, Hali hii imempa furaha kubwa sana Mussa kwa sababu hapo mwanzo aliona kuwa hana uwezo wa kusikilizwa na kuheshimika.

Mussa alisema, ‘’ Sasa naweza kuzungumza yale yanayonihusu na yanayohusu jamii yangu kupitia kikundi kazi hiki, napenda kulishukuru shirika la Raleigh Tanzania kwa kuja na Kampeni hii na Kauli Mbiu #Nawajibika ambayo imewalenga mpaka watu kama sisi tunaoishi na Ulemavu. Kwa sasa sauti zetu zitasikilizwa na kupewa vipaumbele.’’

 

         Mratibu wa Kampeni ya Uwajibika Kupitia VIjana akitoa mafunzo kwa wananchi wa Kilosa

Shirika la Raleigh Tanzania kupitia kampeni hii imeandaa muongozo utakaomwezesha mwananchi kujifunza namna ya kufanya ufuatiliaji na kuishirikisha jamii hasa makundi maalumu hasa vijana, wanawake na watu wanaoishi na Ulemavu. Kampeni hii inatumia muongozo huu kufikia wananchi wengi zaidi ili wajifunze dhana ya Uwajibikaji na Ushirikishwaji kwa kutumia Mfumo wa Kujenga Jamii yenye Uadilifu yaani Community Integrity Building ulioandaliwa na washirika na wadau wa Maendeleo Integrity Action

Wadau  wa Maendeleo yakiwemo mashirika mbalimbali yanayotekeleza miradi ya miundombinu Pamoja na huduma mbalimbali katika jamii yanaombwa kutumia mfumo huu wa Kujenga Jamii yenye Uadilifu ili miradi hiyo iendelee kubaki endelevu na kusaidia wananchi kwa muda mrefu zaidi. Ili uwe sehemu ya kampeni hii tafadhali pakua mwongozo na kujifunza bure kabisa kwenye tovuti ya Raleigh Tanzania [www.raleightanzania.org] au bofya hapa moja kwa moja [mwongozo wa kujenga jamii yenye uadilifu]. Pia unaweza kusirika kwa njia ya mitandao ya kijamii kwa kujiunga Group la Facebook ili kuona maendeleo ya kampeni hii. Shiriki sasa #Nawajibika.