Afya

Jinsi magonjwa ya Kitropiki Yaliyosahaulika Yanavyoigharimu Jamii

Nchini Tanzania watu milioni 16 tayari wanapokea matibabu ya magonjwa ya kichocho, trakoma, matende, na upofu unasababishwa na wadudu wa kwenye mito, bado watu milioni 9 kiujumla wanahitaji dawa na matibabu.

Na Ahmada Yahaya

Magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika (Neglected Tropical Diseases au NTDs) ni magonjwa yanayosababishwa na bakteria na vimilea ambukizi ambavyo hupatikana katika nchi 149 ambazo huhesabika kutokana na hali yao ya anga kama nchi za kitropiki (zenye joto) kabisa au wastani. Magonjwa haya yanaleta athari hatarishi na mhangaiko, na husababisha matatizo kama upofu au matatizo ya tumbo. Magonjwa yaliyosahaulika ya kitropiki husababisha vifo zaidi ya 170,000 kwa mwaka, na watu zaidi ya bilioni huhitaji matibabu ya magonjwa haya. 

Magonjwa ya kitropiki mara nyingi husababishwa na ukosefu wa usafi wa mazingira na upatikanaji wa maji safi  makaazi, na chakula. Hali hii inasababishwa na ukosefu wa maendeleo na umasikini ambao, aghalabu ulisababishwa na misingi ya ukoloni. Nchi nyingi zinazoathiriwa na magonjwa ya kitropiki barani Afrika zina historia za ukoloni, unyonyaji na uporaji wa rasilimali nyingi zilizojenga nchi na maendeleo ya Ulaya. Hali hii imeleta athari za muda mrefu zinazotatiza njia ambazo serikali za Kiafrika zinaweza kujenga miundombinu ya afya kwa umma na usafi tangu zipate uhuru.

Kuna magonjwa matano makuu ya kitropiki yaliyoshaulika ambayo yanaathiri ulimwengu sana. Magonjwa hayo ni:

1.   Minyoo tumboni (intestinal worms)

Huu ndio ugonjwa wa kitropiki uliosahaulika lakini wenye athari kubwa zaidi kuliko mengine ulimwenguni kote, na zaidi ya waathirika bilioni 1.7 wanahitaji matibabu. Minyoo ya tumboni mara nyingi huenezwa kupitia kwa vyakula au vinywaji vichafu. Minyoo huishi na kuhamishwa kupitia udongo na kinyesi cha binadamu, kwa hivyo wakati maji safi hayapatikani kuna hatari kubwa ya maambukizo na ueneaji.

Minyoo husababisha uharibifu kwa kutaga mayai ndani ya miili yetu, ambayo inaweza kusababisha maumivu mwilini au kutokwa damu kwenye njia za kupitisha chakula tumboni. Kutokwa na damu tumboni basi husababisha upungufu wa damu (anaemia), utapiamlo, uvimbe wa tumbo, upotezaji uzito wa kimwili, kuhara, na mengine mengi.

2.  Kichocho (Schistosomiasis)

Ugonjwa wa kichocho (Schistosomiasis) au Bilharzia ni ugonjwa wa kitropiki wa pili kwa kuwa na madhara zaidi,  na unaambukizwa kwa kugusana na maji ambayo yameambukizwa na vimelea ambavyo huishi kwenye konokono ambao huishi katika maji, kwa mfano mito na mifereji; vimelea hivi hupenya katika ngozi na kuingia mwilini. Ingawa ni ugonjwa wa kitropiki uliosahaulika na wa pili unaojulikana zaidi, ndio ugonjwa unayosababisha vifo vingi zaidi na zaidi ya waathirika milioni 228 ulimwenguni kote  wanahitaji matibabu

3.   Matende (Lymphatic Filariasis)

 Ugonjwa wa Matende ni ugonjwa wa kitropiki ambao unaweza ukawa hauna dalili zinazoonekana, daili kidogo tu, na dalili sugu katika mwili. Ugonjwa huu wa matende mara nyingi huitwa ‘elephantiasis’ na hutambulika sana kutokana na athari zake kwenye mwili.

Ugonjwa wa Matende unaweza kusababisha uvimbe mkali katika viungo vya mwili, kama mikono na miguu, ambao husababisha usumbufu mkali na ulemavu. Maambukizi ya ugonjwa huu huenezwa na mbu na vimelea, na unaweza kuambukizwa wakati wa utotoni na kisha ujitokeze baadaye kabisa tu ukiwa mtu mzima.

4.  Trakoma inayopofusha (Blinding Trachoma)

 Trakoma inayopofusha ni maambukizi ya macho ya kibakteria ambayo husababisha upofu. Ndio sababu kuu inayoongoza ya kusababisha upofu wa kuambukizwa ulimwenguni kote, na pia ni sababu ya pili kuu ya upofu kiujumla. Ugonjwa huu unaenea kupitia kugusana moja kwa moja na watu ambao wameambukizwa, na pia kupitia kwa nzi. Ikiwa haijatibiwa, ngozi inayoshikilia kope machoni hugeuka ndani na kisha kope kukwaruza katikati ya jicho (sehemu ya ‘cornea’) na kusababisha maumivu makali na usumbufu mwingi, na mwishowe upofu. Zaidi ya watu milioni 142 walioathirika wanahitaji matibabu.

5.  Upofu wa macho unaosababishwa na wadudu wa kwenye mto (River Blindness)

Ugonjwa wa upofu wa macho usababishwao na wadudu kwa kwenye mto, ujulikanao pia kama ‘Onchocerciasis,’ ni maambukizi ya macho na ngozi ambayo husababishwa na vimelea  vinavyosambazwa na kuumwa na nzi mweusi. Nzi mweusi huishi na kuzaliana kwenye mito mikubwa na midogo midogo, na hapo ndipo pia ugonjwa huu hupatikana na umepatiwa jina hilo. Ingawa ugonjwa huu unasababisha upofu kwa kiwango kidogo kuliko trakoma, kuna zaidi ya watu milioni 217 wanaohitaji matibabu ya ugonjwa huu duniani.

Wanawake na wasichana wanaathiriwa zaidi na magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika

Kulingana na ripoti ya mwaka 2016 ya Kuungana ili Kupambana na Magonjwa ya Kitropiki Yaliyosahaulika, theluthi-mbili ya ukusanyaji/uchotaji wa maji hufanywa na wanawake na wasichana. Hii inawaweka katika hatarii kubwa sana ya kupatwa na magonjwa ya kitropiki yapatikanayo kwenye maji. Wanawake na wasichana mara nyingi huchukuliwa kama watunza mji, na hii inaweza kuwasababishia kukosa: elimu, ajira, maisha, na afya.

Jinsia pia inachangia katika jukumu la upishi na usafishaji; wanawake ulimwenguni  kote mara nyingi hupewa majukumu ya nyumbani, ambayo hayathaminiwi na huwatia hatarini zaidi katika kuambikizwa  magonjwa ya kitropiki: Utumiaji mkubwa magonjwa ya kitropiki.


UNAWEZA PIA KUSOMA:

- MAJI YASIYO NA VIJIDUDU YANAWEZA KUTOKUWA SALAMA KWA KUNYWA

- MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA UNAPOPEWA MAJIBU YA VIPIMO KUTOKA MAABARA


Nchini Tanzania watu milioni 16 tayari wanapokea matibabu ya magonjwa ya kichocho, trakoma, matende, na upofu unasababishwa na wadudu wa kwenye mito, bado watu milioni 9 kiujumla wanahitaji dawa na matibabu.

Katika juhudi za kumaliza magonjwa ya kitropiki yaliyopuuzwa. Mwaka 2020, zaidi ya vijana 150 walikusanyika Dar es Salaam, Tanzania kujadili jinsi ya kupambana na magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika katika kipindi cha maisha yao, na wakaunda kikundi cha kupambana na kutokomeza magonjwa haya kwa kizazi hiki kiitwacho: End Neglect and Commit to an NTD-Free Generation.

Itakumbukwa, serikali ya Tanzania kupitia  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau mwaka 2018 ilifanya kampeni ya kugawa dawa za Kingatiba ya magonjwa ya minyoo ya tumbo, usubi, trakoma, matende na mabusha katika mikoa saba (7) hapa nchini, ambayo ni Dar es Salaam katika Manispaa zote, Iringa wilaya ya Mufindi DC, Mtwara wilaya ya Masasi, Pwani wilaya ya Kibaha na Mafia, Rukwa wilaya ya Kalambo, Songwe wilaya ya Songwe na Tanga wilaya ya Mkinga na Korogwe. Lengo kuu la kufanya kampeni ni kutibu na kuzuia maambukizi ya magonjwa ya minyoo ya tumbo, Usubi, Trakoma, Matende na mabusha au Ngirimaji.

Pindi  jamii zinapokuwa na viwango vya juu vya maambukizi na au ulemavu unaotokana na  magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika, watu na jamii kwa ujumla hutumia fedha nyingi, nguvu na akili ili kuyakabili maradhi haya.  Matibabu ya magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika ikiwa hayapatikani katika eneo hilo inaweza kusababisha gharama kubwa na kuletea familia shida za kifedha.

Watu wazima wanaofanya kazi ambao wanapata magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika hawawezi tena kufanya kazi zao, na hii inaweza kuathiri mapato ya familia zao kwa ukosaji wa ada ya shule, kodi, vyakula na kadhalika. Watoto ambao wanakabiliwa na maumivu sugu ya magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika pia wanaweza kushindwa kuhudhuria masomo yao shuleni kwa  muda wa wiki hadi miezi, na kuwa na wakati  mgumu sana wa kumaliza masomo kulingana na ratiba ya masomo, na vile vile hupata ugumu kupata marafiki lakini pia kushiriki katika jamii zao.

Magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika yanaweza kubebesha jamii mzigo na gharama kubwa za kiafya, maumivu sugu na kutokuwa na uwezo wa kufanya kazi. Katika jamii ambazo umasikini umeenea na upatikanaji wa huduma bora za afya ni mdogo, utunzaji wa wagonjwa unaweza kuwa mgumu na kupunguza fursa za watu kuepuka umaskini kupitia kazi na elimu, au kwa maneno mengine, kupaa/kufanikiwa kimaisha.

Sio magonjwa yote ya kitropiki yaliyosahaulika husababisha kifo. Ingawa magonjwa haya mengi yanaweza kusababisha ulemavu mkali/ wa kudumu, mengine yanaweza kuwa na athari nyepesi au hata dalili tu. Kinga ni njia bora ya kutokomeza magonjwa ya kitropiki yaliyopuuzwa, lakini matibabu yanaweza kusaidia sana kudhibiti dalili na maumivu yanayosababishwa na magonjwa haya.