Afrika

Jeshi la Ethiopia Kuanza Operesheni ya Mwisho Kuchukua Mji Mkuu wa Jimbo la Tigray

Hatua hii imetangazwa na Waziri Mkuu Ahmed Abiy, kufuatia miji mingine yote iliyokuwa chini ya waasi kuangukia mikononi mwa serikali.

Waziri mkuu wa Ethiopia, Amhed Abiy ameamuru vikosi vya kijeshi vya taifa hilo kuanzisha "shambulio la mwisho" kwenye mji mkuu wa jimbo la Tigray, kufuatia amri ya kujisalimisha ndani ya muda saa 72 aliyotoa kwa viongozi wa eneo hilo kumalizika.


Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, Abiy Ahmed alisema uangalifu mkubwa utachukuliwa kulinda raia wasio na hatia dhidi ya madhara na akasema juhudi zitafanywa na wanajeshi wa serikali kuhakikisha mji wa Mekelle, ambao una idadi ya watu 500,000, "hauharibiki vibaya ”.

"Tunatoa wito kwa watu wa Mekelle na viunga vyake kuweka silaha kando, kukaa nyumbani na kukaa mbali na malengo ya kijeshi na kutimiza wajibu wao katika kupunguza uharibifu unaoweza kuendelea kwa sababu ya watu wachache wahalifu," Ahmed alisema.


Mapema wiki hii, maafisa wa jeshi walionya juu ya "kutokuwa na huruma" ikiwa wakaazi wa Mekelle hawatajitenga na  uongozi wa jimbo hilo chini ya chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF), kikiwa ni chama tawala cha eneo hilo.


Debretsion Gebremichael, kiongozi wa TPLF, alisema Jumanne watu wake walikuwa "tayari kufa" wakitetea nchi yao.

Abiy alizindua kampeni ya kijeshi dhidi ya TPLF mnamo 4 Novemba, akiishutumu kwa kushambulia kambi za jeshi za serikali katika mkoa wa kaskazini na kusema kampeni hiyo inakusudia kuleta hali ya utulivu nchini Ethiopia.


Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 44, ambaye alishinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka jana kutokana na makubaliano yake ya amani na nchi jirani ya Eritrea, alisema TPLF ilikuwa imepanga "idadi kubwa ya mashambulio ya vurugu" kote Ethiopia "ili kukomesha mchakato wa demokrasia".


Katika wiki mbili zilizopita, majeshi ya Ethiopia yamekuwa yakishambulia miji mbalimbali katika jimbo hilo la kaskazini na kuiweka chini ya ulinzi, na mji wa Mekelle ambao ni ngome ya mwisho ya waasi unatarajiwa kuwa anguko la mwisho la utawala wa Watigrei ambao ni wachache, huku wakiwa walishikilia uongozi wa taifa hilo katika miongo minne iliyopita.